Kenya, Uganda ‘zatuma’ Tanzania ilete kombe la Afcon na kitita cha Sh1 bilioni
NA MWANGI MUIRURI
Matumaini ya Jumuiya ya Afrika Mashariki yako katika timu ya soka ya Tanzania katika gozi la kupigania kombe la taifa bingwa barani Afrika (Afcon) ambapo pia mshindi atatuzwa Sh1 bilioni za Kenya.
Kipute hicho kitang’oa nanga nchini Côte d’Ivoire Januari 13 hadi Februari 11, 2024 huku Tanzania ikiwa katika kundi la F pamoja na Morocco, DR Congo na Zambia.
Timu hiyo ya Tanzania ikijulikana kama Taifa Stars chini ya ukufunzi wa Adel Amrouche inatamaniwa kwamba iwapo itakosa nafasi ya kwanza, basi iibuke ya pili ndio ituzwe kitita cha Sh630 milioni.
Shirika la kandanda barani Afrika (CAF) limetangaza vitita hivyo kuwa tuzo kwa mabingwa na pia atakayeibuka wa pili, hii ikiwa ni nyongeza ya asilimia 40.
Watakaotinga nusu fainali katika mitanange hiyo watajihakikishia tuzo ya Sh394 milioni kila mmoja huku watakaofaulu kuingia takika robo fainali wakijipa Sh204 milioni kila mmoja.
Vitita hivyo vimetangazwa rasmi na Rais wa CAF Dkt Patrice Motsepe akiongeza kwamba tuzo hizo ni za kusaidia watakaoshinda kukuza soka nchini mwao pamoja na kufadhili harakati za wadau kukuza vipaji na miundombinu.
Taifa Stars itawakilishwa na magolikipa: Kwesi Kawawa, Beno Kakolanya na Aishi Manula huku walinzi wakiwa ni Israel Mwenda, Mohamed Hussein, Bakari Mwamnyeto, Dickson Job, Nickson Kibabage, Lusajo Mwaikenda, Adam Kasa, Zion Chebe Nditi, Mark John na Miano Danilo.
Katikati mwa uwanja itategemea Yusuf Kagoma, Mzamiru Yassin, Sospeter Bajana, Adolf Bitegeko, Roberto Yohana, Edwin Balua, Said Hamis na Tarryn Allarakhia.
Kutikisa nyavu kutakuwa jukumu la Kibu Dennis, Adbul Suleiman, Ladaki Chasambi na Simon Msuva.
Timu zingine ndani ya kipute hicho ni Ivory Coast, Nigeria, Equatorial Guinea, na Guinea-Bissau katika kundi A huku kundi B likijumuisha Misiri, Ghana, Cape Verde na Mozambique.
Kundi la C liko na Senegal, Cameroon, Guinea na Gambia huku kundi D likiwaleta pamoja Algeria, Burkina Faso, Mauritania na Angola huku kundi E likiwa na Tunisia, Mali, Afrika Kusini na Namibia.
Mechi hizo zitaandaliwa katika nyuga za jiji kuu Abidjan, ndizo Felix Houphouet-Boigny na Alassane Ouattara Stadium.
Hizo zingine ni Yamoussoukro, Bouake, Korhogo na San Pedro.