Kenya ilivyopoteza wanamichezo mahiri 2024
KWA mara nyingine kama miaka ya awali, Kenya iliwaaga wanamichezo kadhaa katika kipindi cha mwaka uliopita wa 2024, huku familia zilizowategemea zikibaki pweke.
Orodha ya waliotuaga na kusababisha mshtuko miongoni mwa mashabiki ni pamoja na mabingwa wa Dunia waliovunja rekodi pamoja na nyota wengine wa soka, mpira wa vikapu, voliboli ambao waliacha historia kwenye michezo waliyohusika.
Mwanariadha wa mbio za masafa marefu, Kelvin Kiptum ni miongoni mwa waliokatizwa maisha baada ya kufariki katika ajali ya barabarani pamoja na kocha wake Gervais Hakizimana raia wa Rwanda, 36, mwezi Februari.
Mwanariadha huyo aliyefariki akiwa na umri wa miaka 24 anasalia kushikilia rekodi ya Dunia ya mbio za marathon baada ya kukimbia Chicago Marathon kwa muda wa saa mbili na sekunde 35 mnamo 2023.
Kifo chake cha ghafla kiliwaacha wengi nchini pamoja na mataifa mengine ulimwenguni katika mshangao mkubwa siku chache tu baada ya marehemu kudai kwamba kazi yake ilikuwa “imeanza”.
Kiptum aliyekuwa baba wa watoto wawili alikuwa akilenga kukimbia Rotterdam Marathon na Paris 2024 kwa muda wa chini ya saa mbili ila ndoto yake haikutimia.
Mwaka huo huo, Kenya iliomboleza kifo cha jagina Henry Rono aliyeshindia Kenya nishani kadhaa miaka ya 70s. Rono alifariki Februari akiwa na umri wa miaka 72.
Rono alishikilia rekodi ya mita 3,000 kuruka viunzi na maji kwa zaidi ya miaka 10. Mara mbili aliweka rekodi ya dunia kwenye mbio za mita 5,000 mnamo 1978 na baadaye 1981.
Rono alivunja rekodi ya dunia katika mbio za mita 10,000 alipomaliza kwa muda wa 27:22.5), mita 5,000 (13:08.4), mita 3,000 kuruka viunzi na maji (8:05.4), mita 3,000 (7:32.1).
Mnamo Oktoba 15, 2024 hali ya huzuni ilitanda kote nchini baada ya kifo cha jagina Austin ‘Makamu’ Oduor Origi aliyekuwa nahodha wa klabu ya Gor Mahia na timu ya taifa ya Harambee Stars miaka ya 80 na 90.
Oduor ni babake aliyekuwa kipa wa kimataifa, Arnold Origi ambaye sasa ndiye mkufunzi wa makipa wa kikosi cha Harambee Stars kitakachoshiriki Mapinduzi Cup nchini Zanzibar kwa siku 10 kuanzia wikendi hii.
Jagina huyo alifariki katika hospitali moja mjini Kakamega siku chache tu baada ya kuandamana na majagina wenzake kwenye hafla ya kusaidia timu za mashindano eneobunge la Rarieda, Kaunti ya Siaya kwa mwaliko wa Eliud Owalo Foundation.
Mnamo 1987, Oduor aliongoza Gor Mahia kuweka historia ya kuwa klabu ya kwanza kutoka kanda ya CECAFA kutwaa Kombe la Washindi barani Afrika, zamani Mandela Cup.
Mwaka huo huo, Oduor, 65, alikuwa mmoja wa manahodha wa kikosi cha Harambee Stars chini ya kocha Reinhardt Fabisch kilichofika fainali ya Kombe la Michezo ya Afrika kabla ya kushindwa 1-0 na Misri ugani MISC, Kasarani.
Miongoni mwa wanasoka wengine walioaga dunia mwaka wa 2024 ni Ezekiel Otuoma aliyechezea klabu mbalimbali hapa nchini, ikiwemo AFC Leopards.
Otuoma ambaye pia alichezea Ulinzi Stars, FC Talanta, Western Stima na Muhoroni Youth atazikwa Januari 11 nyumbani kwao Ramula, Gem, Kaunti ya Siaya.
Kwa kudhihirisha ushujaa wake, zaidi ya majagina 50 walikuwa miongoni mwa watu wa tabaka mbalimbali waliohudhuria mazishi ya Austin Oduor eneo la Makunga, Kaunti ya Kakamega.
Wiki chache tu baada ya kushiriki kwenye Michezo ya Olimpiki ya Paris 2024, mwanariadha Rebecca Cheptegei raia wa Uganda aliyeishi Kenya aliaga dunia kwenye kifo cha kushangaza baada ya kuathiriwa na unyanyasaji wa kijinsia.
Cheptegei aliyekuwa na umri wa miaka 33 alifakiri baada ya kumwagiwa petroli na kuchomwa moto na mtu aliyekuwa mpenzi wake.
Ilidaiwa kwamba kisa hicho kilitokea wawili hao walipokuwa wakizozana kuhusu kipande cha ardhi Kaskazini-Magharibi mwa Kenya, ambapo alikuwa akiishi na kupata mafunzo.
Kwenye Michezo ya Olimpiki ya Paris 2024, Cheptegei alimaliza katika nafasi ya 44 na ndizo zilizokuwa mbio zake za mwisho.
Katika kifo kingine cha kushangaza, mashabiki walilia kwa uchungu baada ya kifo cha mwanavoliboli wa kimataifa, Janet Wanja atakayezikwa leo katika Makaburi ya Lang’ata.
Alhamisi, Januari 2, 2025, maelfu ya mashabiki walimiminika katika uwanja wa MISC, Karasani kutoa heshima zao za mwisho kwa jagina huyo aliyefariki akiwa na umri wa miaka 40 baada ya kuugua saratani ya kibofu cha mkojo.
Mbali na kuchezea timu ya taifa na kuisaidia kutwaa mataji mbalimbali, Wanja aliyesomea shule ya Mukumu Girls vilevile alichezea klabu za Kenya Pipeline na KCB. Ugani Kasarani video yenye hisia kutoka kwa ukumbusho wa marehemu iliwagusa waombolezaji walioonekana wakitokwa machozi.