• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 8:55 PM
KIJIWENI: Watetezi wa usawa, tukimbie wapi tulioambiwa hatutoshi?

KIJIWENI: Watetezi wa usawa, tukimbie wapi tulioambiwa hatutoshi?

Na DKT CHARLES OBENE

JAMANI wapi usawa katika dunia hii ambamo watu wanatumbuana usaha?

Maskini haoni cha tajiri naye tajiri hana haja na masikini.

Ndio usawa huo?

Nilidhani kwamba tumekwisha zika fikra na mawazo duni walizotumia mabepari walalahai kuwadunisha kina yakhe walalahoi.

Nilidhani hatupo tena katika enzi za “ana nini yule?”

Nilidhani tumo ndani ya utandawazi – dunia inayozingatia haki, tena inayoheshimu mchango wa kila mmoja katika jamii. Nilidhani tunaishi katika dunia ya usawa japo sijui kasawazisha nani! La hasha!

Kijana mmoja ameingia mafichoni akihofia maisha yake baada ya kutishiwa kwa sababu ya mapenzi.

Tangu kumpenda na kutangaza wazi kwamba alikuwa radhi kumposa binti mmoja kutoka familia tajika, amekumbana na mengi yaliyomfanya kujutia mapenzi katika dunia hii ya usawa! Kosa lake lipi?

Alikuwa mwinyi miaka ya nyuma akihudumia familia ile ile.

Wenyewe wanasema haiwezekani mwinyi kuposa katika familia yao! Ndio dunia ya usawa hiyo! Tusemeje akina sisi tunaokula na kulala mapipani, tena watoto wa yaya tuliozaliwa kwenye koka zilizojaa nguvu, mamlaka, madaraka na pesa? Tufanye nini akina sisi tuliotemwa baada ya wajakazi – mama zetu – kusalitika na madume wenye nyumba?

La ajabu ni kwamba wanaume hao walifurahia tu jazba na mama zetu ila hawana haja kutangamana nasi tunaoitwa mbegu mbaya. Kama kweli tabaka zipo kutofautisha watu, mbona matajiri wakala raha na kuzaa na maskini?

Binadamu kwa kujaaliwa mengi na mema wamesahau kwamba mtu hachagui uzao wala ulezi, hachagui ufukara wala ukwasi. Sote tunazaliwa namna na jinsi moja.

Licha ya ukweli huu dhahiri, wanadamu wanaondokea kuchukiana na kubaguana kiasi kwamba wenzao walio chini darajani wanakosa thamani sisemi maana katika utandu wa mapenzi.

Iweje tofauti ziibuke miongoni mwa waja waliokopolewa kwa jinsi na namna moja? Sasa tumefika kiwango cha kusema hadharani kwamba tabaka moja haitoshi mboga wala kitoweo! Hebu niambieni nyie mnaosimamia kucha na hizo dhana za usawa!

Hata majanga kama ukame na njaa ndio vikwazo zaidi.

Wanaotoka kwenye maeneo yaliyokumbwa na uhaba wa maji na lishe wakaonekana kama watu waliokwama. Wazazi wanakataa katakata mabinti kuolewa maeneo hayo yanayokisiwa kukwama.

Tufanyeje akina sisi ambao urathi wetu ni ufukara miaka nenda miaka rudi?

Nani mwenye kutuona na kutufaa kimaisha? Tuolewe na tuoe nani? Hata tukipenda tunaambiwa waziwazi kwamba hatujatosha kitoweo! Tukipendeza tunazomewa na kukashifiwa kujipendekeza kusikotufaa! Ndio dunia ya usawa hiyo?

Wanaobagua wenzao wanasahau kwamba maisha, kama mto hufuata mkondo!

Licha ya kuzaliwa maeneo kavu na tambarare, kuna wanawake kwa wanaume waliojizatiti kubadili maisha na sasa ni watu mbele ya watu.

Isitoshe, wako vilevile watoto wa matajiri wenye bongo zisizoshika kitu! Mbona sasa kubaguana?

  • Tags

You can share this post!

FUNGUKA: Kipigo toka kwa mke hunikolezea mahaba!

USHAIRI WENU: Mtima wangu tulia

adminleo