Kilimo asilia kinavyopigwa jeki na bayogesi
WALIPOANZA mwaka wa 2011, hawakuwa na mpango wa kujihusisha na kilimo.
Haja yao kuu ilikuwa kutumia uchafu kutoka masokoni kuunda gesi na kusafisha mazingira.
Lakini kadri muda ulivyozidi, pakatokea haja ya kuzamia kilimo asilia. Hii ilichochewa na malighafi wanayotumia katika uzalishaji wa gesi.
Taka kutoka sokoni zimekuwa zikichakatwa na Shirika la Biogas International System kutengeneza bayogesi huku mabaki ya malighafi yanayotumiwa yakiwa muhimu katika kustawisha kilimo.
Hapo ndipo wasimamizi wa kampuni hii waliamua kuanzisha kitengo cha Flexi Biogas Organic Demo Farm kwa ajili ya zaraa.
Sasa, ni mwaka mmoja tangu meneja wa kitengo hiki Samuel Ndolo Mutua kuanza kukita vijishamba vya kisasa kukuza mboga kutumia mbolea asili.
Katika moja ya mashamba eneo la Mathaithi Junction, lililoko umbali wa kilomita mbili kutoka mji wa Karatina, Kaunti ya Nyeri, kumezagaa vijishamba ghorofa (vertical gardens) vyenye mboga zilizonawiri.
Mutua anasema kuwa walianza shamba la majaribio katika kipande cha thumuni ya ekari mwaka wa 2023.
Walipata motisha walipoona mazao yananawiri na wateja wanamiminika shambani kwa hivyo ikabidi wazidishe ukubwa wa shamba hadi robo ya ekari.
“Baada ya utafiti wa muda, Ilituchukua miezi sita ya kuzamia kilimo hiki. Hapo tukajua kuwa mashamba haya ni matimbo ya dhahabu,” Mutua aliambia Akilimali. “Ndiyo sababu tulipanua shamba na kuongeza mazao.”
Mazao safi
Kulingana na Mutua, mbolea kutoka kwa mfumo wa bayogesi imewasaidia sana kuhakikishia wateja kuwa wanaweza kupata chakula bila kemikali hatari kwa afya.
Imani hiyo kutoka kwa wateja wa viunga vya mji wa Mathaithi hadi mji wa Karatina, imewapa motisha zaidi ya kuendeleza kilimo hai na teknolojia.
“Ni vyema kuona kuwa tunatumia ‘uchafu’ kutoka kwa chakula kutengeneza chakula na bidhaa nyingine muhimu,” Mutua anasisitiza. “Ni rahisi kuamini kuwa tunachopata kutoka kwa mashamba haya, ni bidhaa za kuaminika na kutegemewa kuboresha afya na masuala mengine katika jamii likiwemo uchumi.”
Mashamba ghorofa
Mifumo ya kukita vijishamba vidogo vyenye kubeba mazao mengi imekuwa muhimu sana katika kipindi ambacho ardhi inakuwa finyu kwa sababu ya ustawishaji wa miji.
Mutua anaonea fahari sana hatua yao ya kukumbatia mashamba haya katika vipande vidogo vya ardhi.
Anaarifu kuwa tangu waanze kutumia bustani za jikoni (kitchen gardens), wameweza kuzidisha uwezo wa mashamba madogo kuzalisha mazao mengi.
“S hayo tu. Mashamba haya yanasaidia kwa sababu hatuhitaji kuwa na wafanyakazi wengi,” anasema Mutua akiongeza vijishamba hivi havihitaji kulimwa sana na hata kupaliliwa.
Kadhalika, mbinu hii ya kilimo imewaepushia na changamoto za kukabili vimelea na magonjwa.
“Hii imechangiwa na jinsi vijishamba hivi vimeinuliwa juu ya ardhi kuepuka wadudu hatari ambao hutambaa juu ya udongo ama chini yake,” anafichua huku akieleza kuhusu mfumo wa unyunyizaji kutumia mifereji miembamba ambayo inapunguza matumizi mengi ya maji bila lazima ya mfanyakazi kuwa hapo.
Mimea inayokuzwa
Shambani Flexi Biogas Demo Farm mna mazao kama vile Sukuma wiki, spinach, kabeji, mchicha na mengine.
Mutua anashauri familia zinazomiliki mashamba madogo kukumbatia mifumo hii ya kilimo kujikuzia mboga zao wenyewe.
“Huwa tunatoa mafunzo ya mbinu bora za kujenga bustani za jikoni,” anasema. “Tangu tuanze, hatujakuwa na haja ya kujipigia debe kwa kuwa wateja wetu wamekuwa wakiwaleta wengine.”