Makala

Kaunti ya Kiambu yatambulika na Amerika katika uwekezaji

December 3rd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na LAWRENCE ONGARO

AMERIKA itazidi kuwekeza hapa nchini Kenya kutokana na ushirikiano mzuri uliopo baina ya nchi hizi mbili.

Balozi wa Amerika nchini Kyle McCarter amesema Kaunti ya Kiambu, itanufaika pakubwa katika uwekezaji kutokana na eneo kubwa la ardhi mahususi kwa uwekezaji.

Ametaja mji wa Ruiru sehemu ya ukubwa wa ekari 5,000 ambako nchi kama Amerika, New Zealand, Norway na Uingereza zimewekeza biashara zao kubwa huko.

“Uwekezaji huo umeinua uchumi wa Kenya kwa takribani Dola 1.1 bilioni. Hii in njia moja ya kukuhakishia kuwa Amerika ina imani na nchi ya Kenya,” amesema McCarter.

Amesema uwekezaji huo unabuni nafasi za ajira kwa wengi, unapanua nyanja za elimu, na ujenzi wa majumba makubwa.

Katika eneo hilo la uwekezaji la Industrial Park, mjini Ruiru kuna miundomsingi ya barabara ya kilomita 20, umeme, na mazingira ya kufana katika kila sehemu.

Katika eneo hilo, viwanda kadha vimezinduliwa na kubuni ajira kwa watu zaidi ya 2,000 kwa muda wa miaka mitatu ambayo imepita.

Baadhi ya viwanda hivyo ni Cooper K-Brands, Dormans, Africa Logistics Properties, Copia, Nova Pioneer, Crawford International, Hunker Energy, Lifestyle Properties, Unity Homes, na Freight Forwarders Kenya.

Balozi amesema Amerika itafanya juhudi kuona inashirikiana bega kwa bega na Kenya ili kuona ya kwamba ajenda nne muhimu za serikali zinafanikiwa.

Amesema nchi yake inataka kuona serikali ikipambana na ufisadi ili kuifanya Kenya ya kutegemewa na wengi. Aidha amesema Kenya ni mojawapo ya nchi zinazothaminiwa na nchi ya Amerika.

Amebainisha tayari mji wa Ruiru katika eneo la lndustrial Park, kuna biashara 50 zinazoendeshwa hapo huku watu wapatao 10,000 wakifanya kazi eneo hilo

Ameongeza kuna wafanyi kazi wengine 4,000 wanaoendesha Kazi za ujenzi hadi wa leo. Aliongeza kuwa wakazi wapatao 700 pia wameweza kupata ajira.

Wakati huo pia kampuni ya Copia Global, ni mojawapo ya viwanda vinayoendesha mambo yake kwa ustadi mkubwa katika mji wa Ruiru.

Ilibuniwa mwaka wa 2013 ughaibuni na Silicon Valley Veterans, Tracey Turner, na Jonathan Lewis.

Copia Global in kampuni ya kipekee iliyo na matawi mengi kote ulimwenguni.

Kampuni hiyo inaweza huhudumia wateja wote wa kutoka tabaka mbalimbali.

McCarter amezuru kampuni hiyo yenye wafanyakazi wapatao 450.

Kazi muhimu ni kusambaza bidhaa kwa wateja wao popote walipo.

Wateja wa mijini na mashinani wanaarifiwa kutafuta huduma za Copia Global, kupitia anwani yao ya mtandao www.copia.co.ke ambapo wako tayari kusafirisha mizigo yoyote mahali popote, na wakati wowote.

Katika eneo hilo pia kuna chuo cha Nova Pioneer ambacho kinafunza wanafunzi wenye ubunifu na kupata viongozi watakaoleta mabadiliko ya kisasa katika siku za usoni.

Pia kuna shule ya msingi na ya upili yenye wanafunzi wapatao 1,500 ambao idadi imekuwa ikiongezeka kwa muda wa miaka mitatu kufikia sasa.

Bi Jackline Maigwa ambaye ni meneja wa miundomsingi katika eneo la Industrial Park, Ruiru, amesema tayari wamepiga hatua kubwa kwa kufanikisha ubora wa miundomsingi na ujenzi wa majumba ya kununuliwa na wateja.

“Tayari barabara zimejengwa hadi kufikia umbali wa kilomita 20 katika eneo hilo pamoja na umeme huku mpangilio wa kujenga majumba ya miundo tofauti ukiendelea kuwepo. Tuna imani ya kwamba kwa miezi ya hivi karibuni kutakuwa na mabadiliko makubwa ajabu,” akasema Bi Maigwa.

Alisema wataendelea kufanya kazi kwa ushirikiano wa karibu na Kaunti ya Kiambu ili kufanikisha juhudi zao za kupanua eneo hilo kuwa mji mkuu.