KAMAU: Wakati ni sasa hivi kwa Rais kujiandikia historia
Na WANDERI KAMAU
ALIPOTOA hotuba yake Jumanne kwenye sherehe za Sikukuu ya Mashujaa katika Kaunti ya Kisii, mojawapo ya mambo aliyoyarejelea sana Rais Uhuru Kenyatta ni mchango wa vizazi vilivyopita katika ukombozi wa Afrika.
Rais alirejelea kwa kina nyakati tofauti ambapo mashujaa hao walijituma kuhakikisha Afrika imejikomboa dhidi ya udhalimu wa wakoloni.
Bila shaka, hotuba hiyo ilikuwa kumbukizi maalum kwa mchango ambao vizazi hivyo vilitoa, kwani ndoto zao zilikuwa kuona Afrika imepata uhuru kamili kwa kujisimamia na kuendesha mipango yake bila mwingilio wa namna yoyote ile kutoka kwa wageni.
Hili linaonyesha wazi Rais na viongozi wengine wanafahamu safari ndefu ambayo Afrika imepitia kufikia ilipo.
Hata hivyo, mkasa mkuu ni kuwa licha ya ufahamu huo, viongozi wengi wanaonekana kutojali namna vitendo vyao vitarejelewa ama kukumbukwa na vizazi vijavyo.
Kwa mfano, ingawa tawala za marais Mzee Jomo Kenyatta, Daniel Moi na Mwai Kibaki zilikumbwa na matatizo kama ufisadi, uovu huo umeongezeka maradufu tangu serikali ya Jubilee ilipochukua mamlaka mnamo 2013.
Kumekuwa na makumi ya sakata za ufisadi ambazo zimefichuliwa tangu 2013, ingawa serikali bado haijaonyesha makali yake kwenye juhudi hizo.
Ilivyo sasa, Rais Kenyatta anaonekana kuwa mbioni kuhakikisha ametimiza baadhi ya ahadi alizotoa kwa Wakenya kwenye kampeni za 2017, kwani imebaki miaka miwili pekee ang’atuke uongozini.
Rais amekuwa akikosolewa pakubwa kwa kutoa ahadi hewa, kwenye juhudi za kukabiliana na ufisadi.
Mfano halisi ni makataa ya siku 21 alizotoa kwa Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI), Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma (DPP) na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) Agosti, kuwachunguza wale waliotajwa kuhusika kwenye uporaji wa fedha zilizotolewa kuisaidia Kenya kukabili janga la virusi vya corona.
Licha ya agizo hilo, idara zilisema itachukua muda zaidi kuwakabili watu hao, kwani utaratibu huo unajumuisha kukusanya ushahidi wa kutosha kutoka kwa mashahidi na stakabadhi mbalimbali.
Bila shaka, visingizio kama hivyo ndivyo vimekuwa vikitolewa kila mara wakati sakata ya ufisadi inapojitokeza na kuwahusisha watu wenye ushawishi serikalini.
Taasisi husika huwa zinajivuta na kutoa kila aina ya visingizio ili kuchelewesha uchunguzi kimakusudi.
Baadaye, suala jingine huibuka na kuwateka Wakenya ambapo huwa wanasahau kuhusu sakata husika.
Mtindo huo ndio umeipaka tope serikali ya Rais Kenyatta na kuifanya kutajwa miongoni mwa zile zilizoshindwa kabisa kulikabili zimwi la ufisadi.
Rais Kenyatta pia amekuwa akilaumiwa kwa kuongeza deni la nje, ambapo kufikia sasa, Kenya inakisiwa kuwa na deni la zaidi ya Sh6 trilioni.
Ikiwa imebaki chini ya miaka miwili kabla ya 2022, ni wakati Rais Kenyatta azingatie kauli ya hotuba yake—kwa kujenga msingi ambapo atakumbukwa na vizazi vijavyo kwa mchango aliotoa kwa maendeleo ya nchi.
Asipotumia vyema muda huo, Rais yuko kwenye hatari ya kukumbukwa kama kiongozi ‘aliyewaangusha’ Wakenya katika kila nyanja.