KIKWAPA: Mbinu za kuondoa harufu mbaya makwapani
Na MARGARET MAINA
KIKWAPA ni mnuko utokao makwapani.
Vijana wanapofikia umri wa kubalehe, moja kati ya dalili wanazokumbana nazo ni kuota nywele makwapani.
Wengi wao wamekuwa wakishindwa kudumisha hali ya usafi hivyo kujikuta wakitoa harufu kali ya jasho.
Jambo hilo huwakwaza watu wengi na hivyo kujikuta wakijitenga au wakitengwa bila kujua sababu.
Kunuka kwapa ni tatizo kubwa katika mwili wa binadamu.
Tatizo hili husababishwa na bakteria wanaovutiwa na jasho au unyevunyevu chini ya kwapa.
Zifuatazo ni mbinu za kuondoa mnuko au kuzuia harufu mbaya kwapani:
Baadhi ya watu hutumia njia za kisasa ambazo ni pamoja na kupaka deodorant au marashi yanayosaidia kuondoa harufu mbaya mwilini.
Kuna njia za asili zinazoweza kuzuia harufu ya kwapa na ambazo ni pamoja na kutumia kipande cha limau kwenye kama sponji kupaka kwapa na kuacha kwa muda.
Kuvaa nguo safi zenye nyuzinyuzi za asili kama pamba na sufi kutasaidia kufyonza unyevu na kuacha kwapa lako kuwa kavu, safi na bila harufu mbaya.
Kuoga kila siku na kusafisha nguo kwa kutumia maji safi kunasaidia kuua bakteria ambao husababisha harufu mbaya.
Pia kunywa maji mengi kila siku kunakusaidia kutoa sumu mwilini na hivyo kupunguza harufu mbaya ya kwapa.
Njia nyingine inayoshauriwa ni kuhakikisha kuwa unaosha kwapa mara kwa mara kwa kutumia sabuni yenye dawa (medicated soap).
Kupunguza kula chakula chenye viungo vingi hasa vitunguu ni hatua nzuri pia. Inasemekana kuwa kula vitunguu vingi kunachangia mwili kutoa harufu kali.
Licha ya kwamba marashi na deodorant husaidia kuondoa harufu mbaya mwilini, hii si hatua endelevu kwani baada ya muda, harufu inaweza kurudi palepale. Hivyo ni vema kutumia njia za asili kukabiliana na hali hiyo.
Baada ya kuoga, jifute kwa taulo au kitambaa safi na usiache unyevu ambao huwavutia bakteria kukua katika maeneo yaliyojificha (yenye mikunjo).
Jitahidi kunyoa nywele za kwapa mara kwa mara na kuepuka kukaa kwa muda uliopindukia katika sehemu zenye joto kupita kiasi.