Kijana anayeuguza majeraha baada ya kuvizia mke wa polisi
NA MWANGI MUIRURI
POLISI katika Kaunti ya Embu wanachunguza kisa cha mnamo Jumapili, Februari 25, 2024 asubuhi ambapo mwanamume wa miaka 25 alivunjika mkono baada ya kuruka kutoka nyumba ya mwanamke wa wenyewe iliyo katika ghorofa la nne.
Kwa mujibu wa mkuu wa Uchunguzi wa Makosa ya Jinai (DCI) eneo la Mashariki mwa Kenya, Bw Benson Kasyoki, kijana huyo anashukiwa kwamba alikuwa akirushana roho na mke wa wenyewe.
Mzee wa boma, hata hivyo, alifika bila kutarajiwa.
Ili kuhepa adhabu ya mwanamume kuchafuliwa mzinga, kijana wa watu aliamua kuruka mzimamzima hadi kwa hatari ya mauti lakini mazingaombwe ya usherati yakawa na subira, akanusurika mauti.
“Kisa hicho cha mtaa wa Sunrise katika viunga vya Mji wa Embu kilimwacha mwaathiriwa ambaye ametambuliwa kama Daniel Mwinzi, akiwa na mkono uliovunjika kando na majeraha mengine mwilini,” akasema.
Alisema kwamba inaaminika kwamba kijana huyo alikuwa amekesha katika nyumba ya mwanamke huyo kwa kuwa bwana wa nyumba ni afisa wa polisi aliyekuwa katika doria.
“Bwana wa nyumba alikuwa anatarajiwa kufika nyumbani mwendo wa saa tatu asubuhi lakini akajitokeza saa kumi na moja asubuhi. Baada ya kubisha afunguliwe, kijana mzinifu hakuwa na lingine ila tu kuruka kutoka kwa nyumba hiyo,” akasema.
Alisema kwamba jumba hilo linachunguzwa kubaini hali ambayo mtu anaweza akaruka, akilitaja kuwa hatari kwa usalama wa wapangaji.
Kisa hicho kiliripotiwa na chifu wa mtaa huo ambaye alitambuliwa kama Bw Sammy Njagi.
Chifu huyo aliwasilisha taarifa kwamba aliitwa na wapangaji wengine wakimfahamisha kwamba kuna ajali iliyokuwa imetokea katika jengo hilo.
“Chifu alifika kwa haraka na akapata mwanamume huyo akiwa na nusu ya uhai wake huku akipiga nduru kwa maumivu. Mkono wake wa kulia ulikuwa umefura sana ishara ya kuvunjika huku akiwa hoi hata bila uwezo wa kusimama,” akasema Afisa Kasyoki.
Alisema kwamba mwanamume huyo aidha alikuwa ameonekana usiku wa kuamkia mkasa akiwa pamoja na mwanamke huyo wakiburudika ulevi.
“Kwa sasa mwanamume huyo amelazwa katika hospitali ya Embu akiwa na majeraha kadha. Tumerekodi taarifa kutoka kwa mwanamke huyo pia. Tumekuwa na busara ya kutohusisha mzee wa boma kwa kuwa hatutaki kuvunja ndoa ya mwingine,” akasema.
Bw Kasyoki alisema kwamba kwa sasa hakuna kisa cha ukiukaji sheria ambacho kimedadisiwa kutokana na tukio hilo.