Makala

Nyanya mshukiwa wa ukahaba anaswa Thika

May 22nd, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

NYANYA wa umri wa miaka 67 ni miongoni mwa washukiwa 23 wa ukahaba ambao walitiwa mbaroni mjini Thika katika Kaunti ya Kiambu, ripoti rasmi ya idara ya polisi imesema.

Ripoti hiyo ya Mei 21, 2024, inaonyesha kwamba ajuza huyo alinaswa katika mtaa wa McGeorge pamoja na wanawake wengine ambao miongoni mwao ni watano walio na umri wa chini ya miaka 20.

“Wote 23 wanatarajiwa kuwasilishwa mahakamani kujibu mashtaka ya kutatiza maadili ya mji kinyume na sheria za nchi,” ripoti hiyo ikasema.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Kiambu Bw Michael Muchiri, misako hiyo ilizinduliwa baada ya wenyeji kulalamika kuhusu visa vya kusambaratika kwa maadili kupitia tabia za makahaba hao.

“Tulianzisha misako ambapo tuliwanasa hao 23 na la kushangaza ni kuona mwanamke huyo kujiuza katika mazingira sawa na ya nyanya kufanya ukahaba na wajukuu wake,” akasema.

Alisema kwamba kuna washukiwa ambao walikuwa wamekamatwa Jumatatu ambao miongoni mwao kulikuwa na wa umri uliozidi 40 na wengine wakiwa wa umri chini ya miaka 20.

“Hao wote 14 walipigwa faini ya Sh300 kila mmoja mahakamani. Tutazidi kung’ang’ana tukishirikiana na vitengo vingine vya utawala na wadau wa kijamii,” akasema.

Mwenyekiti wa Baraza la Utamaduni nchini Bw Kung’u Muigai aliambia Taifa Leo kwamba hali hiyo ni ya kusononesha na ya kutwika familia nyingi laana.

“Taswira inayokuja akilini ni kwamba mwanamume mpenda ndogondogo mjini Thika anaweza akashiriki mahaba na nyanya, bintiye na mjukuu wake. Hiyo ni laana kubwa kwa familia hiyo ya ukahaba na pia kwa mwanamume ambaye atajipata amerushana roho nao. Ni hali ambayo hata inahitaji tambiko,” akasema Bw Muigai.

Alisema kwamba atashauriana na maafisa wa usalama wahakikishe biashara ya mahaba imekaliwa ngumu katika eneo la Mlima Kenya.

“Ni vigumu kumaliza biashara hiyo kwa kuwa wanaharakati hupambana kulinda haki za binadamu zinazojumuisha hata za makahaba lakini ni ukosefu wa maadili hata kwa watu wanaofaa kuitwa nyanya kujianika kwa wanaume ambao ni kama watoto wao,” akasema.

Alidai biashara ya ukahaba ni laana tupu kwa jamii na nchi.