‘Njoo jinsi ulivyo’: Kanisa linalopokea walevi bila kuwahukumu
KATIKA kijiji tulivu cha Poror, eneobunge la Eldama Ravine, Kaunti ya Baringo, kanisa moja la kipekee linavunja mazoea ya huduma ya kiroho kwa kuwapokea walevi na watumiaji wa dawa za kulevya bila kuwahukumu, kwa upendo, sala na chakula.
Kila Jumapili, waumini wachache hukusanyika si katika kanisa la kifahari, bali kwenye karakana iliyogeuzwa kuwa mahali patakatifu pa kiroho.
Hapa, wale wanaoishi na uraibu wa pombe na dawa za kulevya pamoja na waliotengwa na jamii hupata faraja, uponyaji na tumaini jipya.

Harufu ya supu ya kichwa cha ng’ombe hujaza hewa huku wanaume na wanawake, wengi wakiwa bado katika hali ya kulewa, huinamisha vichwa vyao kuomba, si kwa aibu, bali kwa matumaini ya kupewa nafasi nyingine ya maisha.
“Kanisa si mahakama, bali hospitali kwa wagonjwa,” asema Mchungaji Lawrence Bomet, ambaye hufungua nyumba yake kila Jumapili kuwakaribisha watu wanaopambana na uraibu si kwa mahubiri pekee, bali pia kwa supu, heshima na sababu ya kuamini tena.
Alianzisha Kanisa la Upendo Fellowship mnamo Juni, na ndani ya wiki chache, limekua kwa kasi kutoka kikundi cha watu wachache hadi zaidi ya 50, wakiwemo watoto wanaofika kwa mafundisho kanisani.
Ibada hapa huanza kwa unyenyekevu, si kwa kelele au madoido. Watoto, vijana na wazee huinua sauti zao kwa nyimbo na densi, wakimshukuru Mungu licha ya changamoto walizonazo.
Baada ya nyimbo, ushuhuda hutolewa. Baadhi huomba sala, wengine wanaeleza matatizo yao, akiwemo mshiriki mmoja aliyekamatwa majuzi kwa kuiba mahindi shambani kwa jirani.
Watoto hupelekwa kwenye hema ya karibu kwa mafundisho yao, huku watu wazima wakiendelea na ibada ndani ya karakana hiyo.
“Kanisa si mahakama ya hukumu bali hospitali kwa ajili ya kuponya. Yesu hakuja kwa ajili ya wenye haki, bali kwa ajili ya wenye dhambi,” asema mchungaji Bomet.
Akinukuu maneno ya Yesu kwa Mafarisayo, Mchungaji Bomet aliwakumbusha waumini kuwa ujumbe wa Kristo ni wa rehema, hasa kwa waliokataliwa na jamii.
Kwa nje, huenda hii ikaonekana kama ibada ya kawaida ya Jumapili. Lakini kinachotofautisha ni kuwa wengi wa waumini hapa bado wanapambana na uraibu wa pombe au dawa za kulevya. Hata hivyo, hushiriki kikamilifu kwa kuimba, kusali na hata kutoa sadaka.
Baada ya ibada, waumini hukusanyika nje chini ya anga wazi kushiriki mlo uliopikwa na mchungaji mwenyewe kabla ya kurejea nyumbani.
Huduma hii ya ajabu ilianza kwa swali rahisi ambalo lilimsumbua Mchungaji Bomet kwa muda.
“Kijiji changu kilikuwa na sifa mbaya. Watu wengi waliharibiwa na pombe na maovu mengine. Niliuliza, ‘Ninawezaje kusaidia?’ Nilienda makanisa mengi lakini nikaona pengo kubwa kati ya kanisa na wanaotaabika mitaani,” asema.
Akiwa ameguswa na maandiko na kuona pengo hilo, alizungumza na kaka yake, ambaye pia alikuwa akibugia pombe na akamwomba alete marafiki zake kwa ibada ndogo nyumbani kwake.
Juni 8 mwaka huu ndipo kanisa la Upendo Fellowship lilizaliwa rasmi.
“Nilibadilisha gereji yangu kuwa kanisa na nikawakaribisha – wanaume, wanawake na vijana. Nilipika supu ya kichwa cha ng’ombe na ugali. Baada ya mahubiri ya upendo, tulishiriki chakula. Waliguswa sana. Hakuna aliyewahi kuwahubiria kuhusu neema ya Mungu namna hiyo,” asema.
Mchungaji Bomet hakuishia hapo. Aliona idadi ya waumini ikiongezeka na akaamua kutoa sehemu ya ardhi yake kujenga kanisa la kudumu bila kuandaa mchango wowote.
Waumini wangu hawana uwezo wa kuchangia. Nimewahi kujenga nyumba nzuri bila kusaidiwa, basi kwa nini nisijenge kanisa pia? Karibu tumemaliza, na Jumapili ijayo tutaanza kuabudu huko,” aeleza kwa furaha.
Falsafa yake ni rahisi lakini yenye nguvu: “Njoo jinsi ulivyo.”
Ikiwa mtu atakuja akiwa amelewa, bado anakaribishwa. Akiwa na pombe au sigara, hahukumiwi. Anaweza kutoka nje kuvuta sigara na kisha arudi kuabudu.
“Niliwaambia, hata ukiwa mlevi, njoo tu. Ukiwa umebeba pombe na ukaiacha langoni, sawa. Ukihitaji kuvuta sigara wakati wa ibada, enda chooni uvute kisha rudi. Mungu hamhukumu yeyote. Huponya kwa wakati wake mwenyewe,” alisema katika mahojiano ya kipekee na Taifa Leo.
“Kanisa hili linahusu mazungumzo. Wao huzungumza kwa uwazi kuhusu yanayowasumbua hiyo ni sehemu ya uponyaji,” asema Mchungaji.
“Baadhi yao hufika kanisani wakiwa na njaa na wakiwa wanatetemeka. Kila Jumapili hununua kichwa cha ng’ombe, huchoma supu, huandaa ugali na hula pamoja. Kushiriki chakula ni jambo la Kibiblia,” asema.
Kuanzia Jumatatu hadi Jumamosi, hutoa kazi za mashambani kwa walio katika hatua ya kupona uraibu, akiwalipa Sh300 kwa siku ili kuwazuia kurudi vichochoroni kulewa.
Hata hivyo, huduma yake haijakosa pingamizi.
“Niko mstari wa mbele kusaidia waliopotea na shetani hapendi hilo. Hata makanisa mengine hunikejeli. ‘Lawrence na walevi wake,’ na kuhoji kwa nini nawapa chakula,” alilalamika.