Kashmir Lamu: Makao makuu ya kuharibu mihadarati
NA KALUME KAZUNGU
DAMPO la utupaji taka eneo la Kashmir kisiwani Lamu ndilo kongwe zaidi kuwahi kubuniwa mbali na lile kuu la Wiyoni.
Kwa muda mrefu, dampo hilo ndilo ambalo limekuwa likitumika kwa utupaji wa maelfu na maelfu ya tani za taka zote zinazokusanywa kwenye mitaa iliyoko ndani ya kisiwa cha Lamu na viunga vyake.
Dampo la Kashmir lilipasishwa na maafisa wa Wizara ya Afya ya Umma kuwa eneo mwafaka la kutupa taka, hasa zile za kiwango kikubwa kama cha kisiwa cha Lamu kutokana na kwamba liko mbali au nje kabisa ya Mji wa Kale wa Lamu na sehemu zingine ambazo ni makazi ya binadamu.
Miaka ya hivi karibuni aidha, dampo la Kashmir limegeuzwa kuwa makao makuu au ngome ya kuharibu mihadarati, hasa ile ambayo washukiwa wamekamatwa, kuitikia kesi zao mahakamani hadi hukumu kutolewa, hivyo kesi zao kufungwa.
Ni jalala hilo la Kashmir ambalo limeshuhudia shehena za thamani ya mamilioni ya dawa za kulevya, ikiwemo bangi, kokeni, heroni na malevya mengine vikiteketezwa kwa ndimi kali za moto.
Kwa mfano, mnamo Agosti 23, 2023, Mahakama ya Lamu, ikiongozwa na aliyekuwa Hakimu Mkuu kwa wakati huo, Allan Temba Sitati, iliongoza shughuli ya kuharibu shehena ya bangi, sacheti za heroni na kokeni za dhamani ya Sh2.6 milioni kwenye jaa hilo la Kashmir.
Juni 2022, Mahakama ya Lamu pia iliongoza zoezi lingine la kuchoma bangi ya zaidi ya Sh1 milioni kwenye jaa hilo la Kashmir.
Mwaka huu, jaa hilo pia limeshuhudia msururu wa mihadarati kuunguzwa moto.
Taifa Leo ilizama ndani, kuchimba chini kutaka kujua bayana ni nini hasa sababu za jaa kongwe la Kashmir kutumika sana katika kuziharibu dawa za kulevya kisiwani Lamu mbali na majaa mengine yapatikanayo eneo hilo.
Mohamed Abdulkadir, ambaye ni kiongozi wa dini na mmoja wa maafisa wa Kamati ya Watumiaji wa Korti kisiwani Lamu, anasema sababu kuu inayofanya wao kuongoza shughuli za kuharibu mihadarati kwenye jaa la Kashmir ni mazingira mazuri kwa shughuli ya aina hiyo hapo.
Bw Abdulkadir, ambaye pia anatambulika kwa kipaumbele chake katika kampeni ya kupigana na mihadarati kote Lamu, anasema kutokana na kwamba jaa hilo liko nje ya mji, kabla dawa za kulevya hazijafikishwa eneo hilo kuharibiwa, huwa zimeanikwa hadharani barabara nzima wakati zikisafirishwa, hivyo kutoa tahadhari au onyo kwa wahusika kusitisha biashara hiyo haramu.
Alihoji kuwa dawa za kulevya kama bangi zinapoteketezwa hutoa moshi mwingi ambao ni hatari kwa wanaoishi karibu.
“Tulichagua jaa la Kashmiri ambalo liko mbali na makazi ya binadamu. Hatutaki watu wavute bangi bila kufahamu wakati tukiichoma. Isitoshe, tunaposafirisha dawa za kulevya hadi Kashmiri kwa lori au trekta, huwa tunazitandaza, hivyo walioko mitaani huona kabisa kwamba ile ni shehena ya bangi inaenda kuharibiwa. Hili huwa ni onyo tosha kwa wahusika kwamba biashara hiyo ni mbaya,” akasema Bw Abdulkadir.
Ali Athman, mkazi wa Kashmir, anautaja mtaa wake kuwa miongoni mwa sehemu za Lamu zinazovuma kutokana na vijana wengi kuathirika pakubwa na janga la mihadarati.
Kulingana na Bw Athman, vijana wengi wamegeuzwa goigoi kutokana na uraibu wao wa kuramba au kubugia mihadatati kila kukicha.
Anapongeza hatua ya jaa la Kashmir kuteuliwa kama makao makuu ya kuharibia mihadarati Lamu, akisema hatua hiyo ni mbinu mbadala na ngangari ya kukemea uovu huo mtaani kwao na katika jamii ya Lamu kwa jumla.
“Twafurahia sana hatua ya jaa letu kutumika kuharibia mihadarati. Tangu shughuli za kuchoma dawa za kulevya jaani hapa ianzishwe miaka kadhaa iliyopita, wauzaji wa mihadarati wameogopa. Hata wengine tunaowajua wameacha kabisa kujishughulisha na biashara hiyo,” akasema Bw Athman.
Sababu nyingine inayosukuma wana kampeni ya vita dhidi ya mihadarati kuteua jaa la Kashmir katika kuharibu dawa za kulevya ni kwamba jaa lenyewe liko na nafasi kubwa iliyozingirwa seng’enge, hivyo kuwa salama zaidi kwa timu inayoharibu shehena hizo.
Licha ya kuwa mbali au nje ya kisiwa cha Lamu, jaa hilo pia liko kwenye eneo fiche, hivyo kuwapa imani zaidi na nguvu wenye kutekeleza shughuli hiyo kuiendeleza kwa umakinifu mwingi bila kutapatapa au kuogopa kwamba watavamiwa na makundi ya vijana waathirika wanapoona dawa zao zikiharibiwa.
Kwa miaka mingi sasa, dawa za kulevya zimesalia kuwa donda sugu miongoni mwa vijana wa Lamu.
Ni kutokana na hilo ambapo utawala wa kaunti ya Lamu na wadau mbalimbali wamekuwa wakiibuka na mifumo mbalimbali ya kupiga vita na kumaliza mihadarati Lamu.
Gavana wa Lamu, Issa Timamy, tayari ameweka ahadi ya kumtunuku afisa yeyote wa polisi kitita cha Sh50,000 endapo watafaulu kumnasa na kumshtaki mmojawapo wa wasambazaji wakuu wa dawa za kulevya Lamu.
Kadhalika, serikali ya kaunti imejenga vituo vya matibabu ya methadone ili kuwasaidia waraibu wa dawa za kulevya, hasa heroni kupunguza hamu na makali ya kuendelea kutumia dawa hizo.
Kwa sasa tayari vituo viwili vya methadone vimejengwa na vinaendelea kuwahudumia waraibu wa mihadarati bure bilashi Lamu.
Vituo hivyo vinapatikana kwenye hospitali kuu ya King Fahd mjini Lamu na ile ndogo ya Faza, iliyoko Lamu Mashariki.