Makala

DONDOO: Masihara ya kondakta yamletea balaa akipokonywa simu ya abiria

Na SAMUEL MUIGAI August 18th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KOSOVO MTAANI MATHARE, NAIROBI

KONDAKTA kutoka mtaa huu alijua kilichomtoa kanga manyoya baada ya kupokonywa simu ya abiria wake.

Tangu mtindo wa kulipa kupitia Mpesa kukita mizizi nchini imekuwa kawaida kwa abiria kutuma nauli zao kwa nambari zilizobandikwa kwenye magari ya usafiri.

Majuzi tu polo mmoja aliabiri gari la kuelekea jijini na alipoangalia kushoto kulia hakuona nambari yoyote ya Mpesa kufanya malipo.

Hivyo, alimpa kondakta simu ili abonyeze nambari ambayo angetumiwa nauli hiyo. Ikatokea kwamba dirisha la kondakta lilikuwa wazi wakati huo, na katika harakati zake za kubonyeza namba kwa simu ya polo pikipiki ilipita karibu na ghafla akapokonywa simu .

Kondakta alisimamisha matatu hiyo ajaribu kumfuata mnyang’anyi lakini wapi, boda huyo alitorokea mitini na simu hiyo.

Mhudumu huyo wa matatu akamgeukia abiria mwenye simu akimuangalia kwa huruma amuonee imani ila polo hakutaka kusikia lolote.

“Hakuna utakachoniambia mimi. Unipesa pesa au simu nyingine!” jamaa alikaa ngumu.

Kondakta bado aking’ang’ana kujitetea ghafla bin vu chini alijipata amesukumwa chini na kukabwa koo.

Ilibidi dereva wake aingilie kati kwa kuahidi malipo ya polepole kwa mwenye simu.