KAULI YA WALIBORA: Shime kumuenzi nguli wa fasihi Prof Bukenya angali hai
NA PROF KEN WALIBORA
MNAMO tarehe 30 Agosti kulikuwa na sherehe ndogo ya kumuenzi msomi na mtunzi anayejitambulisha kwa maneno na vitendo kuwa Mwana Afrika Mashariki kamili. Huyu si mwingine ila Prof Austin Lwanga Bukenya (pichani).
Mimi nilikuwa miongoni mwa waalikwa katika hafla hiyo, ijapokuwa mpaka sasa sijui kwa nini niliakwa, mtu mdogo hapa nilipo. Hata hivyo, sina budi kusema nilifurahi si haba kwa heshima na taadhima ya kujumuishwa katika hafla hiyo.
Nilikumbana na mkururo wa kumbukizi za ukuzi wa fasihi Afrika Mashariki tangu miaka ya mwishomwisho wa sitini. Nitakueleza machache kuhusu historia hiyo.
Nilikutana na Prof Bukenya mwanzoni nilipokuwa mwanafunzi katika shule ya sekondari. Nilikutana naye kimaandishi katika shairi lake la Kiingereza, “I met a thief” katika diwani ya Poems from East Africa iliyohaririwa na babu yake mwanahabari Victoria Rubadiri; David Rubadiri na David Cook. Kisha nikakutana naye Prof Bukenya ana kwa ana mara ya kwanza katika kongamano la fasihi katika Chuo Kikuu cha North Illinois, Marekani, mnamo 2008.
Kilichonivutia kwake zaidi ni unyenyekevu wake na ustaarabu wa kupindukia. Alifanya kunichunuku tu kama walivyonichunuku baadhi ya magwiji wa fasihi kama vile Said Mohamed, Chris Wanjala, Kimani Njogu, Henry Indangasi, Evan Mwangi, K.W. Wamitila, Simon Gikandi na Alamin Mazrui, pindi nilipodiriki kukutana nao.
Alinitambulisha kwa msomi na mhariri Helen Nabasuta ambaye baadaye alikubali makala yangu kuchapishwa katika kitabu cha Masculinities in East African Literary and Cultural Texts.
Makala yangu kuhusu Fumo Liyongo ndiyo ya kwanza kwenye kitabu hicho. Prof Bukenya, alichangia makala pia, ndiyo sababu ya makala yangu kuwamo. Namshukuru sana kwa hilo.
Wahudhuriaji katika sherehe ya kumuenzi walikuwa wamejaa maneno ya shukrani kwa msomi huyu mpole na muungwana. Dkt Joyce Nyairo na Mushai Mwangola walisifia msimamo wa Bukenya wa kujitenga na ukware wa wahadhiri wa vyuoni wenye tabia za kuwageukia wanafunzi wao kama simba kula wanawe.
Isitoshe, Alisifiwa kwa kuogelea sawia katika bahari ya lugha na fasihi ya Kiswahili na Kiingereza. Kwa kweli hata Kifaransa na Kiganda amekipigia mbizi vilivyo. Aidha, ameandika makala na vitabu mbalimbali vya Kiingereza kama vile The Bride na A Hole in the Sky.
Isitoshe, akishirikiana na mwalimu wake Pio Zirimu, waliunda neno orature lenye kumaanisha fasihi simulizi, neno linalotumika kote duniani kunakotumika Kiingereza katika mawanda ya fasihi.
Bukenya na Zirimu walidai kwamba kauli ya Kiingereza oral literature haikidhi maana ya fasihi simulizi maana literature siku zote huwa imeandikwa ilhali fasihi simulizi ni ya kusimuliwa.
Kwa hiyo, huyu ni msomi ambaye ameacha nyayo zake katika safu ya magwiji wa fasihi duniani na mchango wake utadumu daima.
Zuri zaidi kaenziwa akiwa hai. Kwa Prof Kimani Njogu aliyeandaa hafla hiyo namwambia Webale nyoo!