Makala

KIKOLEZO: Oktobafest iliwapeleka na rieng

October 11th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na THOMAS MATIKO

WIKENDI iliyopita ilikuwa ya aina yake. Mji wa Nairobi hakukukalika kabisa.

Ikiwa wikendi ya kwanza ya mwezi Oktoba, ilikuwa ni kipindi ambacho kwa kawaida kote duniani mataifa huadhimisha sherehe ya Oktobafest.

Hizi huwa ni sherehe za bia ambapo kwa siku mbili za wikendi ya kwanza za mwezi huo, hadhira hujumuika kustaraabika. Wanaohudhuria sherehe hizi hupata burudani na aina mbalimbali za bia wanazozihusudu.

Kwenye sherehe za mwaka huu zilizofanyika pale Ngong Race Course, mambo kadhaa yalidhihirika waziwazi. Yaliyojitokeza ni ishara tosha kwamba sherehe za Oktobafest sio za mchezo mchezo. Na ndio mwanzo zimeanza kupata umaarufu mkubwa nchini. Haya ndio mambo matano yaliyojitokeza.

WAKENYA WANAPENDA KULA BATA

Licha ya hali ngumu ya kiuchumi na Wakenya wakikesha kulalamika kwenye mitandao ya kijamii, sherehe za Oktobafest zilichora taswira tofauti kabisa.

Mwanzo kulijaa hadi pomoni kiasi kwamba hungelipata sehemu ya kutema mate. Maeneo ya kuegesha magari na sehemu zingine za uwanja huo wa Ngong wenye ukubwa wa ekari kadhaa, yalijaa aina mbalimbali ya magari ungedhani pale palikuwa kiwanda cha kutengeneza au kuuza magari.

Umati uliohudhuria sherehe hizo ulikuwa zaidi ya watu elfu 3,000 licha ya kuwa kiingilio kilikuwa ni Sh1,000 ambacho kwa Mkenya wa kawaida, ni kiwango kikubwa mno.

WASANII WA BONGO, NIGERIA IMEKULA KWAO

Toka harakati za Play Kenya Music zilipoanza mwishoni mwa mwaka jana, mawimbi ya burudani yamebadilika kabisa.

Harakati hizo zilianzishwa na mwanamuziki Khaligraph Jones kupinga kuchezwa kwa miziki ya nje zaidi ya zile za nyumbani. Kipindi hicho miziki iliyokuwa ikitawala kwenye kumbi mbalimbali za burudani hapa nchini zilikuwa za kigeni na hasa za Kibongo na Nigeria.

Kutokana na hali hiyo, wasanii wa mataifa hayo waliishia kupata shoo nyingi tena za mara kwa mara zilizowalipa mamilioni ya pesa, kuja kutumbuiza hapa nchini. Kampuni kubwa kubwa nchini zilikuwa zikiwaalika vile vile kila zilipoandaa tamasha.

Hata hivyo harakati hizo zimebadilisha mkondo wa upepo kabisa. Miziki ya nje haichezwi sana kama zamani, nao wasanii wa nje hasa Bongo na Nigeria hawapati tena ulaji hapa nchini.

Ingelikuwa ni zamani, tamasha kama hiyo ya Oktobafest lazima ingemvuta msanii mkubwa kutoka mataifa hayo.

Kubadilika kwa upepo huo wa kimuziki kulidhihirika waziwazi kwani wasanii wote waliowaroga Wakenya walikuwa ni wazawa wa nyumbani. Jumla ya wasanii 33 wakiwemo Madijei walipata fursa ya kuroga Wakenya na hakika wengi waliridhishwa.

SIDIRIA ZINA KAZI YA ZIADA

Sio kawaida kuona msanii wa nyumbani akionyeshwa mapenzi makubwa na mashabiki hasa wa kike anapokuwa jukwani.

Kumewahi kuripotiwa kutoka sehemu zingine kuwepo kwa visa vya wasanii wa kiume kurushiwa chupi au sidiria na mashabiki wa kike wanapopagawishwa na utumbuizaji wao.

Kwenye Oktobafest, vichuna walivurugika na burudani waliyoitoa bendi ya Sauti Sol na hasa Bien Baraza.

Visura watano hivi waliishia kuvua sidiria zao na kumtupia jukwani kuonyesha ni kiasi gani wanavyomkubali. Naye alijibu mapigo kwa kuamua kuzivaa na kuendelea kutumbuiza. Kisanga hichi kilikuwa thibitisho tosha kwamba wasanii Wakenya nao wana uwezo wa kutoa burudani kubwa.

SAUTI SOL, NYASHINSKI WAKALI WA LIVE BAND

Mgala muue lakini haki yake mpe. Kiuhalisia, kila msanii aliyepata fursa ya kutumbuiza alijitahidi. Japo wasanii wengi waliamua kutumbuiza kwa staili ya ‘playback’, yaani kuimba nyimbo zao wakati zikiwa zinachezwa na DJ, Sauti Sol na Nyashinski walikuja na levo tofauti kabisa. Ndio wasanii pekee walioonyesha uwezo mkubwa na wa kipekee wa kutumbuiza na live band bila ya kutatizika.

VIJANA WAACHE MIHADARATI

Stevo Simple Boy alipata umaarufu mkubwa kutokana na kauli hii ambayo ni mshororo kwenye wimbo wake ‘Mihadarati’.

Kwa hakika, pamoja na utani aliofanyiwa, pana haja ya kuwepo na uhamasishaji dhidi ya utumizi wa mihadarati miongoni mwa vijana.

Licha ya tamasha hiyo kuwa ya bia, kulikuwepo vile vile na misokoto ya kutosha ya bangi japo imeharamishwa. Vijana wengi walikuwa wakivuta bangi kwa starehe zao bila ya usumbufu.