KAMAU: Viongozi tunaowachagua ni picha halisi ya jinsi tulivyo
Na WANDERI KAMAU
JAMII husawiriwa na aina ya viongozi inaowachagua.
Huu ndio uhalisia mkuu alioangazia marehemu Prof Ken Walibora alipoandika tamthilia ‘Mbaya Wetu’.
Kwenye tamthilia hiyo, Prof Walibora anaonyesha jinsi jamii inavyowapenda na kuwatetea viongozi wao, hata ikiwa wanahusishwa na vitendo vya utovu wa maadili.
Na si Prof Walibora pekee ambaye amezamia suala hili kwenye kazi zake, bali wasomi na waandishi wengi wameliangazia kwa karne nyingi zilizopita.
Historia pia imeonyesha kuwa ustawi wa nchi katika nyanja zote huathiriwa pakubwa na aina ya viongozi wanaochaguliwa.
Ni kwa mantiki hiyo ambapo narejelea mdahalo mkali ambao umeibuka kumhusu mbunge Babu Owino (Embakasi Mashariki), kutokana na ripoti ya kutamausha iliyoibuka kuhusu hali ya afya ya barobaro Felix Orinda, maarufu kama ‘DJ Evolve’.
Bw Owino aliripotiwa kumpiga risasi mtumbuizaji huyo katika klabu moja jijini Nairobi katika hali ya kutatanisha mnamo Januari.
Ingawa mwathiriwa amekuwa akipata matibabu hospitalini, ni hadi Jumatatu wiki hii ambapo umma ulifahamu vizuri hali yake, kutokana na taarifa iliyopeperushwa na runinga ya NTV.
La kutamausha ni kuwa, barobaro huyo alipoteza uwezo wake wa kuzungumza. Haeleweki kuhusu anayoyasema. Hasikiki. Anazungumza tu maneno yanayomtoka kinywani, ambapo inamlazimu anayewasiliana naye kuwa makini kuelewa anavyosema.
Bila shaka, hakuna kitendo cha kutamausha kama hicho, kwani maisha ya barobaro huyo yaligeuka ghafla mara tu baada ya mkasa huo.
Na ingawa Wakenya wameanza mchakato wa kukusanya saini kushinikiza haki kufanyika kwa mwathiriwa, uhalisia wa tukio hili unajikita kuhusu aina ya viongozi tunaowachagua.
Si mara moja ambapo viongozi wenye nyendo za kutiliwa shaka wameibuka washindi kwenye chaguzi mbalimbali.
Wakati mwingine, huwa hata wanatetewa na watu wao kwamba “wanaonewa” kila juhudi za kuwaadhibu zinapoanza.
Huu ni mtindo ambao umetuzalia viongozi ambao ni wezi, wauaji, wafisadi, wanyakuzi wa ardhi na walanguzi wa mihadarati.
Ni kinaya kwa Wakenya kuanza kulalamika kuhusu kitendo cha Bw Owino, ilhali yeye ni mbunge aliyechaguliwa na watu na ni ‘kipenzi’ cha watu.
Tukio hili la kusikitisha bila shaka linapaswa kuwafungua macho wananchi kuwa, uhalisia wa kimaadili kuihusu jamii huonekana kupitia kwa viongozi wanaochaguliwa nayo.
Ni kwa sababu hiyo ambapo viongozi maarufu kama Winston Churchill (Uingereza) ama Lee Quan Yew (Singapore) huwa wanarejelewa kutokana na michango waliotoa kwenye nchi zao. Tuzinduke!