Lugha, Fasihi na ElimuMakala

KAULI YA WALIBORA: ‘Shosho’ Cecilia ni mfano hai kuwa ujuzi wa mtu hautegemei umilisi wa Kiingereza

August 8th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na PROF KEN WALIBORA

Hivi majuzi mtangazaji mpya wa kipindi cha Trend cha NTV Amina Abdi alijaribu kumhoji Bikizee wa miaka 80 aiitwaye Cecilia. Hakufaulu. Hakufua dafu hata vibayavibaya.

Kama naibu wa rais William Ruto huwa anateka mahojiano anapohojiwa, bikize huyu aliyateka mahojiano maradufu. Alitawala, aliyadhibiti, aliuliza maswali, akajijibu mwenyewe. Ilmuradi alijitawanya alivyotaka.

Nilimwonea huruma mtangazaji; alikuwa kama samaki katika nchi kavu, hajui afanyaje au asemeje? Je afurahi au akasirike, aulize swali au ajibu? Asimamishe mahojiano au aendelee? Pagumu hapo.

Bibi Cecilia ni fundi wa kutengeneza vyombo vya muziki katika magari. Hilo ndilo liliwafanya NTV kumtafuta wamhoji kwa kipindi chao. Hana kitembo kikubwa cha elimu.

Ni ajuza wa umri wa miaka 80. Ni mwanamke. Haya yote yanaelekea kwenda kinyume na uhalisi wa mambo kwamba bibi huyu ni tegemeo katika kuunda redio na ala nyingine magarini, hasa matatu za Kariobangi zenye muziki wa kuweza kupasua viwambo vya masikio.

Kwa kweli alinikumbusha Mzee Nyandika Maiyoro aliyewakilishi Kenya kwa riadha katika mashindano ya michezo ya Jumuiya ya Madola nchini Kanada 1954.

Nilipomhoji katika QTV alikataa katakata kufuata mkondo wa maswali yangu. Alisema aliyoyataka na mimi, kama Amina Abdi, lilikuwa langu jicho. Ila uzuri wa kuwaleta wazee kama hao kwenye runinga ni kukipa kizazi cha sasa fursa ya kuvuviwa hekima na busara.

Mathalan, kauli moja aliyoisema Shosho Cecilia, kama wanavyomwita watu wengi, ni kwamba kujua kuzungumza Kiingereza hakumaanishi ujuzi wa fani mbalimbali. Alieleza kwamba wahitimu hutoka vyuo vikuu wakiwa na Kiingereza chao lakini hawajui lolote?

Je, huyu bibi kadanganya kwa kusema hivyo? Je, alionyesha dharau kwa wahitimu wa vyuo vikuu?

Kuna tatizo hapa Kenya kwamba ujuzi wa mtu katika fani yoyote unategemea jinsi anavyokijua Kiingereza. Hilo ndilo nililowahi kubishana na Ezekiel Mutua kulihusu mwaka saba hivi iliyopita katika kipindi cha mjadala cha idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Ujerumani, DW.

Mutua alikuwa ameishutumu serikali kwa kumteua Katua Kalembe Ndile kuwa naibu wa waziri ilhali Ndile hakijui Kiingereza. Shosho Cecilia alisema wazi wazi kwamba hatuwezi kupima uwezo wa mtu wa kujua mambo kwa Kiingereza alichonacho.

Haya ndiyo sikuzote wakereketwa wa Kiswahili wanawaambia watunga sera wa nchi hii. Nchi zilizositawi katika Mashariki ya Mbali zinatumia lugha zao katika mawasiliano, kufundishia na kuvumbua vitu ambavyo wanavijaza katika soko letu. Sisi hatuvumbui chochote kwa kung’ang’ania Kiingereza cha wengine.

Nyakati fulani katika mahojiano, bikizee alimkemea Amina Abdi kwa kutomsikiliza au kutomsikiliza vizuri. Kama kauli zetu hazisikizwi natumai kwamba kauli ya Shosho Cecilia itasikilizwa.

Baadhi yetu tutakuwa katika kongomano la Kiswahili la CHAKITA katika Chuo Kikuu cha Moi, Eldoret wiki hii tokea Alhamisi hadi Ijumaa. Tutatoa kauli zetu kama sikuzote tufanyapo. Lakini je, watunga sera watasikiliza?

Watatekeleza? Msikilizeni Shosho Cecilia jamani Kiswahili nacho kisonge mbele?