Makala

KenHA yafaa kutafuta suluhu ya kudumu eneo la Carwash katika barabara ya Thika Superhighway

September 26th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMMY WAWERU

UJENZI wa Thika Superhighway, barabara inayounganisha jiji la Nairobi na mji wa Thika ni kati ya miradi mikuu iliyotekelezwa katika enzi ya Rais (Mstaafu) Mwai Kibaki.

Barabara hiyo, maarufu kama Thika Road, ndiyo kuu nchini na ambayo inasifiwa kurahisisha shughuli za usafiri na uchukuzi mitaa iliyo pembezoni.

Isitoshe, imechangia kuimarika kwa sekta ya biashara katika jiji la Nairobi na viunga.

Huku faida zake zikiwa kibao, kwa kiasi fulani watumizi wake, ndio madereva, kuna baadhi wameigeuza kuwa ‘barabara ya mauti’.

Hata ingawa si wote wenye utepetevu, sehemu ya barabara hiyo kati ya mtaa wa Roysambu na Githurai, almaarufu Carwash inaendelea kutajwa kuwa hatari kwa madereva ambao si waangalifu.

Thika Road ni barabara yenye shughuli chungu nzima za usafiri na uchukuzi, na chini ya muda wa dakika kumi mamia na maelefu ya magari hupita.

Kwa wakazi, eneo la Carwash ni nafuu kwa sababu barabara i’ mita chache kutoka wanakoishi, hivyo basi kuelekea jiji la Nairobi, mtaa wa Ruiru, Juja, Thila au maeneo mengine yaliyoko Thika Road si hoja.

Hata hivyo, kinachohuzunisha wenyeji ni ajali za mara kwa mara kati ya Roysambu na Githurai. Kulingana na James Kithome, leni ya kasi imekuwa kiini cha maafa kwa madereva na wasafiri.

“Kila wiki, imekuwa ratiba ajali kushuhudiwa tangu nihamie Carwash mwaka uliopita, 2019,” akasema mkazi huyo.

Kithome anasema Ijumaa jioni, usiku na Jumamosi, mikasa ya ajali eneo hilo si matukio mageni.

Leni ya kuelekea Githurai, kutoka Roysambu, ni mteremko na katika daraja la watu kuvuka kati ya mitaa hiyo miwili ni mpindo wa barabara.

Mitaa chache kutoka kwenye daraja hilo, kuelekea Githurai, kwa upeo wa macho ni vigumu kuona magari yanayotoka Roysambu.

“Huenda wengi wanaohusika kwenye ajali Carwash ni wageni watumizi ambao hawaelewi muundo wa barabara kati ya Roysambu na Githurai,” mmoja wa wahudumu wa bodaboda eneo hilo akaambia Taifa Leo.

Kulingana na mhudumu huyo, Thika Super Highway ilipozinduliwa 2012, mabasi yanahodumu kati ya Githurai na jiji la Nairobi, yalikuwa yakihusika kwenye ajali mara kwa mara, ila sasa ni nadra kuyaskia kwa kile anataja kama “kutambua eneo hilo madereva wanapaswa kupunguza kasi”.

“Kati ya mwezi Mei na Septemba mwaka huu, nimeshuhudia zaidi ya ajali kumi, na kwenye mikasa hiyo kuna watu kadhaa wameangamia,” akasema.

La kushangaza, licha ya ajali hizo, hakuna vibango au ilani zilizowekwa kutahadharisha watumizi. Mamlaka ya Brarabara Kuu Nchini (KenHA) imeendelea kufumbia macho kiini cha mikasa hiyo, ikizingatiwa kuwa maafisa wake hupiga doria kila saa.

“Ukisimama pembezoni mwa eneo hilo, dakika thelathini hazitaisha kabla kuona gari la KenHA katika leni ya kasi,” akasema mkazi mwingine.

Ni katika barabara hiyohiyo ya Thika Road, eneo la Githurai, Mei 2020 taifa lilimpoteza mwanamuziki tajika wa nyimbo za Benga kwa lugha ya Agikuyu, James Githinji maarufu kama Jimmy wa Yuni kufuatia ajali mbaya.

Agosti 2019, mwimbaji mwingine wa nyimbo za Benga kwa lugha ya Agikuyu, John Ng’ang’a alamaarufu John De’Mathew pia aliangamia Thika Road eneo la Mkahawa wa Blue Post, Thika.

Mazishi ya John De’Mathew yalihudhuriwa na Rais Uhuru Kenyatta, naibu wake Dkt William Ruto, aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga, miongoni mwa viongozi wengine wakuu serikalini, ila suala la usalama Thika Super Highway halikuangaziwa.

Utepetevu, uendeshaji gari kwa mwendo wa kasi na kubadilisha njia kiholela katika leni ya kasi, ni kati ya visababishi vikuu vya ajali.