• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
Kifo cha Jenerali Ogolla chatajwa pigo kwa urejeshaji amani Bondeni

Kifo cha Jenerali Ogolla chatajwa pigo kwa urejeshaji amani Bondeni

NA OSCAR KAKAI

VITA dhidi ya wizi wa mifugo na utovu wa usalama Kaskazini mwa Bonde la Ufa vimekuwa kibarua kigumu kwa serikali zote ambazo zimekuwepo.

Vimepata pigo kuu kufuatia kifo cha Mkuu wa Majeshi nchini Kenya, Jenerali Francis Omondi Ogolla.

Kulingana na wadau wa amani na wakazi, itachukua kipindi kirefu kuafikia ndoto ya Jenerali Ogolla ya kuangamiza ujangili kabisa.

Mzee wa Baraza la Jamii ya Pokot, Harrison Loyatum, anasema kuwa kuna haja ya kujenga kambi ya kijeshi eneo hatari la Chesegon ambayo mkuu huyo wa jeshi alipanga kujenga.

Anasema kuwa kambi hiyo inafaa kuitwa ‘General Ogolla Kerio Valley Security Camp’ kusaidia kuimarisha usalama kwenye mpaka wa kaunti za Pokot Magharibi na Elgeyo Marakwet.

“Jenerali Ogolla alikuja eneo la Chesegon kuangalia ujenzi wa kambi ya jeshi na akafia eneo hilo. Tunahitaji kambi hiyo ipewe jina lake,” akasema Bw Loyatum.

Anasema kuwa eneo hatari la Lami Nyeusi pia linafaa kuwa na kambi kubwa ya kudumisha usalama.

Bw Loyatum anasema kuwa Jenerali Ogolla alikuwa na nia ya kukomesha ujangili katika eneo hilo.

“Itachukuwa muda kwa mipango ambayo alikuwa nayo kutekelezwa,” anasema.

Bw Loyatum anasema kuwa jamii hasimu za eneo hilo zinafaa kuacha wizi wa mifugo kwa sababu suala hilo limepatia serikali gharama kubwa kulishughulikia.

Askofu Jimmy Gor wa Kanisa la Victory Life International (VLI) ambaye pia ni mratibu wa Shirika la Christian Impact Mission (CIM) ambalo hufanikisha amani kwa kubadilisha vijana wanaoasi ujangili eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa anapongeza kazi ya jeshi akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya idara za usalama na jamii za mashinani.

“Nina uchungu moyoni nikikumbuka mafanikio ya Jenerali Ogolla. Nilifanikiwa kukutana naye mwaka jana kwenye hafla ya Life Ministry Kenya ambapo sisi wote ni washirika. Mapenzi ya Jenerali Ogolla kwa Mungu na nchi yetu yalidhihirika kwenye mazungumzo yake. Alikuwa na mipango maalumu na suluhu ya kudumu kutatua visa vya utovu wa usalama eneo la Bonde la Kerio na eneo zima la Kazkazini mwa Bonde la Ufa ambapo mimi hufanya miradi ya amani na shirika la CIM,” anasema Askofu Gor.

Askofu Gor anasema kuwa kwa bahati mbaya, kujitolea kwa Jenerali Ogolla kulichangia kifo chake akizuru shule ambazo zilikuwa zinakarabatiwa na wanajeshi.

“Kumpoteza ni pigo kwa juhudi za amani lakini hatuwezi kurudi nyuma. Ushirikiano wetu na vikosi vya usalama unaonyesha kujitolea na kuendeleza maendeleo kwa jamii zetu,” anasema.

Askofu wa Kanisa la African Inland Church (AIC) eneo la Pokot, David Kaseton, anasema kuwa tayari ukarabati wa shule za eneo hilo umeathirika na matumaini kudidimia.

“Wanajeshi ambao walikuwa wanajenga shule hizo sasa wameshtuka na wako na hofu. Hatujui sasa kama shule hizo zitafunguliwa. Jenerali Ogolla amekuwa akiwapa motisha. Watangojea jenerali mwingine. Ogolla alikuwa tayari kuwafurusha majangili ambao hujificha kwenye misitu ya Kamologon na Embobut,” anasema.

Naye Balozi wa amani Tegla Lourupe ambaye alizungumza na Taifa Leo kwa njia ya simu akiwa jijini Madrid, Uhispania, anasema kuwa nchi kwa ujumla itaumia kutokana na kifo cha Jenerali Ogolla.

Anasema kuwa Jenerali Ogolla alikuwa na mapenzi kuhusu spoti kwa kuwashirikisha vijana ambao waliasi ujangili.

“Alikuwa akisukuma kuajiriwa kwa vijana walioasi ujangili hata kama hawajasoma kiwango cha kuhitimu kujiunga na vikosi vya usalama. Nilikutana naye juzi kwenye mbio za nyika za Nairobi Highway na akasisitiza kuhusu elimu ya watoto wa eneo la Bonde la Kerio. Pia nilifanya naye kazi eneo la Tana River kuhusu masuala ya amani. Nilipenda maneno yake. Kifo chake ni pigo kwetu,” akasema Bi Lourupe.

Joseph Akoule, ambaye ni mratibu wa Shirika la Sikom, anasema kuwa kifo cha Ogolla kitaathiri maendeleo katika eneo la bondeni.

“Jenerali Ogolla hakuwa mtu wa kujipiga kifua. Alijua jinsi ya kuhusisha jamii na kusikiza matakwa yao. Alitumia mazungumzo. Mazungumzo yake hayakuwa kama ya watu wengine ambao hawajakuwa wakihusisha jamii. Mazungumzo yake ya mwisho katika shule ya upili ya wavulana ya Cheptulel yanaonyesha kuwa ni mtu mnyenyekevu na alikuwa amejitolea kukomesha uhalifu bila kutumia nguvu kuondoa silaha haramu bali kupitia kubadilisha akili ya wakazi,” anasema Bw Akoule.

Mbunge wa Kapenguria Samuel Moroto anasema kuwa kupitia uongozi wa Jenerali Ogolla, kulikuwa na mipango ya kujenga mabwawa ya maji, kufanya kilimo cha unyunyiziaji maji mashamba na kufungua barabara kama njia mbadala ya kuleta amani eneo hilo.

“Wanajeshi walikuwa wameanzisha miradi za kuinua uchumi wa eneo hili. Kumekuwa na usalama bila kutumia nguvu wakazi wanaomiliki silaha haramu wakizisalimisha,” anasema Bw Moroto.

Anasema kuwa Bw Ogolla alikuwa na mpango kwa kuimarisha miundomsingi kwa kurejesha huduma za kijamii kuleta maendeleo ambayo yatakuwa suluhu ya kudumu kwa amani katika jamii za wafugaji.

  • Tags

You can share this post!

K’Ogalo walemea Ingwe tena Tusker ikipepeta Ulinzi

Msiba wa mwana wamleta hadharani ‘mpoa’ wa KarehB

T L