Makala

KAMAU: Wanawake waungane kukabili tamaduni duni

December 1st, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na WANDERI KAMAU

HAPANA shaka yoyote kuwa kwa miaka mingi duniani, mwanamke amekuwa akitengwa na wanaume katika masuala muhimu kama siasa na uongozi.

Licha ya dunia kushuhudia maendeleo na ustawi mkubwa katika nyanja mbalimbali, baadhi ya jamii bado zinaendeleza dhana za kikale kumhusu mwanamke kama kiumbe dhaifu.

Hivyo, nyingi zinaamini kwamba mwanamke kamwe hafai kushiriki katika suala lolote la uongozi, hasa siasa.

Jamii nyingi huchukulia hali hiyo kama “uvurugaji” wa jinsi mpangilio wa kijamii unavyopaswa kuwa.

Kwa dhana kama hizo, wanaume wengi wanaamini kuwa wanawake ni viumbe wa “kiwango cha chini” ambao kando kuwa wasaidizi wao, majukumu yao ni kama kuwapikia, kuwachunga na kuwalea watoto, kushiriki kazi kama kilimo, kutafuta kuni kati ya mengine.

Mpangilio wa kimaisha wa jamii hizo unaifanya hata iwe mwiko kuwa mwanamke anaweza “kumpita” mwanamume katika jukumu lolote lile.

Mkasa mkuu ni kuwa, kutokana na kuwepo katika mazingira hayo kwa muda mrefu, wanawake wengi katika jamii hizo wamekubali uhalisia huo.

Bila shaka, huu ni uhalisia mchungu ikizingatiwa dunia kwa sasa ipo katika enzi ambapo teknolojia imegeuka kuwa nguzo muhimu sana katika maisha ya leo.

Tu katika enzi ambapo wanawake wanapigania na kutwaa uongozi wa nchi zenye uwezo mkubwa duniani kama Amerika, Ujerumani, Uingereza kati ya mengine.

Nchini Amerika, Bi Kamala Harris ataandikisha historia kwa kuwa Makamu wa Rais wa kwanza mwanamke asiye asili ya Kizungu tangu nchi hiyo kujinyakulia uhuru wake mnamo 1776 .

Hilo ni baada yake na Rais Mteule, Joe Biden, kuapishwa rasmi hapo Januari 20, 2021.

Nchini Ujerumani, taifa limeshuhudia ukuaji mkubwa wa kiuchumi na uthabiti wa kisiasa tangu Bi Angela Merkel alianza kuhudumu kama Chansela mnamo 2005.

Chini ya uongozi wake, Merkel ameiwezesha Ujerumani kuibukia miongoni mwa nchi zinazotazamwa duniani kuhusu namna zinavyoendesha sera zake, kwa mfano juhudi za kukabili janga la virusi vya corona.

Viongozi wengine wanaoendelea kupiga hatua kubwa ni Bi Arlene Foster, anayehudumu kama Waziri Mkuu wa North Ireland tangu Januari mwaka huu.

Bila shaka, mifano hiyo, kati ya mingine, inapaswa kuwafungua macho wanawake barani Afrika na kwingineko duniani kuwa juhudi zao pekee ndizo zinaweza kuwakomboa dhidi ya tamaduni na dhana zinazowadhalilisha kila mara.

Licha ya juhudi nyingi kuhakikisha usawa wa kijinsia katika uwakilishi kwenye nyanja mbalimbali nchini, ni jukumu lao kujituma na kupambana na wanaume wanapong’ang’ana kutwaa nyadhifa hizo.

Hilo ndilo liliwawezesha marais wa zamani wanawake kama Ellen Johnson Sirleaf (Liberia), Catherine Samba (Jamhuri ya Afrika ya Kati) na Joyce Banda (Malawi) kutwaa urais katika nchi zao.

Hivyo, wakati dunia nzima inaadhimisha siku 16 dhidi ya dhuluma za kijinsia, ni wakati wanawake wafahamu ikiwa hawatajipigania wenyewe, basi watabaki kama “mateka” na watumwa wa kitamaduni kama ilivyo katika baadhi ya jamii.

Ni wakati wazinduke!

[email protected]