Makala

Kibarua kwa Joho wenyeji wakiwa na matumaini ya kufaidi madini

Na LUCY MKANYIKA July 26th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

SIKU chache baada ya Rais William Ruto kumteua aliyekuwa Gavana wa Mombasa Bw Hassan Ali Joho kama Waziri wa Madini na Uchumi wa Baharini, wakazi wa Taita Taveta sasa wana matumaini kuwa watanufaika kutokana na madini yaliyoko katika eneo hilo.

Kaunti ya Taita Taveta imejaaliwa na madini mengi yakiwemo vito vyenye thamani haswa Tsavorite, inayopatikana mbugani Tsavo pekee.

Hata hivyo, kwa miaka mingi, wachimbaji wamekuwa wakilalamikia kutonufaika kutokana na madini hayo na hivyo kutoona manufaa ya uchimbaji wao.

Iwapo ataidhinishwa na bunge, Bw Joho atarithi mipangilio mingi ya sekta hiyo katika kaunti hiyo iliyokuwa imewekwa na mtangulizi wake Bw Salim Mvurya, ikiwemo kujengwa kwa kiwanda cha chuma, wachimbaji kuruhusiwa kuchimba mbugani Tsavo, utoaji wa leseni haswa kwa wachimbaji wadogo wadogo miongoni mwa mengine.

Baadhi ya wachimbaji wa eneo hilo waliambia Taifa Leo kuwa wana matumaini kuwa Bw Joho ataweza kusukuma mbele sekta hiyo kwa manufaa ya wenyeji.

Akiongea mjini Mwatate, mwenyekiti wa wachimbaji wadogo katika kaunti hiyo Bw David Zowe, alitaja kuwa vito vya Tsavorite vimetajwa kuwa miongoni mwa madini ya kimkakati.

Alimtaka Bw Joho kuunga mkono kuondolewa kwa jiwe hilo katika orodha ya madini hayo.

“Ninashukuru Rais kwa kumteua Bw Joho na tunamuomba punde tu atakapochukua hatamu ya afisini, ashughulikie changamoto zinazotukumba sisi wachimbaji wadogo zikiwemo kuondolewa kwa Tsavorite miongoni mwa orodha ya madini ya kimkakati,” akasema.

Alisema kuwa leseni ambazo serikali inawapa wachimbaji na wauzaji wa madini kwa sasa, zimewanyima nafasi ya kuchimba na kuuza Tsavorite.

“Tunakuomba kwanza uunde mikakati na kuwasilisha ombi kwa baraza la mawaziri kukubalia uchimbaji na uuzaji wa Tsavorite,” akasema.

Vilevile, alisema kuwa wanatarajia Bw Joho kuidhinisha kamati ya kusimamia shughuli za jengo la vito lililoko mjini Voi ili liweze kutoa huduma kwa wananchi jinsi inavyopaswa.

“Tunatarajia ahakikishe wachimbaji wadogo wanapata maeneo ya kuchimba madini nje na ndani ya mbuga ya Tsavo. Bado serikali haijatupa maeneo ya uchimbaji,” akasema.

Mchimbaji mwingine Bi Mariam Chirera, alisema kuwa renchi za eneo hilo vilevile zitanufaika kutokana na shughuli za uchimbaji katika maeneo hayo.

“Mimi ni mwanachama wa renchi ya Wushumbu na tunategemea sana uchimbaji wa vito. Tunajua kuwa Bw Joho ni mchapakazi na atatusaidia kuendeleza shughuli hizo katika renchi zote 31 za hii kaunti,” akasema.

Kaunti hiyo pia imejaliwa na uwepo wa madini ya chuma katika eneo la Kishushe.

Kwa sasa, serikali inapangilia kuanzishwa kwa mtambo wa chuma unaotarajiwa kujengwa katika eneo la Ngolia na kampuni ya Devki Steel Mills.

Mtambo huo utakaogharimu Sh11 bilioni, unatarajiwa kubuni nafasi za kazi kwa mamia ya wakazi na vilevile kuboresha uchumi wa eneo hilo.

Hata hivyo, uchimbaji wa madini ya chuma katika renchi ya Kishushe umekumbwa na mizozo baina ya mwekezaji, wenye renchi na wananchi.

Kwa sasa, mwekezaji huyo, Samruddha Resources Kenya Limited, amesimamisha shughuli zake baada ya renchi ya kishushe kuwanyima kibali cha uchimbaji.

Wananchi na viongozi wa eneo hilo wamekosa imani na mwekezaji huyo kwa kutowajibika kufanya miradi ya kijamii kama inavyotakikana kisheria.

Tangu mnamo Machi mwaka jana, mwekezaji huyo alitakiwa kulipa Sh30 milioni za miradi ya kijamii lakini hadi leo, amelipa Sh25 milioni pekee.

Aidha, wenyeji wa Kishushe wamekataa kamati iliyokuwa imeteuliwa na aliyekuwa waziri Bw Mvurya kusimamia miradi itakayotekelezwa kupitia fedha hizo.