Akili MaliMakala

Kidosho anayeoka keki, mikate tamu kwa kutumia ndizi

February 19th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

JANGA la Covid-19 lilipocharaza ulimwengu 2020, biashara nyingi ziliathirika kwa kiasi kikubwa baadhi zikiishia kufunga milango yake. 

Shirika la Afya Duniani (WHO), hata hivyo, miaka miwili baadaye lilitangaza ulimwengu kuwa huru dhidi ya gonjwa hilo lililosababishwa na virusi vya corona.

Wakati kila taifa likipambana kudhibiti makali na msambao, Wambui Kiritu, mfanyabiashara mchanga kiumri Kenya alitumia jukwaa hilo kuonyesha umahiri wake kuboresha vitafunwa.

Matunda yakiwa kati ya chakula kilichohitajika zaidi kuboresha kinga ya mwili, Wambui, ambaye ana Stashahada ya Masuala ya Usimamizi wa Hoteli, aliibuka na mbinu ya kipekee kufanya mikate kuwa kivutio.

“Kilikuwa kipindi ambacho kwenye orodha ya mahitaji ya nyumbani, chakula kiliongoza na wengi walitaka mlo bora,” anasema.

Akiwa na msingi wa masuala ya upishi kutoka Taasisi ya Utalii, Wambui alijumuisha ndizi kama mojawapo ya viungo kuoka mikate na vitafunwa.

Wambui Kiritu akirembesha keki iliyoundwa kwa kutumia ndizi. PICHA|SAMMY WAWERU

Ni shughuli iliyoanza akiwa bado anaishi kwa wazazi wake.

“Ninaridhia chakula na kusafiri, na ninaamini hakuna shida ngumu kutatua ikiwa una kipande cha mkate uliookwa kwa kutumia ndizi,” Wambui anaelezea.

Kwa mtaji wa Sh9, 450, pesa alizoomba kutoka apu moja ya huduma za mikopo nchini, aliingilia biashara ambayo kando na kuunda vitafunwa tamu na vyenye ladha, inalenga kuokoa mazao mabichi ya shambani – ndizi zilizoiva kupindukia, ambazo huishia kuoza na kutupwa.

“Nikianza, nilikuwa natumia jiko la wazazi wangu na si mara moja, mbili, tatu… wangeskika wakilalamikia unga kutapakaa kila mahali,” Wambui anakumbuka.

Hivyo ndivyo alivyoanzisha Bobo Bakes, kampuni inayooka mikate kwa kutumia ndizi zilizoiva kupindukia.

“Kwa mwezi, hutumia kati ya kilo 40 hadi 50 za ndizi na hivyo ni vipande vingi vya matunda hayo ambayo kwa sababu ya uhalisia wake huishia kuharibika na kutupwa. Ninajivunia kuwa kati ya wanaookoa wakulima na wafanyabiashara wa matunda,” anafafanua.

Mikate ya ndizi kwenye jiko la kuoka. PICHA|SAMMY WAWERU

Kulingana na data kutoka Wizara ya Kilimo, Kenya hupoteza karibu asilimia 40 ya mazao mabichi ya shambani (horticultural produce) kwa sababu ya miundomsingi duni wakati wa mavuno na baada.

Hali kadhalika, Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) la Umoja wa Mataifa linakadiria hasara ya upotevu wa matunda na mboga nchini kuwa kati ya asilimia 30 hadi 50.

Ndizi pekee, zinawakilisha asilimia 20 hadi 30 ya upotevu.

Wambui na mkopo wake, wana historia ya kushiriki kuokoa ndizi.

Tangia kuanzia kwa wazazi wake, sasa mjasiriamali huyu ana biashara inayotoa huduma za uokaji mikate kwa kutumia ndizi, iliyoko katika mtaa wa Kifahari wa Kilimani, Nairobi.

Kutoka uokaji wa mikate miwili kila siku, Wambui sasa anazalisha kati ya mikate 24 hadi 20.

Ana brandi ya bidhaa kama Nutellachocolate chipoats na blueberries, na vilevile chaguo la gluten-free.

Keki maridadi iliyookwa na Wambui Kiritu. PICHA|SAMMY WAWERU

Mbali na mikate ya ndizi, pia hutengeneza keki za hafla na vitafunwa vidogo, kwa mujibu wa maombi ya mteja.

