Kifo cha uchungu cha tineja aliyebakwa, kudungwa kisu na kumwagiwa asidi
NA MWANGI MUIRURI
MNAMO Aprili 7, 2024, msichana wa umri wa miaka 18 kutoka Kaunti ya Murang’a alifika ndani ya baa moja iliyoko katika mtaa wa Kenol katika sherehe ya mwenzake aliyekuwa akisherehekea siku yake ya kuzaliwa.
Msichana huyo, ambaye kwa sasa ameshazikwa, alikuwa amekamilisha Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE 2023) na alikuwa ameambia wazazi wake kutoka kijiji cha Kangangu kilichoko eneobunge la Maragua kwamba alikuwa ameenda kutembelea rafiki yake wa kike katika mtaa huo wa Kenol.
Lakini safari hiyo ya sherehe iligeuka kuwa masikitiko makuu katika maisha ya msichana huyo ambaye alilazwa katika hospitali moja ya kibinafsi katika mtaa huo wa Kenol akiwa na ulemavu mkuu.
Shida ilitokea wakati msichana huyo na wenzake wengine walijivinjari katika baa hiyo kuanzia saa moja hadi saa tatu usiku na kisha wakaamua kuhamia hadi baa nyingine iliyo karibu na hiyo ya kwanza.
Ripoti ya polisi ambayo iliandaliwa katika kituo cha polisi cha Kabati ilisema kwamba “msichana huyo alibishana na baadhi ya wanaume katika baa hiyo ya pili, hali iliyoishia kupatikana kwake akiwa ametupwa kando mwa barabara ya Thika-Kenol, kilomita mbili kutoka baa hiyo.
“Alikuwa na majeraha ya kudungwa mara mbili kwa kisu tumboni na kisha mwili wake kumwagiwa kemikali iliyomchoma upande wake wa kulia wa kichwa, kifuani na mapaja hadi kwa miguu,” ripoti hiyo ilisema.
Maafisa wa polisi waliofika katika eneo ambapo msichana huyo alikuwa ametupwa walisema katika taarifa yao kwamba walimpata akiwa hali mahututi na wakampeleka hadi katika Hospitali Kuu ya Thika lakini wakapata madaktari wamegoma.
Ndipo alipelekwa hadi hospitali nyingine mbili za kibinafsi lakini akakosa kupokelewa kwa kukosa pesa.
Mamake msichana huyo Bi Esther Njeri aliambia Taifa Jumapili kwamba “mimi mamake msichana huyu nilisononeka kiasi cha kutojielewa”.
Baada ya kukaa hospitalini kwa zaidi ya mwezi mmoja, Wambui aliaga dunia mnamo Mei 25, 2024, huku akiwa na bili ya Sh2.1 milioni na ambazo kupitia kwa ushirikishi wa Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Kaunti ya Murang’a Bi Betty Maina, Rais William Ruto alituma mchango wake wa Sh1.5 milioni.
Katika mazishi ya Wambui yaliyoandaliwa mnamo Juni 7, 2024, katika kijiji cha Karugia kilichoko Kaunti ya Murang’a, Bi Maina alilalamika kwamba “hadi sasa polisi wanazubaa na hakuna mshukiwa ambaye ametiwa mbaroni”.
“Ningetaka kuwaambia maafisa wa polisi kwamba hili sio suala la mzaha na ikiwa hamtamkamata yeyote aliyehusika, basi mjiandae kwa hali ambapo nitamshawishi Rais atoe sauti kuhusu mwendazake na haki yake,” Bi Maina akasema.
Mzazi – Bi Njeri – alisema kwamba “mimi ninaomba serikali ichunguze kisa hiki hadi iwakamate waliohusika”.
“Ningalikuwa na ufunuo kwamba haya yangalimtokea mwanangu ningalikataa atoke nyumbani kwangu siku hiyo na ikiwa ni lazima angalienda, basi mimi ningaliandamana naye hadi kwa hiyo baa bila kujali kwamba mimi nimeokoka katika imani ya Kikristo ndani ya kanisa la Akorino,” akasema Bi Njeri.
Babake marehemu, Bw Peter Kirii, alisema kwamba kuna ushahidi wa kutosha kuhusu waliohusika na ukatili huo na ni jukumu la maafisa wa polisi kuwanasa na kuwabebesha lawama mahakamani.
Kamanda wa polisi wa Murang’a Bw Kainga Mathiu alisema kwamba kisa hicho kinachunguzwa “na hivi karibuni tutawanasa washukiwa”.
Ni hali ambayo imezua hasira nyingi katika jamii kiasi cha kumfikia Waziri wa Jinsia Bi Aisha Jumwa ambaye ameonya maafisa wa usalama wa Kaunti ya Murang’a kwamba ni lazima wachunguze kisa hicho na waliohusika wakamatwe na wawajibishwe mkondo wa sheria.
“Mimi nimearifiwa kwamba waliohusika katika kisa hicho ni watu wanaojulikana. Ni watu walio na uhusiano wa karibu na mwathiriwa na ningetaka kutoa mwelekeo wa kiserikali kwamba ni lazima wakamatwe na washtakiwe,” akasema Bi Jumwa.