Kifo cha diwani maalum wa Murang’a chafichua mzigo wa bili za matibabu kwa Wakenya wengi
DIWANI maalum wa Murang’a Mark Wainaina amefariki, duru za familia zilithibitisha Jumatano, baada ya kulazwa hospitalini kwa muda mfupi lakini kwa gharama kubwa iliyoangazia mzigo wa bili za matibabu ambazo familia zinabeba.
Kulingana na taarifa ya Eric Mwangi kwa niaba ya familia, Bw Wainaina alifariki katika hospitali ya Karen ambapo alilazwa wiki jana kutokana na matatizo ya mapafu.
Bw Wainaina anayetoka eneo bunge la Kangema alisemekana kupatwa na matatizo ya mapafu yake na kuhitaji matibabu maalum.
“Mpendwa wetu alikuwa amemaliza bima yake. Alikuwa akitegemea teknolojia ambayo inapatikana hapa nchini katika hospitali ya Karen,” taarifa hiyo ilisema kwa sehemu.
Bw Mwangi alisema “kinyume na uvumi uliochapishwa mtandaoni kwamba jamaa zetu wameacha nyuma bili ya hospitali ya Sh40 milioni, deni ni ndogo kuliko hilo.”
Alifichua kuwa makadirio ya muda wa kulazwa kwa Bw Wainaina ni takriban siku 60 kwa gharama ya kila siku ya Sh500,000 kwa siku.
“Alilazwa kwa takriban siku tano. Pamoja na gharama nyingine zilizoambatanishwa na bili hiyo haikuwa kama ilivyoripotiwa,” alisema.
Mnamo Oktoba 18 2024, Wainaina alichapisha kwenye ukurasa wake wa Facebook kwamba “Niliwahi kutoa hotuba shuleni…ambapo inasemekana elimu ni bora kuliko pesa…Pesa, tafadhali nisamehe. Nilikuwa wa umri mdogo” .
Taarifa yake ya hivi punde kwa umma pia ilikuwa ya tanzia kufuatia kifo cha binti ya mfanyakazi mwenzake, Seth Nyakio, 23, aliyepatikana ameuawa katika eneo la Biafra Estate mjini Thika mnamo Oktoba 14, 2024.
Alikuwa bintiye MCA Maalum wa Kirinyaga Bi Lucy Njeri.
Mnamo Novemba 1, 2024 alichapisha ujumbe ambao watumiaji wengi wa mtandao wameshindwa kuung’amua.
Alichapisha: “Fikiria unasema nimefilisika kwa sababu siwezi kukununulia kitu ambacho huwezi kujinunulia. Tunaishi katika ulimwengu mbaya.” ujumbe ambao wengi walichukulia ulikuwa wa dhihaka kwa maskini.
Siku moja kabla ya kuugua, Bw Wainaina alichapisha kwamba “siri ya kubaki kijana ni kuishi kwa uaminifu, kula polepole, na kusema uwongo kuhusu umri wako. Bwana mpendwa, nisaidie kuhesabu umri wangu kwa marafiki, sio miaka. Hesabu maisha yangu, kwa tabasamu, sio machozi.Najitakia heri siku ya kuzaliwa kwangu”.
Mnamo Jumanne, Gavana Irungu Kang’ata alikuwa ametangaza mipango ya kuandaa harambee siku ya Ijumaa jijini Nairobi ili kusaidia MCA kulipa bili ya hospitali.
“Kundi la madiwani wa bunge la Kaunti ya Murang’a linakualika kwa hafla ya kuchangisha pesa ili kumsaidia mmoja wa mwanachama wetu… Bw Wainaina ambaye amepatikana na ugonjwa mkali wa mapafu ambao umesababisha mapafu yake yote mawili kushindwa kufanya kazi,” Kang’ata alikuwa amesema katika taarifa yake.
Wajumbe wa bunge la kaunti na wafanyikazi walikuwa wameheshimu ombi la kuchangia damu ili kumsaidia Bw Wainaina kukabiliana na ugonjwa wake.
Zaidi ya hayo, Kang’ata alikuwa amefichua kuwa alikuwa amejadiliana kuhusu masharti nafuu ya bili huku juhudi zikifanywa kufidia bili hiyo kubwa.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA