KAULI YA WALIBORA: Korona ni baniani akuzaye msamiati wa Kiswahili
NA PROF KEN WALIBORA
KWEMA msomaji wangu mpendwa? Nashukuru sana kwa shauku yako ya kusoma safu hii kila wiki tangu 2016. Kariha yangu ya kuandika inatoka kwako.
Miye si bingwa wa masuala ya afya ila nashauri kwa unyenyekevu uendelee kujilinda dhidi ya janga lililotufikia kwa kunawa mikono, kuvaa barakoa, kutowasalimia watu mikononi, kuepuka vikundi vya watu. Ilmuradi fuata amri ya serikali ujilinde wewe na uwapendao.
Nilikuwa na atiati kuhusu hatima ya safu hii. Sikuwa na hakika nayo kwa sababu virusi vya korona vimeondoa hakika ya chochote duniani.
Rafiki yangu anayefanya kazi kwenye shirika moja maarufu la habari kaniambia kwamba maripota wao wamepunguziwa siku za kufanya kazi na kupunguziwa mshahara sawia.
Msingaji mmoja kaniambia alipewa mshahara wa miezi mitatu na barua ya kumwambia watamwita tena ila akipata ajira kwengineko asiiache.
Mpwa wangu anayefanya kazi na shirika la ndege nchini, kapewa likizo ya miezi mitatu, tena bila mshahara. Sasa anahesabu mende na mbu nyumbani, hatima yake haijulikani.
Kusema la haki hata mimi nilikuwa nimekata tamaa hasa baada ya kupokea baruapepe yenye salamu kwamba safu hii imekomeshwa na wimbi la korona.
Nimeona ukweli wa methali ya Kiswahili isemayo, “Ukiona mwenzako ananyolewa chako kitie maji.” Yaani tulipowaona Wachina wanatetereka kwa janga hili, tulifikiria ni janga lao wao tu. Kumbe hata nasi linatufikia. Sasa limetufikia na kufikia wakati naandika makala haya, zaidi ya nchi 190 zimeathiriwa.
Katika mchafukoge wa janga hili la korona nimebaini mambo machache. Mwanzo, wanadamu wote ni sawa. Korona imetusawazisha.
Pili, hakuna binadamu mwerevu na mwenye nguvu; sote mahambe na dhaifu. Tatu, wanaopona ni wengi zaidi kuliko wafao kutokana na ugonjwa wa korona. Mahitimisho haya yote ukiyachunguza kwa makini yanasheheni chembechembe za faraja.
Ila mimi faraja yangu kubwa ni kuona jinsi Kiswahili kinavyopambana na kadhia mpya. Sijaona lugha nyingine duniani yenye bidii ya kutaka kujua hiki kitu kipya nitakiitaje kama Kiswahili.
Utashi wa kujaribu na mara nyingine kutapatapa kuyatafutia msamiati mambo mapya ni sifa bainifu ya lugha ya Kiswahili, sifa inayofariji si haba, hata nyakati za nakama kama hizi.
Juzi kwenye darasa langu la mtandaoni, (maana siwezi tena kuonana ana kwa ana na wanafunzi wangu), nimeulizwa “Sanitizer ni nini kwa Kiswahili?” Nilifurahi sana. Na kabla sijajibu, mwanafunzi mmoja akadakia na kujibu; “kiyeyushi.”
Nikafurahi zaidi. Furaha yangu haitokani na usahihi wala utosahihi, bali utashi uliopo kuzipatia dhana mpya zinazozuka maneno ya Kiswahili.
Midahalo mipana na mipevu inaibuka kote kuhusiana na jinsi ya kuyaita maradhi haya; je ni corona au korona, karantini au umwali (quarantine), tandavu au mtandavu (pandemic), kumbakumba au ambo mlipuko (epidemic)?