Kiberiti hiki ni adui ya sigara
Na LEONARD ONYANGO
JE, wewe ni mvutaji wa sigara na macho yako hayaoni vizuri? Hivi karibuni utakuwa kipofu iwapo utaendelea kubugia moshi huu.
Kwa kawaida uvutaji wa sigara umehusishwa na kansa ya mapafu. Kulingana na wataalamu wa afya, moshi wa sigara hutoa kemikali ambazo husababisha kansa hii. Kadhalika, moshi wa sigara huharibu mishipa katika mapafu hivyo kusababisha mwathiriwa kushindwa kupumua.
Wataalamu sasa wanasema bali na kusababisha kansa ya mapafu, sigara pia husababisha upofu.
Utafiti uliofanywa nchini Uingereza umebaini kwamba moshi wa sigara ni hatari kwa macho.
Wavutaji sigara wako katika hatari maradufu ya kupofuka macho ikilinganishwa na wenzao wasiotumia sigara, kwa mujibu wa utafiti huo.
Moshi wa tumbako umesheheni kemikali hatari ambazo hudhuru macho.
Wataalamu pia walibaini kwamba huzidisha matatizo ya macho yanayosababishwa na ugonjwa wa kisukari. Aidha huharibu mishipa iliyoko nyuma ya jicho hivyo kusababisha mwathiriwa kupofuka.
Wanaonya kuwa wavutaji sigara wako katika hatari ya kupofuka mara tatu zaidi wanapokuwa wazee ikilinganisha na wasiovuta sigara.
Pia wavutaji wako katika hatari ya kupofuka ghafla mara 16 ikilinganishwa na wenzao wasiovuta. Hii ni kwa sababu kemikali zilizomo kwenye moshi huzuia damu kusambaa kwenye jicho hivyo kulisababisha kushindwa kuona. Kulingana na Aishah Fazlanie, mmoja wa wataalamu waliofanya utafiti huo nchini Uingereza, idadi kubwa ya watu duniani wanafahamu kuwa sigara inasababisha maradhi ya kansa ya mapafu lakini asilimia zaidi ya 80 hawafahamu kuwa sigara inadhuru macho.
Wataalamu wanapendekeza kuachana na sigara kabisa.
Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kuwa asilimia 80 ya visa vya upofu vingeweza kuepukika endapo waathiriwa wangejiepusha na uraibu kama vile kuvuta sigara.
Ripoti ya WHO ya 2013, ilibaini kuwa zaidi ya sigara bilioni 6.4 zilivutwa nchini Kenya. Mnamo 2015 idadi ya sigara zilizovutwa ilipanda hadi bilioni 8. Hiyo inamaanisha kwamba Wakenya wanavuta sigara milioni 22 kwa siku.
Watu 31,000 hufariki kila mwaka humu nchini kutokana na maradhi yanayotokana na uvutaji wa sigara. Takwimu za WHO pia zinaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 40 ya watu wanaovuta sigara wamejaribu kuacha lakini kati yao ni asilimia saba pekee ambao wamefanikiwa kuachana na uraibu huo.
Lakini kampuni moja ya nchini Lebanon sasa imetengeneza kiberiti cha kielektroniki Slighter Lighter kinachowasaidia watu wenye uraibu wa sigara kukoma tabia hii.
Chakataa kuwaka
Kiberiti hicho cha kielektroniki humshauri mvutaji wa sigara kujiepusha na uraibu huo kupitia programme (app) ya simu.
Kiberiti hicho hukataa kuwaka mtumiaji anapokitumia kuwasha sigara zaidi ya mara mbili kwa siku.
Hata hivyo, watu walio na uraibu wa sigara wanaweza kukwepa kiberiti hicho na kutumia viberiti vya kawaida ili kisije kikawakosesha ‘uhondo’.
Kiberiti hicho pia hutuma arafa kwenye simu ya mtumiaji anapovuta sigara kupita kiwango kinachofaa.
“Arafa hizo zinamkumbusha mvutaji kwamba sigara ni hatari kwa afya hivyo kumfanya kupunguza. Baada ya miezi kadhaa mraibu wa sigara anaweza kuachana na uvutaji na badala yake kujiburudisha na mambo mengineo,” anasema mwasisi wa kiberiti hicho, Samer El Gharib.
Licha ya tumbako kuwa na madhara tele kwa afya, ni miongoni mwa bidhaa zinazoiletea Kenya mapato kutokana na kodi ya juu.