• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 5:17 PM
Kibaoni: Eneo lililokuwa la vibandiko kuelekeza wasafiri lilivyogeuka mji

Kibaoni: Eneo lililokuwa la vibandiko kuelekeza wasafiri lilivyogeuka mji

NA KALUME KAZUNGU

KIBAONI ni mmojawapo wa miji tajika katika Kaunti ya Lamu.

Mji huo ni maarufu kutokana na kwamba barabara kuu ya Lamu-Witu-Garsen, ambayo ndio kiunganishi cha pekee kwa Kaunti ya Lamu na maeneo mengine ya nchi, hupasua katikati yake, hivyo kuugawanya mji huo mara mbili.

Mji wa Kibaoni ni muhimu eneo hilo kwani wasichokijua wengi ni kuwa ndio uliochangia kuchipuka kwa miji mingine tajika ya Lamu. Miji hiyo ni pamoja na Hongwe, Mpeketoni, Bahari, Mkunumbi, Mapenya, Hongwe, Majembeni, na Koreni.

Lakini je, ni nini hasa chimbuko la Kibaoni?

Mojawapo ya maelezo ya kimsingi ya kamusi ni kwamba kibao ni kifaa cha kuandikia kitengenezwacho kwa jiwe la grife au kipande cha ubao cha kuandikia kwa chaki au kalamu ya jasi.

Kadhalika, kibao chaweza kuwa kikalio kidogo cha ubao kisicho na kiegemeo, aghalabu kisichozidi sentimita 15.

Kibao pia kinaweza kuelezwa au kufafanuliwa kuwa kipande cha ubao kinachotumiwa kwa shughuli maalumu.

Kulingana na wanahistoria na wazee mbalimbali wa Lamu waliohojiwa na Taifa Leo, mji wa Kibaoni ulianza kama eneo la makutano lililosheheni vibao au vibandiko ambavyo majukumu yake makuu yalikuwa ni kuwaelekeza wasafiri maeneo walikostahili kuenda.

Mwanahistoria na mzee wa Lamu, Francis Chege, alifafanua kuwa vibao hivyo vilivyokithiri michoro na alama za kuwaelekeza watu kunakowapasa kuelekea vilianza kuwekwa miaka kati ya 1959 na 1960.

Kwa wakati huo, miji tajika kama vile Hongwe, Mpeketoni, Majembeni, Mapenya, Baharini, Mkunumbi, Koreni na mingineyo ilikuwa bado haijabuniwa.

Kulingana na Bw Chege, Kibaoni ndilo eneo lililochochea kuchipuka kwa miji hiyo mingine ya Lamu kwani ni kupitia vibandiko vya Kibaoni ambavyo ndivyo vilivyowaelekeza waja na kuwawezesha kutembea hadi kufikia maeneo ya mbali kabisa kuanzisha makazi.

“Sehemu nyingi za Lamu zilikuwa msitu lakini Kibaoni angalau kulikuwa na barabara au vichochoro vya waja kuingilia na kutokomea sehemu zingine nyingi za Lamu. Kibaoni lilikuwa sawa na eneo la makutano, hivyo kila aliyefika pale alisaidiwa kupitia kudurusu vibandiko vingi vilivyokuwa pale kuelezwa ni wapi walikotaka kwenda. Ni kupitia hali hiyo ambapo mwishowe k Kibaoni ilikua, ikanawiri hadi kufikia kiwango cha sasa,” akasema Bw Chege.

Waweru Kamande, mkazi wa Kibaoni, anataja kampuni mashuhuri ya mafuta ijulikanayo kama Rogers kuwa miongoni mwa vichocheo vikuu ilivyochangia kubuniwa kwa mji wa Kibaoni.

Kulingana na Bw Kamande, maafisa wa kampuni ya mafuta ya Rogers ndio waliofika eneo hilo la makutano na kuanza kuweka au kutundika vibao vya maelekezo ambavyo mwishowe viliishia kuzaa Kibaoni.

