Lugha, Fasihi na ElimuMakala

KAULI YA WALIBORA: Kanuni ya msingi ya utamkaji izingatiwe katika utohozi

January 23rd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA PROF KEN WALIBORA

Je, ni sawa kutafsiri “Central Police Station” kama “Kituo cha Kati cha Polisi”? Ikiwa ni sawa basi “Central Bank of Kenya” itatafsiriwa “Benki ya Kati ya Kenya.”

Neno “Central” ni kivumishi kinachotokana na nomino “Centre” kwa tahajia za Kiingereza cha Uingereza au “Center” kwa Kiingereza za tahajia za Marekani. ‘Ukatikati’ unaoashiriwa umo katika maana ya kitamathali tu sio kihalisi.

Kati kwa sababu ya umuhimu, kati inayokubalika katika Kiingereza, lakini maana hiyo haiwezi kupatikana kwa kulitumia neno lililo kisawe chake halisi katika Kiswahili. Ndiposa siku zote tunahimiza tafsiri ya dhana zaidi kuliko kukimbilia kutafsiri maneno.

Mantiki ya kutafsiri ya maana ndiyo msingi wa kutafsiri Central Bank of Kenya kuwa “Benki Kuu ya Kenya?” Ukilitazama jengo la Benki Kuu ya Kenya, utaona limeandikwa Banki Kuu ya Kenya.

Je, hilo ni kosa? Mbona waliotafsiri hawakuandika Benki badala ya Banki? Hapana shaka maneno yote mawili hayana asili ya Kiswahili, bali yametoholewa kutoka kwa nomino ya Kiingereza, ‘bank’.

Katika utohozi wengine huzingatia tahajia ya maneno katika lugha chanzi au utamkaji wa maneno katika lugha chanzi. Yamkini walioamua kutumia “banki” kwanza walizingatia tahajia ya Kiingereza na kuswahilisha neno hilo kwa kuliongezea irabu “i” mwisho.

Pili yamkini kwao utamkaji wa neno ‘bank’ unakaribiana na kisawe cha Kiswahili walichokiteua ili kutajirisha lugha hii ya mawasiliano mapana Afrika Mashariki. Tatu, hawakuelekezwa wala kukwazwa na hofu kwamba neno hilo, yaani ‘banki’ linakaribiana na kasumba iitwayo bangi.

Bangi ni aina ya dawa za kulevya ambazo baadhi ya watu wanaozuiliwa katika kituo cha Polisi cha Central au wameshikwa nayo ama wamesingiziwa kuwa wameshikwa nayo.

Tukiamua kutafsiri kituo hicho tutasema “Kituo Kikuu cha Polisi” sio “Kituo cha Kati cha Polisi.” Ila mjadala wa matumizi ya ‘banki’ na ‘benki’ unaweza kuhusianishwa na matumizi ya Disemba na Desemba au Bayolojia na Biolojia.

Watunzi wa kamusi ya Biolojia, Fizikia na Kemia, kupitia kwa ile ikiitwa Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili, (TUKI) Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, waliamua kupuuza msingi madhubuti wa utohozi ambao huzingatia utamkaji.

Kosa la kubwa hasa lipo katika tafsiri yao ya neno la Kiingereza “Biology.” Ingawa tahajia za Kiingereza zina herufi “bio,” herufi hizo zinatamkika “bayo” katika Kiingereza kilichokipa Kiswahili neno hilo geni na Kigiriki au Kiyuyani kilichokipa Kiingereza neno hilo jipya.

Tafsiri sahihi ilijuzu iwe Bayolojia ili kuelezea dhana kusudiwa. Tunashukuru wataalamu hao kwa kazi nzuri. Mgalla muue na haki yake umpe. Ila tungekuwa na uwezo tungewafunga katika Kituo Kikuu cha Polisi cha kukiuka kwao kwa kanuni ya msingi ya utohozi.

Kanuni hiyo hiyo inakiukwa na wale wanaong’ang’ania kusema Desemba badala ya Disemba. Desemba inazingatia mno tahajia ya Kiingereza badala ya kuzingatia utamkaji wa neno katika lugha hiyo.