Makala

Khadija Bakari: Mshonaji vikapu na mikeka anayetia wageni hamu ya kubakia Lamu

March 16th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

NA KALUME KAZUNGU

BI Khadija Bakari ni mama aliyejizolea sifa kochokocho ndani na nje ya kisiwa cha Matondoni, Kaunti ya Lamu kutokana na weledi wake wa kushona bidhaa mbalimbali za miyaa.

Akiwa na umri wa miaka 50, Bi Bakari amedumu kwenye biashara hiyo kwa zaidi ya miaka 30, akiwa ameianza kazi hiyo akiwa na umri wa miaka 20 pekee baada ya kurithishwa ujuzi huo na mababu na mabibi zake.

Yeye hushona bidhaa kama vile vikapu vya kuendea sokoni, vile vya kuhifadhia matunda sebuleni, vipochi vya simu na vipakatilishi, teo, mikeka na majamvi, iwe ni ya mvirongo, mraba au duara dufu.

Pia hushona vipepeo, kofia za kujikinga dhidi ya jua miongoni mwa bidhaa nyingine, zote zikitokana na kili za miyaa.

Mara nyingi utampata Bi Bakari akiwa amejibanza kwenye kibanda chake au barazani akiendeleza sanaa yake ya kushona aliyoipenda na kuienzi si haba.

Wahenga wakasema ‘Kipendacho Moyo ni Dawa.’

Ila kwa Bi Bakari, yeye kazi yake si kushona bidhaa za vivi hivi tu ilmradi ajipatie mtaji bali pia anazingatia ubunifu wa hali ya juu na wenye kuvutia.

Ni kupitia ubunifu wake katika kushona vikapu, mikeka na bidhaa nyingine ambapo huwatia wageni hamu ya kubakia Lamu.

Baadhi ya bidhaa za Bi Khadija Bakari. PICHA | KALUME KAZUNGU

Mshonaji huyu mara nyingi hutumia bidhaa zake kuuza sura ya Lamu.

Utapata vikapu, vipochi, mikeka, majamvi na bidhaa zake nyingine nyingi za miyaa zikiwa zimepambwa kwa majina kama ‘Lamu,’ ‘Amu Tamu,’ na ‘Tembea Lamu.’

Pia utapata bidhaa zake zikiwa zimechorwa nembo maalumu ya Lamu, almaarufu ‘Jicho La Lamu.’

Unaponunua bidhaa hizo basi moja kwa moja wewe unakuwa balozi kimpango wa kuiuza Lamu kwa njia nzuri.

Katika mahojiano na Taifa Leo kibandani kwake kisiwani Matondoni, Bi Bakari alisema ni kupitia ufundi wake wa kutengeneza bidhaa za miyaa ambapo amefaulu kukimu mahitaji ya familia, ikiwemo chakula, mavazi, karo ya watoto nakadhalika.

Yeye huuza bidhaa zake kwa kati ya Sh1000 kwenda juu.

Bei yake hukadiriwa kulingana na saizi au muundo na umaridadi wa bidhaa ambayo mja anahitaji.

“Nimezingatia vilivyo ubunifu kwenye ushonaji wa bidhaa zangu. Utapata vikapu au mikoba ya tarakilishi ikiwa imeandikwa au kuchorwa nembo ya Lamu, hasa hili jicho la Lamu. Unaponunua bidhaa zangu na kwenda nje ya Lamu basi unakuwa balozi wa kuiuza Lamu kule nje. Yaani mtu akikuona na bidhaa iliyoandikwa nembo ya Lamu anajua fika kabisa kwamba wewe ni wa Lamu ama umezuru eneo hili, hivyo kumtia hamu na mshawasha mwingine kuja hapa kujionea yaliyoko,” akasema Bi Bakari.

Bi Bakari anasisitiza kuwa ushonaji wa mikeka, hasa kwa Waswahili wa Lamu ambao ni wa asili ya Wabajuni ndiyo tamaduni yao ya tangu jadi.