Anasema kutokana na harakati za maafisa wa kampuni ya mafuta ya Rogers za kutaka kutafuta sehemu za kuwekeza na kuingia ndani zaidi ya Lamu kuendeleza biashara ya kutafuta na kuuza mafuta, hapo ndipo walipoanza kubuni vibarabara au vichochoro na kuweka maelekezo ya vilikoelekea.

“Wasimamizi wa kampuni ya Rogers walikuwa wakiingia sehemu mbalimbali za Lamu, ikiwemo zile za ndanindani kabisa. Kwa sababu Kibaoni ndilo eneo ambalo kidogo lilikuwa sehemu ya kukutanisha vichochoro tofauti vya maeneo ya mashambani, ndipo vibandiko vikawekwa kuwaelekeza waliotaka kuingia ndani zaidi. Hapo ndipo umaarufu wa Kibaoni ulianza hadi kufikia kubuniwa na kupanuka kwa mji uliopo sasa,” akasema Bw Kamande.

Bi Mary Njuguna, mkazi wa Mpeketoni, anasema katu hawezi kusahau mchango mkubwa wa Kibaoni ambao mwishowe wanajivunia kupelekea miji mingine mikuu kuchipuka.

Bi Njuguna anataja miaka ya sabini (1970s), wakati ambapo Rais Mwanzilishi wa taifa hili, Hayati Mzee Jomo Kenyatta alizuru Lamu kwa mara ya kwanza, ambapo alipitia eneo hilo la Kibaoni.

Anasema mbali na miji, Kibaoni pia ndio iliyokuwa barabara ya kwanza iliyochangia barabara nyingine kama zile za Kibaoni-Hongwe, Kibaoni-Mpeketoni, Kibaoni-Muhamarani-Mapenya, Kibaoni-Majembeni, Kibaoni-Baharini, Kibaoni-Ziwa Kenyatta na nyinginezo kuanzishwa.

Bi Njuguna anakumbuka miaka hiyo ya 1970, ambapo hayati Mzee Jomo Kenyatta alifika Kibaoni na kisha kuelekea Ziwa Mkunguya, ambalo kwa sasa linatambuliwa kama Ziwa Kenyatta.

“Mzee Jomo Kenyatta alikula mlo wake wa mchana pale kandokando ya Ziwa Mkunguya. Kulikuwa na mti mkubwa uliompa  kivuli wakati akijivinjari kwa mlo wa mchana. Kisha baada ya mlo aliuliza mti huo mkubwa uliitwaje. Alipoambiwa mti huo ni Mpeketo, alisema basi, eneo lote hilo liitwe Mpeketoni na Ziwa Mkunguya libadilishwe jina na kubandikwa jina lake kuwa Ziwa Kenyatta. Hiyo ndiyo siku eneo la Mpeketoni na pia Ziwa Kenyatta vilizaliwa na vikadumu hadi leo. Isingekuwa Kibaoni kuunganisha maeneo haya, leo hatungekuwa majina haya ya Mpeketoni na Ziwa Kenyatta,”  akasema Bi Njuguna.

Wakazi aidha walisifu juhudi za serikali kuimarisha miundomisngi, hasa barabara kwenye eneo hilo la Kibaoni, hali ambayo imechangia mji huo kukua kwa kasi.

Anayefika Kibaoni kwa sasa atapata ni eneo lililokua kimaendeleo kwani utapata kuna kituo cha kivyake cha polisi, zahanati na pia shule ya msingi ya Muhamarani, miongoni mwa masuala mengine ya kimsingi.

“Twashukuru. Kibaoni ya sasa imeendelea vilivyo. Biashara zimenoga. Tumekuwa na maduka madogomadogo lakini miaka ya hivi punde tumeanza kushuhudia na kupokea huduma za maduka ya jumla. Pia tuko na usalama kwani kituo cha polisi kiko hapa. Tuko na hospitali na shule zetu hapa. Kujengwa kwa barabara kuu ya Lamu-Witu-Garsen pia kumeletea mji wetu natija. Mji umepanuka si haba,” akasema Bw Lucas Mwangi.

  • Tags

You can share this post!

Wakulima wa viazi wakadiria hasara baada ya bakteria...

Fahamu sababu za upole wa punda wa Lamu

T L