Makala

Kando na Eliud Kipchoge, wafahamu ‘macelebs’ waliowahi kukaangwa na Wakenya mitandaoni

February 13th, 2024 2 min read

NA WANDERI KAMAU

SHUTUMA ambazo bingwa wa mbio za marathon, Eliud Kipchoge, ameelekezewa na Wakenya kwenye mitandao ya kijamii kufuatia kifo cha mwanariadha Kelvin Kiptum, zimeibua kumbukumbu za matukio kama hayo yaliyowahi kuwakumba watu maarufu nchini hapo awali.

Mnamo Jumatatu, Kipchoge alielekezewa kila aina ya lawama, baadhi ya Wakenya wakisema kuwa alichelewa kutuma ujumbe wa rambirambi kwa familia ya Kiptum.

Pia, baadhi yao walidai kuwa hakutoa ujumbe wa kumpongeza alipovunja rekodi ya Mbio za Marathon za Chicago, nchini Amerika, Oktoba 8, 2023.

Ijapokuwa Kipchoge ni mtu maarufu, ambaye ameiletea Kenya sifa kem kem hapo awali kutokana na ushindi wa mbio hizo katika sehemu tofauti duniani, Wakenya hawakukumbuka hilo, bali walimwelekezea kila aina ya lawama.

Baadhi ya ‘macelebs’ wengine ambao washawahi kujipata katika hali hiyo ni wanamuziki Jimmy Gait, Samidoh, mwanasiasa Phelix Odiwuor (Jalang’o), Seneta Maalum Karen Nyamu, Rais William Ruto, wanamuziki Bahati, Willy Paul kati ya wengine wengi.

Mnamo 2016, mwanamuziki Jimmy Gait alijipata pabaya, baada ya Wakenya kumkosoa kutokana na wimbo ‘Yesu Ndiye Sponsor’. Wengi wakisema kuwa wimbo huo ulimkejeli Mungu.

Kinaya ni kuwa hapo awali, mwanamuziki huyo alikuwa ametoa nyimbo maarufu zilizopendwa na mashabiki wake kama vile ‘Muhadhara’, ‘Wakati wa Kubarikiwa’, ‘Huratiti’ kati ya nyingine nyingi.

Kwenye mahojiano, alisema kuwa lawama alizoelekezewa ni moja ya sababu zilizomfanya kuacha muziki.

“Wakenya walisahau nyimbo zote nzuri ambazo nilikuwa nimewafanyia na kuamua kunishambulia kutokana na wimbo mmoja ambao hawakuelewa maana yake kwa undani,” akasema huku akibubujikwa na machozi kwenye runinga moja.

Baada ya mkewe, Edday Nderitu, kutangaza kuhamia nchini Amerika mwaka uliopita, mwanamuziki Samuel Muchoki, maarufu kama ‘Samidoh’ alijipata pabaya machoni mwa mashabiki wake, wengi wakimlaumu kwa kushindwa “kudhibiti familia yake”.

Lawama hizo zilitokana na uhusiano ambao amekuwa nao na Seneta Karen Nyamu. Wawili hao wana watoto wawili.

Mashabiki wa mkewe walimwita kila aina ya majina, wakisema ni mwiko katika jamii za Kiafrika mume kumtupa mkewe wa kwanza kutokana na mahusiano yasiyo rasmi anayoweza kuwa nayo na mwanamke mwingine.

Hadi sasa, Edday bado yuko nchini Amerika na watoto wake.

Kinaya ni kuwa, mashambulio hayo ni licha ya nyimbo nzuri na maarufu ambazo mwanamuziki huyo ametoa, kama vile ‘Nairobi City’.

Mwanasiasa, mcheshi na mtangazaji wa redio Jalang’o amekuwa akijipata pabaya kwenye mitandao ya kijamii, baada ya wafuasi wa chama cha ODM kumlaumu kwa “kumsaliti” kisiasa kiongozi wa chama hicho, Bw Raila Odinga.

Hili lilifuatia mkutano aliofanya na Rais William Ruto katika Ikulu ya Nairobi, Septemba mwaka uliopita.

“Wewe ni msaliti. Umemsaliti ‘Baba’! Hatukutaki ODM!” wakafoka baadhi ya mashabiki wake.

Kinaya ni kuwa, mwanasiasa huyo, ambaye ni mbunge wa Lang’ata, alikuwa miongoni mwa watu maarufu zaidi, hasa katika eneo la Nyanza kutokana taaluma yake ya utangazaji.

Vivyo hivyo, Rais Ruto pia amejipata lawamani, baadhi ya Wakenya wakionekana kughadhabishwa na sera ya serikali yake kuwaongezea ushuru.

Wakenya wengi wamempa jina la kupanga ‘Zakayo’ kutokana na sera hiyo ya kuwaongezea ushuru.

Hata hivyo, amesisitiza lawama hizo hazitamwathiri hata kidogo.