Makala

Kampuni ya bwanyenye aliyehusishwa na SHA yahusika na masaibu ya bima ya walimu

Na DAVID MUCHUNGUH February 12th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

JAYESH Umesh Saini ndiye mmiliki wa Medical Administrators (K) Ltd (MAKL) na Bliss Healthcare (K) Ltd, ambazo zinahusishwa na utata wa bima ya matibabu ya walimu ya kima cha Sh55 bilioni, Taifa Leo inaweza kufichua.

Kampuni hizo mbili ambazo zina mizizi katika Umoja wa Milki za Kiarabu zina mchango mkubwa katika mpango wa bima ya afya ya walimu ya Sh55 bilioni, ambayo hivi majuzi ilizua utata baada ya baadhi ya hospitali kuondoa huduma kwa walimu zikitaja malimbikizi ya malipo.

Mpango huo wa matibabu unasimamiwa kupitia muungano wa kampuni za bima ambazo zinaongozwa na Minet Kenya Insurance Brokers Limited kama mwanachama mkuu wa muungano na mratibu.

MAKL hufanya kazi kama msimamizi wa mpango huu wa matibabu na ina jukumu la kuteua hospitali zinazotoa huduma za matibabu kwa walimu na malipo ya bili zao.

Bliss Healthcare ndio mwezeshaji mkuu na ina mtandao wa kliniki 63 kote nchini. Inasimamia utoaji na kandarasi na kutia saini ushirikiano na hospitali zinazotoa huduma ambazo hazipatikani kupitia MAKL.

MAKL ilianzishwa Desemba 7 2018. Inamilikiwa na Bliss Healthcare (K) Ltd, ambayo inamiliki hisa zake zote 1,000. Madni Ali Asif Ansari ameorodheshwa kama mkurugenzi pekee wa MAKL, huku Lenah Chelangat akiorodheshwa kama katibu wa kampuni.

Bliss Healthcare (K) Ltd ilianzishwa Desemba 6 2019. Kampuni hiyo inamilikiwa na Bliss Healthcare and Administrators LLC iliyosajiliwa  UAE, ambayo inamiliki hisa zote 1,000. Bw Ansari ndiye mkurugenzi wa pekee wa kampuni hiyo UAE.

Alipokuwa akimshtaki mwanaharakati Nelson Amenya nchini Ufaransa, Bw Jayesh Saini alijitambua kama mmiliki wa Bliss Healthcare, ambayo alisema ina kliniki zaidi ya 60 kote nchini Kenya, na Dinlas Pharma, ambayo ilihusika na  uagizaji wa chanjo ya Covid-19 aina ya Sputnik V kutoka Urusi.

Bw Saini pia amehusishwa na mojawapo ya kampuni zinazohusika na mfumo wa kidijitali wa kima cha Sh104.8 bilioni ambao muungano unaoongozwa na Safaricom PLC unatoa kwa serikali chini ya Mamlaka ya Afya ya Kijamii (SHA).

Kampuni zingine katika muungano huo ni Apeiro Ltd, kampuni inayomilikiwa na familia ya kifalme ya UAE, na Konvergenz Network Solutions ya Kenya.

Rufus Marundu Maina, mkurugenzi katika kampuni zingine zinazohusiana na Bw Saini kama vile Lifecare Hospitals, anashikilia nyadhifa sawa katika kampuni mbili zilizojumuishwa na Apeiro katika mpango huo wa Sh104.8 bilioni. Bw Maina ni mkurugenzi katika Apeiro Kenya Technologies Ltd na SIH Africa Ltd. SIH Africa inamiliki hisa zote 1,000 katika Apeiro Kenya Technologies Ltd.

Wakurugenzi wa Apeiro Kenya Technologies Ltd, wasio na hisa zozote, ni Bw Maina, Inder Deep Singh Virdi, Judy Mwende Gatabaki, na Aswanth Bindhu Lambodaran. Bi Gatabaki ni mtaalamu wa IT na mke wa David Ndii, mmoja wa washauri wa Rais Ruto awa masuala ya kiuchumi.

Katika SIH, Bw Lambodran na Nishant Mishra wanamiliki hisa 500 kila mmoja, kwa uaminifu. Bw Maina ni mkurugenzi katika kampuni hiyo, lakini hana hisa.