KAMUGISHA: Uzee ni mtihani, kila mtu hutaka kuishi miaka mingi ila hakuna atakaye kuitwa mzee
NA FAUSTIN KAMUGISHA
KUNA methali ya taifa la Iceland isemayo kuwa, kila mmoja anataka kuishi maisha marefu, lakini hakuna anayetaka kuitwa mzee.
Katika maisha utajitahidi kula mlo kamili, kufanya mazoezi, kupumzika, kujitunza vizuri kwa muda wa miaka sitini mwisho wa siku, funga fungua uzee unaingia. “Uzee hasa uzee unaoheshimika, una mamlaka makubwa, na una thamani kubwa kuliko raha zote za ujana,” alisema mwanafalsafa Cicero.
Mtunga-zaburi aliimba hivi kuhusu wazee waaminifu: “Bado wataendelea kustawi wakati wa kuwa na kichwa chenye mvi, wataendelea kuwa wanono na wabichi” (Zaburi 92:14).
Licha ya utukufu wa uzee, uzee ni mtihani. Katika uzee watu wanapoanza kusema kuwa unaonekana kama kijana ni namna nyingine ya kusema umezeeka. Katika uzee unaona kila kitu gharama iko juu. Katika uzee ni kama watu wanaongea kwa sauti ya chini. Katika uzee unagundua herufi za maneno katika gazeti ni ndogo hazisomeki vizuri. Katika uzee unaona mabasi yanaanza safari asubuhi na mapema sana. Katika uzee inakuchukua muda kuwatambua wanadarasa na wao kukutambua, wamebadilika na wewe umebadilika. Katika uzee unaona watoto wanaanza shule wakiwa wadogo mno kuliko nyakati zako.
Uzee kadiri ya Kamusi Kuu ya Kiswahili ni hali ya kuwa na umri mkubwa kwa kuishi miaka mingi. Kadiri ya Kamusi ya Karne ya 21 uzee ni hali ya kuzeeka. Kuzeeka ni kuingia katika umri mkubwa na kupungukiwa na nguvu na uwezo. Uzee una maana tofauti kwa watu tofauti.
Jane Ellen Harrison anaona uzee kama kuondoka kwenye jukwaa na kukaa kama mtazamaji na ukiwa umetimiza wajibu wako katika maisha na kutoa mchango wako katika jamii utaridhika kukaa chini na kutazama.
Maggie Kuhn anaona uzee kuwa si ugonjwa bali ushindi dhidi ya misukosuko ya aina yote, ni ushindi dhidi ya majaribu na mambo ya kukatisha tamaa. Kuna aliyesema kuwa uzee ni wakati ambao unajua majibu yote lakini hakuna anayekuuliza swali. Mimi kwangu uzee ni mtazamo. Unaweza kuwa kijana ukawa na fikra za kizee na unaweza kuwa mzee ukawa na fikra kama kijana.
“Mtu hajazeeka mpaka majuto yanapochukua nafasi za ndoto,” alisema John Barrymore.
Ili usije kujuta ukiwa mzee katika umri wa ujana na umri wa kati timiza ndoto zako. Katika ujana tabasamu ili katika uzee mifunyo kwenye uso ikuonyeshe tabasamu zilipokuwa. Licha ya ukweli huo unaweza kutimiza ndoto zako ukiwa mzee. Historia imebeba ukweli huo.
Mheshimiwa Emmerson Dambudzo Mnangagwa amekuwa rais wa Zimbabwe akiwa na umri wa miaka sabini na tano. Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikuwa mpatanishi mkuu wa pande zilizokuwa zinaasimiana huko Burundi akiwa na umri wa miaka sabini na nne.
Thomas Edison alishughulika sana katika mahabara yake alipokuwa na umri wa miaka themanini na tatu. Mwanasayansi Galileo alifanya ugunduzi wake mkubwa alipokuwa na miaka sabini na tatu.
Benjamin Disraeli alikuwa Waziri Mkuu wa Uingereza kwa mara ya pili alipokuwa na umri wa miaka sabini. John Milton aliandika kazi yake inayoitwa Paradise Regained alipokuwa na umri wa miaka sitini na tatu.
Noah Webster alitunga Kamusi kubwa kama mlima alipokuwa na umri wa miaka sabini. Grandma Moses alichora michoro yake mingi baada ya kufikisha miaka tisini. Giuseppe Verdi alitunga kazi inayoitwa Othello akiwa na umri wa miaka sabini na tatu na wimbo unaoitwa Te Deum akiwa na umri wa miaka themanini na tano.
Katika uzee unaloweza kufanya lifanye. “Tukiwa na miaka ishirini tuna wasiwasi watu wanatufikiriaje. Tukiwa na miaka arobaini hatujali wanachofikiri. Tukiwa na miaka sitini tunagundua kuwa hawakuwa wakifikiria juu yetu hata kidogo,” alisema Jack Falson.
Zuri litende bila kuogopa macho ya watu na bila kuogopa wanachofikiria juu yako.