Kwa wengi, sanaa hiyo ya kushona bidhaa za miyaa si ya kukaa darasani kufundishwa bali wameifahamu kupitia kurithishwa na mababu, mabibi au wazazi.

“Yaani ushonaji kwetu sisi ni wa kurithishwa tu. Tunakua tukiwaona mababu na wazazi wetu wakishona. Tunatazama wanachokifanya na kukinasa au kukiiga vilivyo hadi kuwa weledi kama wao. Yaani tunarithishwa hii Sanaa kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Ni Sanaa ya jadi sana,” akasema Bi Bakari.

Mshonaji huyo anasema kigezo kikuu kinachomtofautisha na washonaji wengine ni ule ubunifu wa kuweka madoido kwenye bidhaa zake anazoshona, ikiwemo nembo ya Lamu.

Hilo limemfanya kukimbiliwa na wateja wa kila tabaka, ikiwemo watalii wa ndani kwa ndani na wale wa kimataifa.

“Ubunifu wangu umevutia watu wa tabaka zote, matajiri kwa maskini. Wageni na watalii wa papa hapa nyumbani na ng’ambo pia wamekuwa wakizuru kibandani kwangu kujinunulia bidhaa tofauti tofauti zilizoandikwa majina ya kuvutia yenye asili ya Lamu. Jicho la Lamu hasa ni nembo wanayoipenda sana. Ndiyo sababu nimehakikisha kila bidhaa ninayounda ninachora hiyo nembo. Yaani nembo ya jicho ni fahari ya Lamu. Imenisaidia kuuza bidhaa zangu kwa wingi,” akasema Bi Bakari.

Anasema kwa mwezi ,yeye hakosi kati ya Sh20,000 na Sh30,000 kiasi ambaco ni mapato kutoka kwa ushonaji na uuzaji bidhaa hizo za miyaa.

Bi Khadija Bakari akiwa katika eneo lake la kazi mjini Matondoni, Lamu Magharibi. Yeye hushona vikapu na mikeka vyenye maandishi yanayouza sera ya Lamu kwa uzuri. PICHA | KALUME KAZUNGU

Aidha soko lake kubwa hujiri wakati wa maadhimisho ya kila mwaka ya Tamasha za Utamaduni wa Lamu ambazo huandaliwa kwenye mji wa kale wa Lamu.

“Wiki hiyo moja ya maadhimisho ya Tamasha za Utamaduni wa Lamu huniwezesha kuuza bidhaa zangu kwa wingi. Bidhaa ambazo ningeziuza kwa mwezi mmoja au miwili naishia kuziuza kwa juma moja tu la maadhimisho ya tamasha za utamaduni wa Lamu. Wiki hiyo mimi huingiza kati ya Sh40,000 na Sh60,000 kupitia uuzaji hizi bidhaa zangu za miyaa. Wageni na watalii wanaohudhuria tamasha hizo wanapenda sana hizi bidhaa zangu za ki Amu,” akasema Bi Bakari.

Ombi lake kwa serikali ya kaunti na ile ya kitaifa, mashirika na wahisani ni kwamba wajitokeze kuwafadhili washonaji bidhaa za miyaa Lamu ili kuwawezesha kupanua zaidi biashara au sekta hiyo.

Anasema mara nyingi changamoto zinazomkabili ni ukosefu wa soko la tayari la kuuzia bidhaa zake.

“Unapata watu wanapenda hii mikeka au bidhaa zetu za miyaa kutoka hapa Lamu lakini hawajui pa kutupata kwani tuko mashinani sana. Ukienda Mombasa, Kilifi, Malindi na mwaambao wa Pwani kwa jumla utapata hii mikeka na vikapu vya miyaa vilivyoshonwa hapa Lamu. Iwapo serikali, mashirika na wahisani watajitokeza kutupiga jeki kifedha, kututangazia biashara zetu na pia kututafutia soko nchini na mataifa ya nje tutashukuru. Maisha ni magumu kwa sasa na twahitaji kusukuma hili gurudumu la maisha,” akasema Bi Bakari.