• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 2:29 PM
KAULI YA WALIBORA: Wanaoenda kufunza wageni Kiswahili wachujwe kuondoa makapi ya wababaishaji

KAULI YA WALIBORA: Wanaoenda kufunza wageni Kiswahili wachujwe kuondoa makapi ya wababaishaji

Na KEN WALIBORA

UMEKUWEPO msisimko mkubwa kuhusu ufundishaji wa Kiswahili Afrika Kusini na kuibuka kwa fursa za ajira kwa wajuzi wa Kiswahili.

Wadau wa Kiswahili wamelisisimkia hilo na baadhi wamelimakinia kwelikweli kama wenzo wa kujikwamua kimaisha.

Kama ilivyo ada Watanzania na Wakenya ndio waliosisimka zaidi kwa ambavyo wanaamini sikuzote kwamba wao ndio mahiri wa Kiswahili. Yaani kwao suala la nani afundishe Kiswahili Afrika Kusini ni rahisi kulijibu, au Watanzania au Wakenya.

Kama wanavyosema watu wa Pemba, hilo halitaki tochi, au kama alivyozoea kusema mwalimu wangu wa shule ya upili Alex Ngure, ujumbe u wazi. (Siku moja nitaandika kuhusu maisha yangu katika shule ya sekondari penye uzima na uhai).

Walimu wa Kiswahili wa Kenya na Tanzania wanaamini wana hatimiliki ya ufundishaji wa lugha hiyo popote duniani .

Je, wanaweza? Walimu wa Kiswahili wengi walioko katika mataifa ya kigeni ni wazawa wa nchi hizi pacha za Kiswahili. Ukienda katika vyuo vikuu vingi Marekani vinavyofundisha Kiswahili utakutana na walimu kutoka Kenya na Tanzania.

Baadhi ya walimu hawa hawajabobea katika Kiswahili.

Mathalan ule mpango wa Fulbright wa kuwaleta walimu kutoka Afrika Mashariki hususan huchukua wale waliosomea Kiingereza.

Wapo walimu wengi waliotolewa Tanzania kwenda kufundisha Kiswahili ingawa shahada zao za kwanza katika vyuo vikuu ni katika taaluma ya Kiingereza.

Baadhi ya walimu hao wamefikia hadi kuandika makala na vitabu vya sarufi ya Kiswahili vinavyolenga hadhira ya wanafunzi wa Marekani ingawa kwa kweli hawakubobea katika Kiswahili.

Nafasi katika safu haitoshi kutaja majina mahususi ya walimu wa Kiswahili Marekani waliobobea katika kilimo, mbinu za ufundishaji, isimu ya Kikerewe, sera ya elimu, sosholojia, kemia, fizikia, na afya ya jamii.

Mfumo uliopo ni wa ufundishaji wageni yake mambo ya msingi kabisa ya lugha—kama vile mama, baba, dada, kaka, habari na mtoto. Haya hayahitaji ubobevu katika Kiswahili.

Yamkini anachohitaji mwalimu ni Kiingereza kidogo cha mwanafunzi wake na Kiswahili cha kuomba maji ya kunywa alichokiokota kwao Afrika Mashariki—sana sana Kenya au Tanzania. Vitabu ya Kiswahili vya chekechea au madarasa ya chini ni vigumu zaidi kwa wageni wanaojifunza Kiswahili.

Afcon

Baadaye mwezi Juni huu mataifa ya Afrika yalifuzu kuingia kinyang’anyiro cha kombe la taifa bingwa Afrika (Afcon) yataenda Misri.

Hebu fikiria itakuwaje kila taifa likipeleka wanariadha wao wa masafa mafupi au marefu au wanaoruka kwa mapana au wanaorusha mikuki au wasanii kucheza kandanda Misri.

Matokeo yatakuwaje? Kocha wa Harambee Star akimchukua David Rudisha kuwa golikipa badala ya Patrick Matasi, Kenya haitageuzwa pilau na wapinzani wake? Nayo Tanzania ikimchukua Diamond Platnumz kuwa mshambuliaji atafunga mabao mangapi?

Je, nani hawa tunawapeleka kufundisha wageni Kiswahili? Je, wana mbinu mwafaka za kuwafundisha wageni au ni wababaishaji tu? Kiswahili wanakijua au hilo si muhimu?

You can share this post!

GWIJI WA WIKI: Deon Musau Muia

Waislamu wa Kaskazini na Pwani wagawanyika kuhusu Idd

adminleo