Kilichofanya Matiang’i kuondolewa adhabu ya kukaidi korti
Aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i amepata ushindi baada ya Mahakama ya Rufaa kubatilisha faini ya Sh200,000 aliyotozwa miaka saba iliyopita kwa tuhuma za kushindwa kumwachilia huru wakili Miguna Miguna alivyoagizwa na mahakama.
Mahakama ya Rufaa pia ilibatilisha faini kama hiyo kwa aliyekuwa Katibu wa Uhamiaji, Gordon Kihalangwa, na Mkuu wa Polisi wa zamani, Joseph Boinett, waliopatikana na hatia ya kukaidi mahakama kwa kutomwachilia Dkt Miguna bila masharti walivyoagizwa na Mahakama Kuu mnamo Machi 2018.
Majaji Wanjiru Karanja, Lydia Achode na Joel Ngugi walisema kuwa Mahakama Kuu iliwaadhabu bila kufuata taratibu rasmi za ombi la kukaidi mahakama.
Majaji hao pia walisema hakuna kinachozuia Dkt Miguna au mtu mwingine mwenye mamlaka kuwasilisha ombi rasmi la kuhusu jambo hilo katika Mahakama Kuu ambalo litasikilizwa na kuamuliwa kisheria.
“Rufaa inakubaliwa kwa sababu Mahakama Kuu iliwaadhibu kwa kukaidi mahakama bila ombi rasmi na taratibu za haki za kusikilizwa,” walisema majaji.
Dkt Miguna aliwasilisha kesi Februari 2018 akitaka kuachiliwa huru na serikali imsaidie kuingia nchini.
Wakili huyo alishtaki serikali kwa tuhuma za kumzuia kurudi nchini alipofika Uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA) Machi 26, 2018.
Alidai alikamatwa na stakabadhi zake za kusafiri kutwaliwa na washtakiwa walijaribu kumtimua nchini. Hatimaye alitimuliwa nchini na pasipoti yake ya Kenya kufutwa.
Lakini kabla ya hapo, alisema alizuiliwa bila mawasiliano ndani ya Terminal 2 katika JKIA, jambo lililokiuka haki zake.
Jaji Roselyn Aburili aliagiza aachiliwe huru.
Kesi iliwasilishwa mbele ya Jaji George Odunga (sasa jaji wa Mahakama ya Rufani) aliyeagiza serikali itekeleze maagizo ya mahakama.
Serikali ilidai Dkt Miguna alikuwa na pasipoti ya Canada na alikataa kuonyesha kwa maafisa wa uhamiaji.
Mahakama ilielezwa Dkt Miguna alitaka atumie kitambulisho cha taifa, na alizuiliwa kama mtu asiyekuwa na stakabadhi kusubiri suala hilo kusuluhishwa.
Jaji alitaka maafisa hao watatu wafike mbele yake kueleza sababu za kutoadhabiwa kwa kukiuka maagizo ya mahakama.
Hawakujitokeza na Jaji Odunga aliwaadhibu kwa kuwatoza Sh200,000 kila mmoja, fedha hizo ambazo zingekatwa kutoka mshahara wao wa mwezi uliofuatia.
Katika rufaa, maafisa hao walilalamika jaji aliendesha kesi kwa maombi ya mdomo badala ya maombi rasmi ya kukaidi mahakama. Pia walisema walinyimwa haki ya kusikilizwa na mahakama ilikuwa imetoa maagizo ambayo hayakuweza kutekelezwa kwa sababu ya tabia ya Dkt Miguna uwanjani.
Mahakama ya Rufaa ilisema hakukuwa na malalamishi rasmi yaliyowasilishwa kwa maafisa hao kwa mujibu wa taratibu.
“Kwa maoni yetu, kwa hali hii, njia bora na ya haki ilikuwa ni kutaka maombi rasmi ya kukaidi mahakama yaliyoambatishwa hati ya kiapo na kusikiliza pande zote kabla ya kutoa adhabu au maagizo,” walisema majaji.