• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 3:31 PM
Kang’ata aiga Gachagua akiahidi kutuza wakulima wa maembe na maziwa unga na mafuta ya kupikia

Kang’ata aiga Gachagua akiahidi kutuza wakulima wa maembe na maziwa unga na mafuta ya kupikia

NA MWANGI MUIRURI 

GAVANA wa Murang’a Irungu Kang’ata ameonekana kufuata nyayo za Naibu Rais, Rigathi Gachagua ambaye amekuwa akituza wapiga kura wa eneo analotoka kwa bidhaa za kula kama njia kutekeleza ahadi yake kwamba atachunga WanaMlima Kenya kama maziwa motoni.  

Kabla ya kutwaa serikali 2022 pamoja na Rais William Ruto, kama Rais na Naibu Rais, Bw Gachagua aliahidi atakuwa akiwapa wenyeji wa Kati mchele na nyama, jambo ambalo ametimiza.

Akiashiria kufuata mkondo huo, Gavana Kang’ata ametangaza kuwa atakuwa akiwapa wakulima wa maembe Murang’a na wa wafugaji wa ng’ombe wa maziwa, unga na mafuta ya kupika kama njia ya kuwasaidia kupata faida.

Busara ya Kang’ata ni kwamba, wakulima hao wakipata malipo yao baada ya kuwasilisha bidhaa zao sokoni, ikiwa wataondolewa mzigo wa kujinunulia unga na mafuta ya kupikia basi watabakia na pesa mfukoni.

Kupitia taarifa, Gavana huyo amesema kwamba mpango wake wa awali kuwapa wakulima hao pesa taslimu umeingiwa na dosari na utaandaliwa upya kupitia fidia mbadala ikiwemo ile ya kuwatuza kwa unga na mafuta.

Katika mpango wa awali ambao Dkt Kang’ata alikuwa amezindua Aprili 2, 2023, kila mkulima wa maziwa aliyejisajili alikuwa akipata Sh3.50 kwa kila lita aliyowasilisha kwa chama cha ushirika, naye anayekuza maembe akipata Sh7 kwa kila kilo aliyowasilisha kwa kampuni za ununuzi.

Lakini baada ya kutekeleza mpango huo kwa mwaka mmoja sasa, Gavana Kang’ata amelia kwamba umeingiwa na dosari na kuhitaji marekebisho ya kuulainisha.

Amesema kwamba mpango huo mpya utanufaisha wakulima 41,000 hii ikiwa ni nyongeza ya wakulima 20, 000 ambao wataanza kufaidika kuanzia Aprili 2024.

“Tutaanza kusajili wakulima wapya katika mpango huu na kisha tuzindue misururu ya kushirikisha umma watupe maoni. Hatimaye tutaanza kuwapa wakulima vocha za kujinunulia bidhaa katika maduka ya kilimo na pia ya bidhaa za kinyumbani,” akasema.

Kulingana na takwimu za 2019 kuhusu hesabu ya wakulima wa Murang’a, kuna takribani wakulima 317,459 katika maboma 231,171 wakishiriki mitandao 150 za kilimo.

Murang’a ina wakazi 1.1 milioni katika wadi zote 35.

Bw Kang’ata alisema wakulima hao wakipokezwa vocha hizo, watakuwa huru kufika katika maduka ya uuzaji bidhaa kama pembejeo, chakula cha mifugo, kununua huduma za madaktari wa mifugo “na pia kujinunulia bidhaa za nyumbani kama unga na mafuta ya kupikia”.

Hata hivyo, wengine wameteta kwamba mpango huo unabagua wakulima wengi ikizingatiwa kwamba unahusisha wakulima wa maembe na maziwa pekee na idadi ya walengwa ikiwa 41, 000 pekee ambapo 21, 000 ndio wamekuwa wakinufaika hadi sasa, wengine wakitarajia kuanza kunufaika mwezi wa Mei.

Kabla ya mpango huo, ukumbatie wakulima wote 318, 000 huenda uchukue miaka 16 kuwajumuisha, hili likiwa ni lengo la hadi 2040.

“Na hilo lina maana kwamba kunao watakuwa wamenufaika kwa miaka 16 ambao ni walioanza kupata ruzuku hizo za kaunti, huku watakaokuwa wa mwisho kusajiliwa wakinufaika kwa mwaka mmoja pekee.

“Kang’ata akipata awamu ya pili ataondoka mwaka wa 2032 hivyo basi kuacha wakulima wengine katika orodha ya sintofahamu,” akasema mwenyekiti wa muungano wa wazalishaji maziwa na biashara Bw Martin Kamande.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Mti wa kitamaduni ulioanguka unavyozua hofu  

Kidosho anayetamba kwa kuigiza kwa lugha ya mama

T L