Makala

Karani ambaye ujauzito akiwa angali shuleni hakuzima ari yake ya kuelimika

December 2nd, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na SAMMY WAWERU

TRIZAH Musyoki alijikakamua katika masomo ya msingi ili awahi shule bora ya upili, bidii ambazo alikuwa na matumaini zingemsaidia kuafikia ndoto zake maishani.

Matamanio yake yalikuwa awe daktari, baada ya kufuzu kila ngazi ya masomo iliyohitajika ama inayohitajika.

Mwaka wa 2000, alifanya mtihani wa kitaifa wa darasa la nane, KCPE na akapita vyema, akapata nafasi katika kidato cha kwanza shule moja ya upili nchini.

Licha ya kuwa wavyele wake, yaani wazazi hawakuwa na uwezo vile kifedha, Trizah anasema mwaka wa kwanza na wa pili, kidato cha kwanza na cha pili, aliendeleza azma yake kukata kiu cha masomo bila matatizo.

Katika mojawapo ya likizo, wakati akiwa kidato cha pili, alitembelea mmoja wa wanafamilia kiungani mwa jiji la Nairobi.

Akiwa mzaliwa wa mashambani, alifurahishwa na ziara ya Nairobi. Ni ziara ambayo licha ya kuiridhia, ilichangia maisha yake kuchukua mkondo tofauti.

Ni mwanadada mcheshi na anasimulia kwamba alikutana na kujuana na mwanamume ambaye usahibu wao uliishia kuwa wawili wapendanao.

Anaendelea kueleza kwamba kilichoanza kama mzaha kilitunga usaha, akapata ujauzito.

“Kwa hakika lilikuwa pigo kubwa. Sikujua nianzie wapi kuarifu aliyenikaribisha Nairobi na jinsi ambavyo ningeeleza wazazi wangu waliojikakamua kuona nimeafikia ndoto zangu kwa kujinyima mengi nisome,” Trizah anakumbuka.

Aliamua liwalo na liwe, akapasua mbarika, habari ambazo zilifikia wazazi wake kwa kishindo. Wasiwasi wake ulikuwa maisha yangekuwa vipi baada ya kuteleza.

Trizah Musyoki ni karani jijini Nairobi. Picha/ Sammy Waweru

Kulingana na simulizi yake, wazazi wake hata hivyo walimuitikia alivyo na bada ya kujifungua akaendelea na masomo.

Kufikia mwaka wa 2005, Trizah akawa amekamilisha masomo ya shule ya upili, kwa kufanya mtihani wa mwisho na wa kitaifa kidato channe, KCSE.

Kwa sababu alikuwa na majukumu, majukumu ya ulezi wa malaika wake, alikita kambi jijini Nairobi kuzimbua riziki.

Anaeleza kwamba alifanya vibarua vya hapa na pale, ikiwemo kazi ya uyaya.

Ndoto zake kuwa daktari kwa kiasi fulani zilionekana kufifia kwani fedha alizopata alizielekeza kukithi mwanawe riziki, ikiwa ni pamoja na mahitaji mengine muhimu ya kimsingi.

Licha ya kibarua kigumu cha majukumu kilichomkodolea macho, Trizah anasema alikuwa na nidhamu ya kuweka akiba.

“Baadaye, kupitia akiba niliyoweka kwa muda, nilisomea kozi inayohusiana na masuala ya ukarani,” anadokeza.

Aidha, alipofuzu kwa cheti, alisaka ajira na kwa neema za Mwenyezi Mungu akapata nafasi ya ukarani katika kampuni moja jijini Nairobi. “Maisha yalianza kuimarika, angalau ikawa rahisi kulea mwanangu ambaye tayari alikuwa shuleni,” anaelezea mama huyo.

Hatua ya kutokata tamaa shuleni na pia kujiendeleza kimasomo katika taasisi ya elimu ya juu ni ya kupigiwa upatu, ikizingatiwa kuwa wengi wa watoto wa kike wanaotungwa mimba huishia kuacha shule.

Ni hatia kisheria mwanamume kuwa katika uhusiano wa kimapenzi na mtoto ambaye hajafikisha umri wa miaka 18, umri ambao kuenda chini wengi huwa wangali shuleni.

“Ni muhimu wazazi kufungua nyoyo zao, waeleze wanao mambo waziwazi hatari ya kuwa katika uhusiano wa kimapenzi mapema, hasa wakiwa wangali shuleni,” anahimiza Daisy Kinyua, mzazi wa msichana mwenye umri wa miaka 9.

Daisy anasema alipata mwanawe akiwa katika kidato cha tatu.

“Mtoto hususan wa kike akiwa katika kiwango cha kubaleghe anahitaji maelekezo na ushauri wa kina kumtahadharisha hatari zinazomkodolea macho.

“Binti yangu niko huru naye, ili asifuate nyayo nilizokanyaga,” anaelezea, akifichua kwamba licha ya kuteleza alikamilisha masomo ya shule ya upili na akafanikiwa kusomea kozi ya kiufundi, kushona.

Kwa upande wake Trizah Musyoki, anasema baadaye alikutana na mwanamume ambaye waliishia kuoana, ila ndoa yao haikufanikiwa.

“Tulijaaliwa kupata mtoto pamoja, na licha ya kuwa tulitengana anatekeleza majukumu yake kama mzazi,” anadokeza.

Anafichua kwamba mwanambee wake, yaani kifungua mimba licha ya kumpata akiwa angali shuleni, amegeuka kuwa baraka chungu nzima katika familia yake.

Ni msanii mwimbaji wa nyimbo za injili, na ambaye anapanga baada ya kufanya mtihani wa kitaifa kidato cha nne, KCSE, mwaka huu, japo kalenda ya 2020 imesongeshwa hadi 2021 kufuatia athari za janga la virusi vya corona nchini (Covid-19), ataingia studioni kurekodi vibao vyake.