KILIMO BIASHARA: Covid-19 yaharibu faida ya wakulima wa machungwa
Na SAMMY WAWERU
MANDHARI yanayokulaki katika shamba la Aaron Ndisya Muthini ni michungwa iliyozaa machungwa yanayoning’inia kwa uzuri kwenye matawi yake.
Ni mkulima mahiri wa machungwa maalum aina ya pixie Kijiji cha Muthyoi, Nziu Kaunti ya Makueni. Eneo hilo ni maarufu katika uzalishaji wa machungwa aina ya pixie, Washington navel, chenza (sandara) na pia tangelo.
Shamba la mkulima huyo lenye ukubwa wa ekari tano, ekari tatu anakuza pixie. Kati ya ekari hizo tatu, moja ndiyo inazalisha, akidokeza kwamba anaendelea kupandikiza matawi ya pixie kwenye mindimu aliyopanda katika ekari mbili na miaka michache ijayo itaingia katika orodha ya michungwa inayompa mapato.
“Ekari moja inayozalisha ina jumla ya michungwa 250, japo 80 ndiyo ina matunda yaliyokomaa kila mti nikikadiria utanipa kati ya pixie 60 – 90,” Ndisya anafichua.
Huu ukiwa msimu wa kwanza mwaka huu, ambapo kila mkulima eneo hilo anaendelea kufanya mavuno, mkulima huyu ana wasiwasi huenda akapata pigo kufuatia athari za Covid – 19, janga la kimataifa ambalo limehangaisha sekta mbalimbali, kilimo ikiwemo.
Michungwa inayotunda ni maridadi na inayoleta tabasamu kwa anayeitazama, ila kwa mkulima huyu tabasamu imefifia.
Ni mwaka wa tano tangu Ndisya, 28, aingilie kilimo cha pixie, lakini anasema hajawahi kushuhudia nyakati ngumu kama za kipindi hiki cha janga la Covid-19.
Mwanazaraa huyu ambaye 2019 baada ya kuhitimu Shahada ya Masuala ya Kilimo kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Meru, alijiajiri kupitia shughuli za kilimo, anasema wateja wake wengi wanatoka masoko ya Nairobi.
Mikakati na sheria zilizowekwa kuzuia msambao wa Covid-19, ugonjwa unaosababishwa na virusi vya corona, hususan zuio la kuingia na kutoka Nairobi na viunga vyake (ingawa liliondolewa) na kibali cha wasafarishaji mizigo, Ndisya anasema imeathiri kwa kiasi kikuu soko la mazao yake.
Kufikia sasa, amefanya mauzo jumla ya tani 1.3 sawa na kilo 1,300
“Nakadiria mazao yaliyosalia shambani ni tani 1.5 nikiwa na wateja wawili pekee. Vizuizi vya barabara na kupata leseni kusafirisha mizigo, imekuwa kikwazo kikuu kwa wakulima kupeleka mazao sokoni au wateja kuyajia shambani. Pixie zikikomaa, zinadumu mtini kipindi cha miezi miwili, nahofia kufikia Agosti 2020 ikiwa sitakuwa nimepata wateja huenda nikakadiria hasara. Wasiwasi wangu pia unagubika wakulima wenza,” Ndisya anafafanua, akiongeza kusema kuwa wengi wa wateja wake wanatoka Nairobi.
Mazao yaliyoko shambani alianza kuvuna Mei 2020, na anaeleza kiangazi kikibisha hodi matunda yataanza kunyauka, kupoteza juisi, ishara ya kuharibika.
Ndisya anaiambia Akilimali kwamba miaka ya awali, kama vile 2019, wakati kama huu mazao shambani huwa yameisha kufuatia ushindani mkali wa soko. “Wakati kama huu malori ya wateja hupiga doria yakitafuta machungwa. Kwa sasa mazao yangali shambani, hayana wanunuzi,” analalamika.
Isitoshe, anasema bei imekuwa duni, kiasi cha kukandamiza wakulima. “Kilo kwa bei ya jumla shambani ni kati ya Sh40 – 80. Kupata mnunuzi wa Sh80 kwa kilo, ni kwa neema ya Mungu. Mavuno niliyouza msimu huu yamenunuliwa kati ya Sh40 – 50,” anaelezea.
