Kilimo cha kuzalisha mapapai
Na SAMMY WAWERU
SHAMBA la Bw Steven Macheru lilikoko kijiji cha Kiangoma, Kaunti ya Nyeri limesitiri matunda aina mbalimbali kama vile ndizi, matunda damu (tree tomato), maparachichi, mapapai, maembe na karakara.
Udongo katika eneo hilo ni ule mwekundu maarufu kama ‘red loam soil’.
Kwa jumla, Nyeri ni mojawapo ya kaunti zinazofahamika nchini katika uzalishaji wa matunda na mboga kwa wingi.
Kinachovutia zaidi katika shamba la Mzee Macheru ni miti kadhaa ya mapapai. Ni michache tu na kulingana naye kilimo cha matunda hayo ni chenye tijara kuntu.
“Mapapai ni miongoni mwa matunda yasiyokosa soko. Hayana ugumu kuyakuza, ikiwa ni pamoja na gharama ya chini kuzalisha,” aeleza mwalimu huyu mstaafu.
Anasema alianza kuyapanda miaka ya 70, na kwamba yamemfaa pakubwa kulea watoto wake, ambao kwa sasa wana familia zao.
Mapapai hutunda miezi sita baada ya upanzi. Aidha, kilo moja haipungui Sh40.
Mapapai ni baadhi ya matunda yanayopendekezwa kulishwa watoto hasa wanaoendelea kunyonya.
Yamesheheni Vitamini C. Pia, ni kiini kizuri cha madini kama Magnesium, Iron na Copper.
Madini mengine yanayopatikana katika mapapai ni Manganese, Calcium, Phosphorus na Zinc.
“Matunda haya hayana asidi na ndio maana yanapendekezewa watoto. Wenye shida ya asidi pia wanahimizwa wayale kwa wingi,” aeleza Juliet Wanga, mtaalamu wa masuala ya afya.
Mbali na Nyeri, maeneo mengine tajika katika uzalishaji wa mapapai ni Embu, Meru, Kiambu na Kirinyaga.
Harrison Mbachia, mkulima wa matunda haya Kiambu, anasema kazi ni kuandaa shamba, kuyapanda na kuyatunza kwa maji. “Nilianza kilimo cha mapapai 2017 na kamwe sijutii kuyakuza. Hakifanyi mkulima mtumwa baada ya kuyapanda kwani hayana kazi za sulubu,” asema Bw Mbachia.
Kulingana na wataalamu wa masuala ya kilimo, mapapai yananawiri maeneo yenye udongo mwekundu na pia ule wa kufinyanga.
Mipapai – mimea inayoyazalisha, hupandwa kwenye kitalu kwa muda wa miezi miwili na nusu ili kupata miche.
Julius Nduati kutoka African Soil & Crops Care Ltd, shirika la kibinafsi linaloshughulikia masuala ya udongo na miche anasema kiasi kikubwa cha miche ya mipapai inapaswa kuwa ya kike.
“Mipapai ya kiume iwe michache ili kujamiisha ile ya kike, shughuli hii husaidia na upepo,” aeleza Bw Nduati. Inapendekezwa ya kike isiwe chini ya asilimia 95.
Upanzi wake ni sawa na wa matunda mengine.
Michungwa, miembe na migomba ya ndizi huhitaji makoongo yenye kimo futi moja, na upana wa karibu futi mbili.
Kipimo cha nafasi ya mashimo kiwe mita 2.5 mraba.
Upandaji kwa kutumia mboleahai yaani kinyesi cha mifugo na kuku, ndiyo inapendekezwa.
“Changanya udongo na mbolea sawasawa, halafu upande miche yake. Kazi inayosalia ni kuitunza kwa maji, mbolea na palizi,” aeleza Bw Nduati.
La kutia moyo katika kilimo cha mapapai ni kwamba nafasi kati ya mipapai, mkulima anaweza kukuza maharagwe. Aidha, maharagwe ni kiini kizuri cha madini ya Nitrojini ikiwa ni pamoja na kudumisha rutuba udongoni.
Magonjwa kwa mapapai ni Pawpaw ring virus na Bacterial wilt. Wadudu wanaoshuhudiwa nu vithiripi. Mkulima anashauriwa kupata maelekezo maalum kutoka kwa mtaalamu au wataalamu ili kukabiliana na changamoto za magonjwa na wadudu.
Hata hivyo, mkulima akizingatia mfumo asilia, changamoto hizo zitadhibitiwa.