Kifo cha Papa Francis chaibua kumbukumbu ya ziara yake Kenya
KIFO cha Papa Francis, Mkuu wa Kanisa Katoliki ulimwenguni na kiongozi wa jiji la Vatican Jumatatu, kimezua kumbukumbu kwa Wakenya na Bara Afrika.
Papa Francis alihiari kutembelea Afrika kama bara la kwanza alipochukua uongozi mnamo Machi 2013 kufuatia kujiuzulu kwa mtangulizi wake Papa Benedict XVI kutokana na ukongwe na maradhi.
Papa alitembelea Kenya kwa siku tatu kutoka Novemba 25-Novemba 27, 2015, ziara ambayo ilisherehekewa na raia ikizingatiwa idadi ya waumini wa kanisa Katoliki nchini ni juu.
Hii ilikuwa ziara yake ya kwanza nchini na alikuwa Papa wa pili kutembelea Kenya baada ya John Paul II, ambaye alitembelea Kenya mara tatu wakati wa utawala wake.
Papa Francis alitembelea Kenya wakati wa enzi za Rais Uhuru Kenyatta ambaye naye ni muumini wa Kanisa Katoliki. Akiongea katika Ikulu ya Nairobi wakati huo, Papa aliirai serikali iwashirikishe vijana kwenye uongozi wake.
“Vijana ndio mali na tegemeo la nchi. Serikali inastahili kuwekeza, kuwalinda na kuwasaidia ili wawe na maisha mazuri. Mwongozo kwa vijana utawasaidia kuwa na hekima, chakula cha kiroho na kuwa na roho nzuri,” akasema Papa.
Aliongeza kuwa Kenya ni taifa ambalo limebarikiwa kwa kuwa ina maziwa makuu, mito na maliasili tele.
“Naomba serikali ishughulikie maslahi ya vijana. Tuwasaidie vijana kutimiza ndoto zao kwa sababu tuko katika taifa ambalo limebarikiwa,” akaongeza.
Wakati wa ziara yake, Papa alikutana na Rais Kenyatta, hafla ambayo ilihudhuriwa pia na viongozi wa upinzani, nchi ikiweka kando tofauti za kisiasa.
Mikutano na Rais Kenyatta iligusia amani nchini, umuhimu wa umoja na vita dhidi ya ufisadi serikalini. Akihutubia Bunge, Papa alitoa wito kwa viongozi wote washirikiane kupambana na ufisadi.
Wakati wa ziara hiyo Papa Francis alizuru kanisa la St Joseph inayopatikana mtaa wa Kangemi.
Alizuru kanisa hilo na kujionea jinsi wengi walivyokuwa wakiteseka kwenye mitaa ya mabanda huku akitoa wito kwa serikali kusaidia kuimarisha maisha yao.
Wakati wa ziara hiyo alisikitika kuwa wengi hawakuwa wakipokea au kunufaikia huduma za serikali.
“Kuna tatizo kubwa kwa sababu hakuna miundomsingi bora na raia hawapati huduma za kawaida. Namaanisha vyoo, mabomba ya kupitisha majitaka, uzoaji wa takataka, umeme, barabara, shule, hospitali, viwanja na mahitaji mengine ya kimsingi,” akasema Papa Francis.
Hasa aliirai serikali iwachimbie wanaoishi mitaa ya mabanda visima ili kuhakikisha nao pia wana maji safi ya kunywa na kuhakikisha kuna viwango vya juu vya usafi.
Papa pia alihudhuria na kuongoza misa takatifu katika Chuo Kikuu cha Nairobi ambapo jukwaa bora lilijengwa alikohutubia. Misa hiyo ilihudhuriwa na halaiki ya raia wakiongozwa na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta ambaye alikuwa uongozini wakati huo.