Wakati wa mahojiano Ndisya alisema mwaka uliopita kilo ilinunuliwa kati ya Sh100 – 150. Katika hotuba ya Rais Uhuru Kenyatta kwa taifa mnamo Jumatatu, Julai 6, 2020, ambapo alitangaza kuondoa zuio la kuingia au kutoka nje ya kaunti ya Nairobi, Mombasa na Mandera, Ndisya ni mwingi wa matumaini mazao yake sasa yatapata wanunuzi.
Alianza kilimo cha pixie akiwa mwaka wa kwanza chuo kikuu 2015 na ambapo ilimgharimu mtaji wa Sh25,000 kuzalisha machungwa haya ya aina yake kwenye shamba lenye ukubwa wa ekari moja.
Mazao ya kwanza, 2018, anasema alifanya mauzo jumla ya Sh20, 000 pato hilo likiashiria alikadiria hasara. Anasema hakufa moyo, na msimu wa mavuno ya pili alitia kibindoni kima cha Sh62,000
Kwa mwaka, pixie ina misimu miwili ya mavuno.
“Baada ya kuvuna, huanza kulisha michungwa ya pixie kwa maji na mbolea na fatalaiza. Muhimu pia ni kufanya palizi kuzuia kwekwe,” Ndisya anasema.
Matunda anayoendelea kuvuna yakiwa yamefanikishwa na mvua iliyoshuhudiwa kati ya Machi – Mei 2020, mkulima huyu pia anasema hutegemea maji ya Mto Kyambui hasa wakati wa ukame. Ana jenereta la kupampu maji, alilonunua kupitia mapato ya kilimo.
Miti ya pixie inachukua kati ya miaka miwili hadi mitatu kuanza kuzalisha matunda. Changamoto sugu kwa machungwa haya ni magonjwa aina ya Citrus kanga na scale. Wadudu wanaoshuhudiwa ni pamoja na Fruit flies, thrips, white flies, red spider mites na avids.
Huku lengo la Ndisya likiwa kuwa na zaidi ya michungwa 2, 500, anasema mti uliokomaa na kutunzwa vyema unaweza kuzalisha wastani matunda 300 kila msimu.
Soko likimkubali, aghalabu Sh100 kwa kilo, ina maana kuwa barobaro huyu anaweza kupokea mapato yasiyopungua Sh75,000 kila msimu, sawa na kima cha Sh150, 000 kwa mwaka, hatua itakayomuingiza katika ligi ya mamilionea nchini.
Licha ya janga la corona kutishia kuzima ndoto zake, Ndisya anasema ni kwa muda tu anahangaika. Anatumia mitandao ya kijamii kama vile Facebook na WhatsApp kutafutia mazao yake soko, ambapo wateja wawili wanaoyanunua aliwapata kupitia mitandao.
Ili kukwepa kero la soko, Steven Mwanzia mtaalamu wa masuala ya kilimo anashauri wakulima kukumbatia mfumo wa kuongeza mazao thamani, kama vile kuunda sharubati itokanayo na matunda. “Mazao yakiongezwa thamani, kwa kuunda bidhaa zitokanazo nayo, thamani ya bei pia inaongezeka,” Mwanzia anaelezea.
Kulingana na mdau huyo, soko halitakuwa kikwazo kwa sababu pia yataweza kuhifadhika kwa muda ili kutafuta wateja.
“Kiwanda cha kuongeza thamani matunda kilichoko Makueni ni cha kutengeneza sharubati ya maembe pekee. Kwa niaba ya wakulima wenza, ninahimiza serikali ya kaunti chini ya Gavana Prof. Kivutha Kibwana kuzindua cha kuunda juisi itokanayo na machungwa ili tuepuke vikwazo na hasara tunayokadiria,” Ndisya ambaye pia mtaalamu wa masuala ya kilimo anarai.
Ni muhimu wakulima wajiunge na vyama vya ushirika, Sacco, vilivyosajiliwa na pia makundi, miungano ambayo ni rahisi kufikia serikali iwasaidie kupata soko la mazao nje ya nchi.
Mbali na kukuza pixie, Ndisya pia ni mkulima wa sukuma wiki, spinachi, nyanya na matikitimaji.