Lugha, Fasihi na ElimuMakala

KAULI YA WALIBORA: Kiswahili hakitapiga hatua bila mikakati, amri na mapinduzi

March 6th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na KEN WALIBORA

KINA CHA FIKIRA

CHUO Kikuu cha Riara kilichoko katika barabara ya Mbagathi, Nairobi, kilipokea nakala zake za kwanza za Taifa Leo wiki iliyopita.

Nilibaini kwamba hakuna nakala ya gazeti hili la pekee la Kiswahili nchini Kenya iliyokuwa inaletwa katika maktaba ya chuo. Maktaba ikichukua magazeti ya Kiingereza tu, si Daily Nation, si Sunday Nation, si The Standard, si The Star.

Nilikuwa najiuliza kwa nini chuo hiki kinakosa kabisa matoleo ya gazeti la pekee la Kiswahili nchini? Isitoshe, katika mauzo–kama sikosei—Taifa Leo ndilo gazeti la tatu katika wingi kwa nakala zinazouzwa kila siku.

Yale magazeti ya Kiingereza ya kampuni ya usambazaji habari ya NMG niliyokwishayataja yapo mbele, yakifuatwa na The Standard na kisha Taifa Leo.

Kwa kweli labda hizo hesabu huenda zimebadilika tangu nilipokuwa katika tasnia ya vyombo vya habari, ingawa sidhani kwa kiwango kikubwa.

Vyovyote viwavyo, gazeti la Taifa Leo linaandikwa na kuchapishwa katika Kiswahili—na wala usilione dogo hili.

Kiswahili ndiyo lugha ya taifa ya Kenya, lugha rasmi, (sambamba na Kiingereza) na lugha ya mawasiliano mapana au lingua franca kama wasemavyo wataalamu. Unaweza kuongeza kwamba Kiswahili ndiyo lugha ya mawasiliano mapana katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (JAM) lugha rasmi tarajiwa (baada ya kupasishwa na bunge la Afrika Mashariki) na lugha ya utambulisho.

Ukweli ni kwamba hakuna lugha nyingine inayozungumzwa na wakazi wa Afrika Mashariki kama Kiswahili hata kama wapo wanaoiita ‘Chiswahili’ kama baadhi ya Wanauganda na Wanyarwanda. Lakini mgogoro nilio nao unahusu nchi ya Kenya.

Je, haya madai makubwa makubwa ya kusema katika katiba kwamba Kiswahili ni lugha ya taifa na lugha rasmi yana tija gani? Zamani zile za gazeti la serikali Kenya Times na Kenya Leo, maofisi yote ya umma yalilazimika kununua nakala za magazeti hayo.

Kizazi cha sasa cha vijana huenda hakina habari kuhusu kuwepo kwa magazeti hayo mawili ya serikali ya KANU na ambayo sasa yamekufa na kuzikwa katika kaburi la sahau.

Ila ninapokumbuka amri ya kununuliwa kwa magazeti hayo kwa maofisi ya umma, nakosa kujiuliza kwa nini isiwe sheria kwamba gazeti la pekee la Kiswahili—lugha ya taifa, lugha rasmi, na lugha ya mawasiliano mapana-linanunuliwa na kila asasi.

Amri

Naam, wapo watakaosema huo ni udikteta tena mbaya sana. Ila ukweli ni kwamba Kiswahili hakitaendelea bila amri na mikakati ya mapambano na mapinduzi.

Mbona ni amri ya kukifanya Kiswahili somo la lazima katika shule za msingi na sekondari ndiyo imechangia maenezi mapana zaidi ya Kiswahili tangu enzi ya Rais Moi.

Kwa sasa vipo vizazi vya Wakenya waliolazimishwa kusoma Kiswahili kwa takriban miaka 14.

Ni amri, ni udikteta na tazama tija ya kuwa na taifa la wasemaji Kiswahili.

Shukran muktubi wa Chuo Kikuu cha kuitika wito wa mnyonge kama mimi.