Makala

Kanisa lililodumu kwa miaka 121 hatimaye kufanyiwa ukarabati

Na ELIZABETH OJINA November 27th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

KWA miaka 121, Kanisa Katoliki la St Joseph’s Milimani, Kisumu, limekuwa ushahidi wa mseto wa dini na historia katika eneo la Magharibi mwa nchi.

Kanisa hilo linaweza kuwa ndilo kongwe zaidi. Kwa miaka mingi limestahimili dhoruba za wakati likihudumia maelfu ya waumini wanaomiminika kuabudu hapo kila mwaka.

Kanisa hilo lilianzishwa na Wamishenari wa Mill Hill mnamo 1903, miaka miwili baada ya reli kufika Kisumu.

Wakiongozwa na Padre Nicholas Stam, wamishenari walielekea kijiji cha Bandani, eneo ambalo wafanyakazi wengi wa ujenzi wa reli walikuwa wakiishi.

Misa takatifu ya kwanza

Historia inasema kwamba Misa Takatifu ya kwanza iliadhimishwa ndani ya kanisa hilo Februari 2, 1903.

Desemba 18, 1903, Padre Leonard van den Bergh alifungua rasmi kanisa la kwanza la parokia mjini Kisumu.

Kwa miaka na vikaka, kanisa hili limekuwa parokia iliyozaa nyingine zinazopatikana eneo la Kisumu.

Pia, lilizaa makanisa hadi Mumias (1904), Ojolla na Kakamega (1906) na ndani ya miaka mitatu, kulikuwa na parokia nne Magharibi mwa Kenya.

Leo karibu parokia 64 zimebuniwa kutokana na kanisa hilo la St Josephs.

Mnamo 1908, Padre Luke Plunkett alifungua kituo kingine mjini Nakuru ili kuhudumia Wakatoliki waliokuwa wakifanya kazi katika kituo cha reli katika eneo hilo.

Waumini wakishiriki sala katika kanisa la St Josephs, Milimani, Kisumu. Picha|Maktaba

Kanisa lilipoanza, lilihudumia hasa Wazungu na Wagoa huku kanisa la St Teresa of the Child Jesus Kibuye, Kisumu likihudumia Waafrika.

Kadiri idadi ya waumini wa Kikatoliki inavyoongezeka, ndivyo mahitaji ya nafasi kubwa zaidi ya kuabudu inavyoongezeka.

Hata hivyo, kutokana na hadhi ya kihistoria ya kanisa hilo, jengo haliwezi kubomolewa ili kujengwa jipya.

Chaguo lililopo ni kupanua kanisa ili kushughulikia idadi inayoongezeka ya waumini. Upanuzi wa kwanza ulifanyika baada ya miaka 100 tangu kanisa hilo lilipoanzishwa.

Sehemu ya paa kung’olewa na upepo

Hii ilitokea baada ya sehemu ya paa kung’olewa na upepo. Matokeo yake yalikuwa na kuvuja karibu na altari.

Francis Maangi Nyamango ambaye amekuwa muumini katika Kanisa Katoliki la St Joseph tangu 1973, anasimulia kwamba kulikuwa na mipango ya kulibomoa kanisa zima lakini ilikabiliwa na upinzani.

“Hapo awali, Askofu Mkuu mstaafu Zacchaeus Okoth alikuwa ametoa idhini ya kubomoa jengo hilo na kujenga jipya lakini mapadri wa Mill Hill walipinga hatua hiyo. Walisisitiza kwamba ni lazima jengo la awali la kanisa lidumishwe,” akasema Bw Nyamango.

Kutokana na hali hiyo Parokia iliamua kupanua kanisa ili kutoshe Wakristo wengi zaidi.

“Mnamo 2003 tulifanya upanuzi wa kwanza mdogo kwa sharti jengo la asili la kanisa lidumishwe. Tulikuwa na safu mbili, lakini baada ya upanuzi tulikuwa na safu nne kanisani,” alieleza.

Kulingana na Padri Fredrick Odhiambo, tena mwaka wa 2022, baadhi ya sehemu za paa lilingolewa na upepo.

Krismasi 2022 wakati wa Misa Takatifu

“Ilifanyika Krismasi 2022 wakati wa Misa Takatifu ya kumi na mbili na nusu asubuhi. Kuanzia wakati huo tulifikiri kanisa linahitaji ukarabati mkubwa,” kasema Padri Odhiambo.

Changamoto nyingine waliyokumbana nayo ni idadi kubwa ya waumini waliolazimika kuketi nje ili kuhudhuria misa hasa siku za Jumapili.

“Ilitubidi kuweka madawati nje hasa wakati wa Misa Takatifu ya tatu na ya nne lakini kulikuwa na tatizo wakati wa misimu ya mvua,” alieleza.

Hii ilimlazimu kasisi huyo kuomba ruhusa kutoka kwa Askofu Mkuu wa Kisumu Maurice Muhatia kupanua kanisa.

“Baada ya tafiti, Askofu Mkuu alitoa idhini ya upanuzi wa kanisa na ukarabati. Maagizo yalikuwa kudumisha jengo la zamani bila kuharibu kama madhabahu ya Vatican I,” alisema.

Mwaka huu, mchakato wa kuipa parokia uboreshaji mkubwa unakaribia kukamilika.

Kwanza walipanua sehemu ya nyuma ya kanisa ili kutoa nafasi kwa ujenzi wa ghorofa ya juu ili kutoshea Wakristo wengi zaidi.

Madirisha mapya

Vile vile waliweka madirisha mapya ili kuruhusu hewa zaidi ndani ya jengo.

Kabla ya kupanuliwa kwa kanisa, waumini wapatao 400 wangeweza kuketi kwa misa, lakini sasa watu 1200 wanaweza kuketi.

“Bado tutakuwa na misa nne siku za Jumapili kwa sababu watu wana muda wao wanaoupendelea kuhudhuria ibada za maombi,” alisema.

“Madirisha ya awali yalikuwa madogo; tulidumisha muundo asili wa jengo la kanisa lakini tukaufanya kuwa mkubwa zaidi,” akasema Padri Odhiambo.

Aliongeza kuwa kwa kuwa kuna ukarabati mkubwa unaofanywa, wangetaka kuweka viti vipya.

Huku ukarabati ukiendelea, waumini wanaendelea kuhudhuria misa katika kanisa. Hata hivyo, Jumapili wanafanya ibada nje kwenye mahema.

Kanisa hilo litafunguliwa rasmi tarehe Desemba 7 2024 baada ya ukarabati unaondelea kukamilika.

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA