Makala

Kiini cha Mlima Kenya kuwa ngome ya siasa za pombe

Na MWANGI MUIRURI September 4th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KWA miongo mitano iliyopita, eneo la Mlima Kenya limekuwa ngome ya siasa za pombe.

Siasa hizi bado huenda zikaelekeza siasa za uchaguzi mkuu wa 2027.

Huku wanasiasa wakishirikisha suala hilo katika midahalo ya kisiasa, maafisa wa usalama wanachukulia sekta ya pombe kama chanzo cha maovu.

Kwa upande wao, wamiliki wa baa, baadhi yao wakiwa watengenezaji pombe haramu, wanasemekana kuendelea kutetea uwepo wa sera bora kwa biashara hiyo.

Duru zinasema kuwa wamebuni njia za kushawishi majopo kazi yanayobuniwa kudhibiti sekta hiyo.

Biashara hiyo ni kubwa kiasi cha kushawishi siasa, dini, utamaduni na uchumi katika eneo la Mlima Kenya.

Hii ndiyo maana imekuwa vigumu kwa kampeni za kupambana na pombe haramu; juhudi zinazoanzishwa kila mara na kukosa kufaulu.

Wakati huu, Rais William Ruto amempa naibu wake, Prof Kithure Kindiki kibarua cha kupambana na kero hilo ambalo, aghalabu, husababisha maafa.

Waziri wa Usalama, Bw Kipchumba Murkomen amekuwa akizunguka maeneo mbalimbali ya Mlima Kenya akiapa kuangamiza jinamizi la pombe haramu, wenye mabaa wasio na leseni na maafisa fisadi wa usalama wanaoendeleza biashara hiyo.

Bw Murkomen anadai kuwa zaidi ya asilimia 55 za pombe zinazouzwa nchini ni haramu na huwa hazilipiwi ushuru.

Anasema faida kutokana na biashara hii huwapa wahusika nguvu za kushawishi sera, vita vya kuiangamiza na hata siasa.

“Ninawajua wafanyabiashara ambao huunda leseni bandia na kutengeneza pombe na wakauza kwa ushirikiano na baadhi ya maafisa wetu. Aidha, maagizo mabovu ya mahakama yamefunga mikono yetu,” Bw Murkomen akasema akiwa Kiambu mnamo Julai 31, 2025.

Lakini kiongozi wa chama cha Democracy for Citizens’ Party (DCP) Rigathi Gachagua amemsuta Rais Ruto kwa kuhujumu vita dhidi ya pombe haramu “kimakusudi”.

“Nilipohudumu kama naibu wa rais kati ya 2022 na 2024 tulipunguza kabisa pombe eneo la Mlima Kenya.

“Vijana walitambua uwezo wao, familia zilipona na idadi ya watoto wanaozaliwa ilipanda. Nilipoondolewa waliruhusu janga hili kurejea ili kuniharibia sifa,” akasema.

Kujibu madai hayo, Bw Murkomen na Prof Kindiki wamechukua hatua kali ikiwemo kumtuma Naibu Mkuu wa Kikosi cha Recce Clinton Kimaiyo kuongoza vita dhidi ya pombe katika Kaunti ya Murang’a.

Aidha, wamempandisha cheo Joshua Nkanatha kuwa Kamishna wa Ukanda wa Kati kutokana na kazi yake nzuri ya kupambana na magenge ya wahalifu.

Hata hivyo, wakosoaji wanasema hatua hiyo haiwezi kuzaa matunda.

“Makanisa yanalalamika, wanasiasa wanapaza sauti, wazee wanatetea Muratina wakidai ni kinywaji cha kitamaduni na familia zingali zinaaathiriwa na uraibu wa pombe,” akasema Askofu Edward Nyutu, Mwenyekiti wa Muungano wa Madhehebu ya Kiasili eneo la Kati mwa Kenya.

Viongozi wa makundi ya kibiashara pia wanaisuta serikali kwa kuendesha kile wanachotaja kama “vita butu” dhidi ya pombe.