Kampuni 3 zinazohusishwa na Gachagua ambazo hazijasajiliwa
KAMPUNI zilizotajwa katika hoja ya kumtimua Naibu Rais Rigathi Gachagua zilisajiliwa kati ya 2001 na Januari 2024, rekodi rasmi zinaonyesha.
Rekodi zinaonyesha kuwa kampuni hizo zina afisi zao jijini Nairobi katika Barabara ya Ikulu, Lang’ata, katikati mwa jiji na makazi rasmi ya Naibu Rais huko Karen.
Kampuni hizi zitakuwa ushahidi katika mchakato unaoendelea wa kumuondoa Rigathi Gachagua kutoka wadhifa wa Naibu rais, ambaye hujigamba kuwa ‘msema ukweli’ lakini alionekana kujipalilia makaa alipokiri hadharani kuwa familia yake inamiliki baadhi ya kampuni zilizotajwa.
Uchunguzi wa Taifa Jumapili, umegundua kuwa kampuni tatu kati ya 22 zinazohusishwa na naibu rais hazina rekodi katika ofisi ya msajili.
Lakini mmiliki wa kampuni hizo 19 ni Naibu Rais Rigathi Gachagua na mkewe Dorcas Wanjiku Rigathi na wanawe wawili, Kevin Gachagua na Keith Ikinu.
Suala moja ambalo linaweza kuibuliwa wakati wa hoja ya kumtimua ni iwapo ni halali kwa afisa wa umma kusajili kampuni za kibinafsi kwa kutumia makazi rasmi kama ofisi.
Uchunguzi unafichua kuwa kampuni mbili kati ya hizo zinahudumu kutoka kwa makazi rasmi ya naibu rais na kampuni ya tatu imesajiliwa kuhudumu kutoka Harambee House Annex, ambayo ni afisi ya naibu rais.
Kulingana na rekodi rasmi kutoka kwa msajili wa kampuni, naibu rais ni mkurugenzi wa Grand Bypass Apartments Limited, ambayo inamilikiwa na Vipingo Beach Resort Limited. Wakurugenzi wengine katika Grand Bypass Apartments ni John Mwai Mathenge na Peter Njoroge Regeru.
Kampuni hiyo ilisajiliwa Januari 11, mwaka huu. Rekodi hizo pia zinaonyesha kuwa mke wa naibu rais, Bi Dorcas Wanjiku Rigathi anamiliki kampuni ya Spirit Way Ltd, ambayo ilisajiliwa Novemba 14, 2023, mwaka mmoja baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2022. Bibi Rigathi anamiliki hisa zote 100 za kampuni hiyo. Ofisi iliyosajiliwa ya kampuni hiyo iko katika jengo la Fortis Suites lililoko kwenye Hospital Road Upper Hill, Nairobi.
Fortis Vis Group Limited inamilikiwa na wanawe Bw Gachagua, Kevin na Keith, ambao kila mmoja ana hisa 50 katika kampuni iliyosajiliwa mnamo Februari 14, 2023.
Ni mojawapo ya kampuni zinazofanya kazi kutoka makazi rasmi ya naibu wa rais kulingana na rekodi kutoka kwa msajili wa kampuni