Wanunuzi wake wakuu ni familia zenye watoto na wanaoandaa hafla kama vile kuadhimisha siku maalum ya kuzaliwa, harusi na kufuzu shuleni, kati ya nyinginezo.

“Ni furaha iliyoje kuona watoto wakiridhia bidhaa nilizounda!”

Hatua za kuoka ni rahisi mno.

“Ndizi ninazotumia, huzipondaponda na kuzichanganya na Nutella (mojawapo ya viungio anavyotumia), na miujuza hutendekeza kwenye jiko la kuoka. Harufu ya kuvutia, ni kikosi cha kunogesha mauzo,” akaambia Akilimali wakati wa mahojiano ya kipekee.

Hutoa ndizi kutoka kwa wafanyabiashara Eastleigh, Nairobi na kutoka soko la Wangige, Kaunti ya Kiambu.

“Kila kitu huwa freshi, na huandaa bidhaa kwa oda,” akadokeza.

Mkorogo wa unga na ndizi, na viungio vingine kuoka snaki. PICHA|SAMMY WAWERU

Kulingana naye, ndizi zilizoiva kupindukia ndizo bora kwa sababu ni rahisi kuchanganya na unga wa ngano na viungio vingine.

“Kila ndizi ninayotumia, ni iliyoiva sana ambayo huenda ingeishia kuharibika na kutupwa. Kumbuka, ndizi za aina hiyo hazipendwi na walaji. Ninazipa thamani, kwa kuunda vitafunwa,” anaelezea.

Shirika la Utafiti wa Kilimo na Mifugo Kenya (KALRO), linakadiria kilimo cha ndizi Kenya kinachangia asilimia 35 kwa sekta ya uzalishaji matunda, na kujumuisha ndizi kwenye chakula ni kuwapa wakulima tabasamu kimapato.

“Chaguo la ndizi zilizoiva kupindukia kama kiungo kuoka, huongeza thamani ya bidhaa kwa sababu matunda haya yana sukari, na pia huongeza ladha,” Dkt Joseph Kori Njuguna, Mkurugenzi wa Kitengo cha Utafiti wa mazao mabichi yanayochukua muda mfupi kuzalisha, katika taasisi ya KALRO akasema kwenye mahojiano.

Kuchanganya ndizi na unga wa ngano, Dr Njuguna alisema huboresha bidhaa kwa madini kama potassiumiron, na vitamin.

Kilimo cha ndizi huingizia taifa mapato ya Sh35 bilioni kila mwaka – uzalishaji wa tani metri milioni mbili.

Wambui Kiritu akipakia keki. Mfanyabiashara anayeokea keki Nairobi anasaidia pakubwa kuokoa ndizi. PICHA|SAMMY WAWERU

Ni matunda rahisi kukuza, na yanaweza kuzalishwa mfululizo kwa sababu yanastahimili mikumbo ya athari za tabianchi, hivyo basi ni mimea faafu kimapato kwa wakulima.

Kenya, ina jumla ya hekta 75, 000 zenye migomba ya ndizi, kaunti zinazoongoza kwa uzalishaji zikiwa ni Meru, Taita Taveta, Kisii, Nyamira, Tharaka Nithi, Bungoma, Homa Bay, Murang’a, Kiambu, na Kakamega.

Mwaka 2023, Kenya iliuza nje ya nchi tani 78.22 za ndizi, zilizokadiriwa kuingiza Dola (USD) 141,000, hilo likiwa ni ongezeko kutoka tani 53.16 mwaka 2022, ambazo ziliingiza Dola 74,000.

Mwaka 2021, wakati virusi vya corona vilikuwa vimeshika kasi, uuzaji wa ndizi ng’ambo uliandikisha kiwango cha chini mno, ambapo tani 6.71 zilizoingiza Dola 13,000 ziliuzwa, ikilinganishwa na tani 15.39 mwaka 2020 na tani 12.03 mwaka 2019, mauzo yaliyoleta Dola 27,000 na Dola 21,000, mtawalia.

Ufanisi wa Wambui Kiritu kwenye biashara yake, anasema umewezeshwa na matumizi ya majukwaa ya mitandao ya kijamii kama vile Instagram na Twitter, ambayo yamekuwa nguzo kuu kuhamasisha mauzo.