Kenya haibanduki Haiti maafisa 230 spesheli wakitua humo Jumatatu
KIKOSI kipya cha maafisa 230 wa polisi kutoka Kenya kiliwasili Haiti Jumatatu, polisi wa taifa la Haiti wamesema, wakiwa maafisa wa kwanza wa kigeni tangu Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipoidhinisha kuongezwa kwa kikosi kinachopambana na magenge nchini humo.
Hawa ndio maafisa wa kwanza tangu Februari mwaka huu kikosi hicho kilipoongezwa, msemaji wa operesheni hiyo, Jack Ombaka, aliambia Reuters, akiongeza kuwa sasa kina jumla ya maafisa 980.
Jukumu la kikosi hicho ni kupambana na magenge yaliyojihami kwa bunduki nyingi zinazosafirishwa kutoka Amerika, ambayo yamepanua ushawishi na kutawala maeneo mengi ya mji mkuu huku yakisambaa katika sehemu za kati ya Haiti katika miaka ya hivi karibuni na kuathiri vibaya uchumi wa taifa hilo.
Yakiungana chini ya umoja unaoitwa Viv Ansanm, magenge hayo yanadaiwa kuhusika na mauaji ya halaiki, ubakaji wa kikundi, uporaji na utekaji nyara katika vita ambavyo tayari vimewalazimu takriban watu milioni 1.4 kutoroka makazi yao.
Mwisho wa Septemba, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliazimia kubadilisha kikosi kilichopo sasa na kukifanya kuwa “Kikosi cha Kuzima Magenge”, baada ya idadi ya maafisa kubaki chini ya 1,000 — kiwango cha chini sana ikilinganishwa na matarajio ya maafisa 2,500.
Muundo mpya umeidhinishwa kuwa na hadi maafisa 5,500, lakini michango ya mataifa imekuwa ikijikokota. Kama ilivyokuwa awali, kikosi hicho kinategemea michango ya hiari kutoka kwa mataifa wanachama.
Kenya, iliyopewa jukumu la kuongoza operesheni ya awali, ndiyo mchangiaji mkubwa zaidi, ingawa Jamaica, Bahamas, Belize, Guatemala na El Salvador pia zimepeleka maafisa.
Amerika imesema imetoa zaidi ya dola bilioni moja kusaidia operesheni hiyo, ikijumuisha vifaa, chakula, malazi, utengenezaji wa magari na huduma za afya, lakini sasa haitaki kubeba mzigo mkubwa wa gharama kama hapo awali.
Amerika imetoa dola 15 milioni pekee katika Hazina maalum ya Umoja wa Mataifa unaofadhili operesheni hiyo, ikiwa ya pili baada ya Canada ambayo imetoa takriban dola 63 milioni.
Hakuna mchango wowote uliotolewa kwa hazina hiyotangu Agosti, kwa mujibu wa takwimu za UN.
Kwa jumla, hazina ina dola 113 milioni, kiwango ambacho ni cha chini sana ikilinganishwa na mahitaji ya awali ya zaidi ya dola 800 milioni kwa mwaka ili kufadhili kikosi hicho.