Makala

Kigogo: Tamthilia inayotabiri kuporomoka kwa viongozi madhalimu

March 20th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Tamthilia ‘Kigogo’ yake Pauline Kea Kyovi. Picha/ Wanderi Kamau

Mwandishi: Pauline Kea

Mchapishaji: Storymoja Publishers

Mhakiki: Wanderi Kamau

Kitabu: Tamthilia

Jina la Utungo: Kigogo

Kurasa: 94

WATAWALA madhalimu daima huishia katika majuto makuu. Hakuna wakati ambapo ukatili wao utadumu milele wakiwanyanyasa raia.

Ni ujumbe mkuu anaowasilisha mwandishi Pauline Kea Kyovi kwenye tamthilia ‘Kigogo.’

Ni kitabu kinachourejelea utawala kandamizi wa Majoka, kiongozi wa jimbo la Sagamoyo.

Majoka anaibuka kuwa kiongozi katili, anayewatesa raia kutokana na miongozo potoshi anayopewa na mshauri wake mkuu, Bw Kenga kuhusu njia za kuwakabili na kuwanyamazisha wapinzani wake.

Kwanza, wakazi wa jimbo hilo hawapati huduma muhimu, kama usafishaji wa maeneo kama soko licha ya kulipa kodi.

Haya yanajitokeza kupitia mazungumzo ya wahusika Sudi, Kombe na Boza, ambao ni wachonga vinyago.

Majoka anatoa kauli mpya, ambapo soko la Chapakazi linafungwa ili kuwaruhusu Wanasagamoyo “kushiriki kikamilifu” katika sherehe za uhuru.

Kimsingi, hili ndilo soko la pekee ambalo linategemewa na maelfu ya wakazi kupata riziki yao ya kila siku.

Hata hivyo, kauli hiyo inapingwa na baadhi ya watu waliokuwa wamechoshwa na maovu ya Bw Majoka.

Watu hao wanaongozwa na mhusika Sudi, Tunu, Siti kati ya wengine.

Wanahisi njama ya hila, jambo linalobadilika kuwa ukweli, kwani mpango uliopo ni kulifunga soko ili kumruhusu Majoka kujenga hoteli kubwa ya kisasa.

Tunadhihirishiwa maovu mengi yanayoendelea, ikiwa ni pamoja na migomo ya wafanyakazi muhimu kama madaktari kwa kutolipwa mishahara.

Walimu pia wanagoma wakiwa likizoni wakilalamikia mishahara duni.

Unyakuzi wa ardhi, ufisadi, uzandiki, uhatinafsi, hadaa kati ya maovu mengine ndiyo yanajitokeza kuwa mihimili mikuu ya uongozi wa Majoka.

Ili kufanikisha ujumbe zaidi, mwandishi anatumia mbinu ya mchezo ndani ya mchezo (uk 78-83) ambapo Majoka anazungumza na babu yake, anayemwonya kuhusu matokeo ya udhalimu wake.

Harakati za ukombozi zinaendelea ambapo upeo wake ni wakati Tunu, Sudi na wanaharakati wengine wanafanikiwa kuwakusanya maelfu ya Wanasagamoyo katika uwanja wa soko la Chapakazi wakimtaka Majoka alifungue.

Vibaraka wote wa Majoka wanamgeuka na kujiunga na raia.

Kupitia kwa Tunu, mwandishi anaonyesha kuwa wanawake wana uwezo wa kuleta mabadiliko ya kimfumo katika jamii, kinyume na dhana kuwa wao ni dhaifu.

Maudhui makuu tamthiliani ni utawala mbaya, tamaa ya uongozi, mapinduzi kati ya mengine.

Mbinu kuu za lugha zinazojitokeza ni utabiri, kinaya, jazanda na uhuishi.

Ni tamthilia nzuri, kwani inaakisi hali halisi ya hali ilivyo katika nchi nyingi za Afrika.

Baruapepe ya mhakiki: [email protected]