Kenya imepoteza ubabe wake wa kibiashara kwa Tanzania, akiri Ruto
RAIS William Ruto anaonekana kukiri kwamba chini ya utawala wake, Kenya imepoteza nafasi yake kama mbabe wa kibiashara Afrika Mashariki huku Tanzania ikiimarika pakubwa.
Na wadadisi wanasema hali inaendelea kuwa mbaya chini ya sera za serikali ya Kenya Kwanza huku mazingira ya kisiasa na kisera yakiathiri sekta tofauti na uchumi kwa jumula.
Akizungumza katika kongamano la viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki jijini Arusha Tanzania Ijumaa, Rais Ruto aliipongeza Tanzania kwa kuipiku Kenya katika biashara ya ndani kati ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
“Katika biashara kati ya mataifa yote, Kenya ilikuwa ikiongoza kwa bidhaa na huduma ambazo tunafanya biashara katika Afrika Mashariki. Leo, Tanzania imeipiku Kenya na lazima niipongeze kwa maendeleo inayofanya na kwamba idadi inaongezeka,” Ruto alisema.
Ruto pia alisema katika mkutano huo kwamba Jumuiya ya Afrika Mashariki ndiyo inayoongoza kwa biashara katika bara zima la Afrika na inawajibika kwa kati ya asilimia 25-28 ya biashara zote barani.Jumuiya ya Afrika Mashariki inajumuisha nchi nane: Kenya, Tanzania, Uganda, Burundi, Rwanda, Sudan Kusini, Somalia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
“Lazima liwe jukumu letu la pamoja kudumisha amani na usalama na uthabiti wa eneo letu,” Ruto aliongeza.Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni za Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kwa mara ya kwanza, Tanzania ilisafirisha bidhaa nyingi zaidi hadi DRC kuliko Kenya na Uganda.
Soko la pamoja
Hii ni pamoja na kwamba DRC ilijiunga na EAC mwaka 2022 ili kuchangia soko la pamoja la watu wasiopungua 300 milioni katika nchi hizo nane.
Huku bidhaa ambazo Tanzania iliuza DRC zikiongezeka, bidhaa ambazo Tanzania inauza Kenya zilipungua kutoka asilimia 6.7 hadi asilimia 4.1 kati ya 2022 na 2024.
Haya yanajiri huku kampuni kubwa zikifunga biashara Kenya na kuhamia nchi jirani kutokana na mazingira magumu yanayosababishwa na sera za utawala wa Kenya Kwanza.Procter & Gamble, Base Titanium, G4S, na Tile & Carpet ni baadhi ya kampuni za hivi punde kutangaza kupunguza wafanyakazi au kufunga shughuli zake Kenya.
Procter and Gamble (P&G) kampuni kubwa ya Amerika na Base Titanium ya Australia zinaondoka Kenya mwezi huu wa Desemba. Nyingi ya kampuni hizo zinataja changamoto za kiuchumi na kupungua kwa uzalishaji kuwa vichocheo cha kusitisha shughuli.
“Kwa kupongeza Tanzania kwa kushinda Kenya kwa biashara Afrika Mashariki, Rais Ruto alikiri ukweli kwamba sera za utawala wake zimefanya nchi anayoongoza kupoteza nafasi yake kama mbabe wa kiuchumi katika kanda hii. Hali hii huwa inajiri na athari hasi na kubwa kwa uchumi,” asema mtaalamu wa masuala ya uchumi Dkt Jeremy Waciuri.
Anasema hali ya kupoteza biashara kunachangiwa na mseto wa mambo ukiwemo ufisadi, mfumo wa sera, uthabiti wa siasa, mfumo wa ushuru na hali ya haki za binadamu.
Kuhama kwa makampuni
“Kuhama kwa makampuni kunadhoofisha uchumi. Mazingira ya siasa na sera za nchi hasa kuhusu ushuru zinachangia katika imani ya wawekezaji. Kukadamiza demokrasia na haki za binadamu ni tishio kwa uwekezaji pia na haya ni mambo ambayo yameshuhudiwa Kenya chini ya utawala wa sasa,” akasema.
Wataalamu wanasema mazingira ya kufanya biashara nchini Kenya yanaendelea kuwa magumu zaidi kwa wawekezaji ambao sasa wanatafuta mataifa mengine kuwekeza.
Hili linaendelea kuwaweka Wakenya wengi zaidi katika hatari ya kukosa ajira, licha ya ahadi ya Rais William Ruto ya kubuni nafasi zaidi za kazi.
Gharama ya kufanya biashara imesalia kuwa kero kubwa,ikifuatiwa na ushuru mkubwa na kutokuwa na uhakika wa kisiasa.
Bw Waciuri anasema sera ya serikali ya Kenya Kwanza ya kukumbatia ajira ugenini badala ya kuvutia na kupanua uwekezaji katika sekta ya viwanda nchini inafanya ipoteze nafasi yake mbabe wa kibiashara.