Makala

Kauli ya mwimbaji Mary Lincoln kuhusu utamu wa maisha

May 14th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MWANGI MUIRURI

UNAJIHISI kuwa umefika mwisho wa maisha yako, kuwa hakuna lolote la kukupa tabasamu limebakia na unaona afueni ni bora tu uhai wako ungekuondokea?

Au, unamjua yeyote ambaye amefika katika njia panda hiyo na anaonelea tu mauti ndiyo tu afueni?

Mwimbaji Mary Lincoln anakuambia tuliza roho au umwambie mtu anayehisi hivyo aache kubabaika.

“Kwa kuwa hii dunia uionavyo iko na nafasi ya kila mmoja wetu na aliye juu katika Kiti cha Enzi akiwa ndiye Mola hajatufungia jicho lake la neema,” anasema Mary Lincoln.

Anasema kuwa wengi huwa na wasiwasi wa maisha, ilhali Mungu katika uwazi wake wa kuwa Baba wetu halisi ametuahidi kuwa hatawahi kukubali tuteseke zaidi ya uwezo wetu wa kustahimili.

Mwimbaji Mary Lincoln. Picha/ Mwangi Muiruri

Anasema kuwa wengi hufika katika uamuzi wa kujidhuru kutokana na uzembe wa kungoja tu neema ya Mungu katika maisha yao.

“Mungu ametuagiza kuwa tuweke macho yetu katika mbingu wakati wa usiku na tujitazamie idadi ya nyota alizoziumba. Ukiambiwa wewe uumbe nyota utaanza kutafuta nyaya za stima, viini vyote ujuavyo vya umeme ili ukaunganishe na vifaa vingine katika Sayansi yako utupe nyota bandia! Lakini Mungu anakuambia uangalie nyota zake alizoziumba kimiujiza. Anakuambia kuwa baraka zako zitakuwa sawa na hiyo idadi hiyo ya nyota,” anasema.

Katika hali hiyo anakuuliza: “Utajiua namna gani eti hupati baraka zako na unasononeka kimaisha?”

Bi Lincoln anasema badala ya mja kujiangazia kama aliye katika maisha ya uchochole, anafaa kujiangazia kama aliyebarikiwa na uhai.

“Baraka ya uhai ni moja ambayo wengi hawaitambui. Hawajui kuwa wengi wa rika lao waliaga dunia kitambo, wengine jana na hata wengine asubuhi hii. Lakini wewe uko katika uhai na huoni kama hiyo ni Baraka,” anahoji.

Anasema Baraka nyingine wengi hawatambui ni ile ya kuwa na afya njema.

“Unaenda kwa duka kununua sumu au kamba ya kujitoa uhai… Unajipeleka kwa miguu yako na unaagiza kwa sauti yako na pia kwa pesa zako. Huoni kama hiyo ni baraka ya kuwa na uzima wa mwili wa kujitembeza, kuwa na sauti na pia kuwa na hizo pesa kidogo za matumizi?” anahoji.

Maisha matamu

Anasema kuwa maisha huwa ni matamu sana, kuwa kila mmoja wetu amebarikiwa na yake ni vile tu wengine hulalia bahati za wenzao milango wazi na hivyo basi kupoteza matumaini haraka wakijilinganisha na wengine.

“Wengine wamebarikiwa na pesa nyingi, lakini wako na maradhi zaidi ya 50 ndani ya miili. Wewe huna hizo pesa nyingi lakini huna ugonjwa unaokutatiza… Hizo ndizo neema ambazo hutenganisa sisi na pia kutuweka sambamba katika mapenzi ya Mungu,” anasema.

Anaeleza kuwa Mungu aliyekuumba hujua sababu ya kila safu ya maisha yako, anajua mbona kwa sasa unasononeka katika majaribu na anajua tu hutaangamia katika mahangaiko hayo kuwa atakuneemsehea maisha yako…. Hata hivyo, wengi hawana imani; baadhi wako nayo ila finyu huku wengine wakiwa tu ni kujiangamiza kimakusudi kwa ubutu wao wa kuelewa maisha na mchango wa Mungu ndani yao.

Huku sheria za Kenya za kudhibiti hatia za jinai katika kipengele cha 226 zikiwa huweka adhabu ya kifungo cha miaka miwili gerezani, faini isiyoelezewa au zote mbili katika ibara ya 36 ya sheria hiyo kwa yeyote ambaye atajaribu kujiua lakini anusurike, Lincoln anasema kuwa sheria si kitu, kuelewa umuhimu wa Mungu ndiyo ‘mambo yote’.

Anasema kuwa dawa ya maisha, siri ya maisha, na uwazi wa maisha kwa mpigo ni kutumainia Mungu, ufanye yale yote unawajibishwa na maisha na kasha uyakabidhi kwa muumba wa yote na vyote, akuneemeshee.

“Nisisikie tena ukisema utajiua. Ngoja Mungu aliyekupa uhai akudai huo uhai wako. Ikiwa huna yale unayoorosdhesha kuwa Baraka, omba na umwelezee unayoyahitaji. Kisha ungoje ukitenda mema katika msingi wa maelekezo ya Mungu…Utajiua leo na kumbe Baraka zako zilikuwa ziingie kesho…” anasema.