KCSE 2024: Idadi ya wasichana walioandika mtihani yapita ya wavulana
IDADI ya wasichana waliokalia Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE) mwaka uliopita, 2024 ni ya juu ikilinganishwa na ya wavulana.
Kulingana na Wizara ya Elimu, kwa jumla ya watahiniwa walioandika mtihani huo, Baraza la Kitaifa la Mtihani (KNEC) liliandikisha wasichana 482,202, nao vijana wakiwa 480,310.
Akizungumza wakati wa utoaji wa matokeo ya KCSE 2024 mnamo Alhamisi, Januari 9, 2025, Waziri wa Elimu, Bw Julius Ogamba alisema idadi ya wasichana waliokalia mtihani huo inawakilisha asilimia 49.9 ya idadi jumla.
“Hilo linaashiria mikakati kuhakikisha kuna usawa kijinsia kupata elimu inazaa matunda,” Waziri Ogamba akasema.
Waziri alisema ongezeko hilo la wasichana kukalia KCSE, ni la kihistoria kuwahi kushuhudiwa nchini.
Wavulana wamekuwa wakivuna kila mwaka, kwa idadi ya juu.
Kwa jumla ya watahiniwa 899,453 walioandika KCSE 2023, wavulana walikuwa 450,554, huku wasichana wakiwa 448,899, takwimu hizo zikiwakilisha asilimia 50.09 na 49.91, mtawalia.
Data za KNEC, vilevile, zinaonyesha KCSE 2022 kwa jumla ya watahiniwa 881,416, wavulana walikuwa 443, 644 wasichana nao wakiwa 437,772.
Bw Ezekiel Machogu alihudumu kama Waziri wa Elimu kati ya 2022, serikali ya Rais William Ruto ilipotwaa mamlaka kutoka kwa Bw Uhuru Kenyatta, ambaye kwa sasa ni mstaafu, Machogu akivuliwa mamlaka Julai 2024 mabadiliko katika Baraza la Mawaziri lilipofanywa.
Waziri Ogamba akizungumza katika makao makuu ya KNEC, pia alifichua kwamba idadi ya watahiniwa wa KCSE 2024 iliongezeka na kufikia 964,512, kutoka 899,453 mwaka wa 2023.
Nyongeza hiyo iliwakilisha nyongeza ya asilimia 7.19.
Ongezeko la idadi ya watahiniwa; wasichana na jumla, Bw Ogamba alisema ni thibitisho la serikali kujitolea kuhakikisha kila mtoto nchini anakata kiu cha masomo.
Waziri Ogamba alitumia jukwaa la kutangaza matokeo ya KCSE 2024, kuonya wakuu wa shule wenye tamaa kuongeza karo za sekondari kiholela, akisema inayolipwa mwaka huu, 2025, ni sawa na ya mwaka uliopita.
Baadhi ya Wakenya tayari wameelekeza ghadhabu zao mitandaoni, wakilalamikia nyongeza ya karo.