KAULI YA WALIBORA: Tusiogope kuzungumza Kiswahili kwa kuchelea kutoeleweka na wageni
NA PROF KEN WALIBORA
UBALOZI wa Tanzania nchini Ufaransa uliandaa kongomano kukipigia upatu Kiswahili majuzi yale. Hafla hiyo ilihusisha washiriki kutoka shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).
Hafla hiyo iliyoongozwa na balozi wa Tanzania nchini humo, Samwel Shelukindo ilitia fora si haba. Kimsingi shirika la UNESCO lilitambua dhima ya Kiswahili ya kuleta utangamano barani Afrika.
Mimi siku zote hufurahia taarifa za namna hiyo. Lolote linalohusu maendeleo ya Kiswahili hunifariji. Kwenye hafla balozi wa Tanzania alitaja hatua ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika, (SADC) inayoongozwa na mwenyekiti wake Rais John Pombe Magufuli kukifanya Kiswahili kuwa moja ya lugha za matumizi kwenye jumuiya hiyo.
Alitaja pia hatua ya nchi za Afrika Kusini na Namibia kukipatia Kiswahili fursa katika mfumo wa elimu ambapo wanafunzi wa nchi hizo wanaweza kujifunza katika lugha hiyo yenye asili mwambao wa Afrika Mashariki.
Mimi naafikiana na balozi Shelukindo kwa haya yote. Zipo dalili nyingi kwamba mustakabali wa Kiswahili ni mzuri sana.
Nilifarijika sana kutazama runingani mazishi ya rais wa pili wa Kenya, Daniel Toroitich arap, pale viongozi mbalimbali walipozungumza Kiswahili.
Rais wa Kenya aliyeko sasa, Uhuru Kenyatta, alitoa mfano mzuri kwa kukitumia Kiswahili sana katika hotuba yake, licha ya kwamba walikuwapo wageni wasiokijua. Hivyo ndivyo inavyopasa kuwa.
Katika nchi za watu wanaojielewa na kujikubali, hakuna kuhofu kuzungumza lugha yako kwa sababu ya mgeni asiyeielewa.
Kama mgeni haelewi, kosa si lako, ni lake yeye. Kutokuelewa kwake kunaweza kumfanya ama akuchukie au akuheshimu zaidi kwa kuzingatia turathi yako ya kilugha na kitamaduni.
Miaka miwili iliyopita nilikwenda sherehe za posa ya rafiki yangu huko Elburgon, katika Kaunti ya Nakuru. Sherehe zote zilifanywa kwa Kikikuyu ambacho miye sikielewi be wala te yake. Lakini niliona raha ilioje, kuwaona wadau wakisakata lugha yao kwa madaha na fahari!
Haikuwa taabu sana kwamba kukisia mwelekeo na mkondo wa mazungumzo yao na kuburudishwa na lugha nisiyoelewa. Kubwa zaidi niliwaheshimu na kuwahusudu kwa wasemaje hao.
Kwamba sikuelewa lugha yao, halikuwa kosa lao bali langu mimi.
Kwa mantiki hiyo hiyo, tusiogope kusema Kiswahili kwa kuchelewa balozi wa Uingereza au Kanada, au Marekani yupo kwenye hafla na Kiswahili kinamchenga. Kama Kiswahili kinamchenga atulie, akubali kuchengwa, atafute mkalimani au aanze kujifunza mwenyewe.
Na hapo ndipo hutokea mambo ya ajabu wasiyoyaona watu kwetu, wanayafumbia macho. Mabalozi wengi wanaokuja mataifa yetu ya Afrika Mashariki hujifunza Kiswahili ama kabla hawajaja au wakishakuja au yote mawili.
Mimi mwenyewe nimehusika katika kufundisha Kiswahili mabalozi na maafisa wa kibalozi kutoka mataifa mbalimbali. Ndiyo maana, hutokea mwenyewe akakitema tema Kiingereza kwenye hafla ya umma, kisha akiinuka balozi wa nchi za Ulaya, akakimenya Kiswahili.
Ninachosema ni kwamba, tusiogope kusema Kiswahili kwa kuchelea kutoeleweka na wageni.