Makala

Kilimo cha pilipili hoho na nyanya kinalipa

August 24th, 2020 Kusoma ni dakika: 4

 

NA RICHARD MAOSI

Changamoto kubwa inayoweza kuwakumba vijana wenye ari ya kuanzisha miradi ya kilimo, ni ukosefu wa mtaji wa kutosha pamoja na ujuzi finyu wa kitaaluma, wakati wa kutafuta soko la ndani na nje ya nchi kwa mazao yao.

Licha ya hayo Ayub Otieno 20, ni kielelezo cha kuigwa, akiwa mwanafunzi wa uhandisi(Software Engineering) mwaka wa tatu kutoka Chuo Kikuu Cha KCA Nairobi, ameamua kujitosa kwenye kilimo kipindi hiki cha mkurupuko wa Covid -19, ili ajiongezee kipato.

Bidii ya mkulima huyu imempatia tija ya muda mrefu akiamini kuwa siku moja atakuja kushinda tuzo kama mkulima bora mwenye umri mdogo kote nchini.

Aidha anajisomesha shahada ya pili Data Science katika chuo kikuu cha Strathmore kutokana na faida anayotengeneza kutokana na kilimo cha pilipili hoho, nyanya na mboga za michicha ndani ya nyumba ya kioo.

Akilimali ilimkuta katika mtaa wa Lanet, kilomita 16 hivi kutoka mjini Nakuru akiendelea kupulizia pilipili hoho msimu huu wa mvua rasharasha, na bila shaka mazao yake yamestawi vizuri kwa vile maji yanapatikana kwa wingi.

Anasema alianza mradi huu kwa sh 200,000 kutengeneza nyumba ya kwanza ya kioo na kisha 300,000 kujenga nyumba ya kioo ya pili.

Katika kipande cha ardhi cha ekari mbili Ayub amatengewa sehemu ya ukulima na kufikia mwaka huu amefanikiwa kusimamisha nyumba ya kioo ya pili kila mmoja ikiwa ya kimo chenye mita 8 kwa 30 mstatili.

Alianza kilimo kwa mtaji wa 200,000 akiwa na miaka 20, hii ni baada ya wazazi wake kumsaidia kupata mkopo uliomsaidia kutengeneza nyumba ya kwanza ya kioo kukuza nyanya na hatimaye pilipili hoho.

Alieleza kwa wiki moja huvuna kilo 20 ya pilipili hoho ambapo kilo moja huuzwa baina ya 150-200, na wanunuzi wengi ni wamiliki wa maduka ya kijumla kama Gilanis na Woollmatt mjini Nakuru.

Hata hivyo anasema kwa sababu bado alikuwa mchanga alijiongezea tajriba ya ukulima kwa kuhudhuria makongamano ya wakulima na kufanya utafiti kuhusu soko la bidhaa anazokuza, ikizingatiwa kuwa Lanet ni eneo kame hivyo basi ukulima unahitahi maji ya kutosha.

Kwa wiki moja anaweza kuvuna pilipili hoho kati ya kilo 20-25 ambapo kilo moja ni 200.

Ndani ya nyumba ya kioo alitengeneza mbinu ya kunyunyiza almaarufu kama Drip irrigation, kisha akanunua mihimili ya kusimamisha matawi ya nyanya, vyuma vya kuezeka paa na kulipa vibarua waliosimamisha mradi wake wa nyanya.

Ingawa anasema kuwa changamoto kuu ya kukuza nyanya ni uharibifu kutokana na wadudu wanaofahamika kama white flies, ambao mara nyingi hushambulia mimea ikiwa changa shambani.

Pili fuko wasumbufu wana mazoea ya kutafuna mizizi ya nyanya nyakati za usiku, na endapo mkulima hatakuwa makini kuangalia mimea yake kila wakati anaweza kuambulia hasara kubwa.

Anasema kuwa ikiwa mimea haina maji ya kutosha katika mizizi yake inaweza ikaanza kukunjika na isitoshe madini ya kutosha kama vile Calcium hufanya mimea ikaanza kupoteza rangi yake ya asilia na kupata rangi nyeusi.

Hata hivyo mradi wa nyanya mnamo 2018 ulifanya vyema na kumsukuma kwenye mradi wa pili wa kutengeneza nyumba ya kioo ambapo ilimgharimu 300,000 kuanziasha mradi wa pilipili hoho.

Kwa ujumla ametumia nusu milioni, na kulingana naye mara ya kwanza safari haikuwa rahisi ikizingatiwa alijitosa katika ukulima mara tu baada ya kuhitimisha masomo ya shule ya upili.

Ayub anasema kwanza alinunua mbegu kutoka kampuni ya Amiran zilizoidhinishwa na serikali,ambapo yeye hukuza hoho za rangi nyekundu, kijani kibichi na samawati.

Anasema pilipili hoho huwa na faida nyingi ikilinganishwa na nyanya za kawaida ikizingatiwa kuwa soko lake ni la uhakika na huchukua muda wa kati ya siku 70-90 kukomaa.

“Zoezi la kwanza ni kufanya uchunguzi wa hali ya anga kabla ya kuongeza virutubishi vingine kama vile mbolea ya kuku na sungura, kutajirisha mchanga”asema.

Alieleza kuwa hoho hupandwa sentimita 16 hivi kutoka kwenye mmea mmoja hadi mwingine, hii ni baada ya kuamishwa kutoka kwenye kitalu na kusafirishwa hadi kutoka kwenye nyumba ya kioo, baada ya kukamilisha siku 14.

Anasema kuwa maji yalikuwa yakipatikana kwa sababu ya kisima cha borehole ambacho kinapatikana katika boma lao, maji haya yanaweza kusukumwa na mtambo wa petroli hadi ndani ya matanki ya lita 1800.

Pili anasema kuwa drip irrigation ni mwafaka kwa sababu ni nafuu, kinyume na aina nyingine ya unyunyizaji kwa sababu hutumia kiwango kidogo cha maji, huku kila mmea ukipata maji ya kutosha.

Ayub anasema mara tu baada ya kuhitimisha nyumba ya kioo ya pili alitengeneza mihimili ya mbao ambayo husaidia pilipili hoho kuegemea kutokana na uzito wa matunda yake, baada ya miezi mitatu ya kukomaa.

“Nilijifunza kukuza pilipili hoho katika maonyesho ya Kilimo ya Nakuru ASK, na baadae nikatengeneza tovuti yangu binafsi katika mtandao wa kijamii ili kuwavutia wanunuzi, na kuwafaa wakulima wadogo mashinani”akasema.

Aliwatembelea wataalamu wa mimea ambao walimsaidia kuchunguza aina ya pilipili hoho ambazo zinaweza kufanya vyema katika maeneo kame ya Lanet.

“Kabla ya kusafirisha miche ya pilipili hoho kutoka kwenye kitalu inampasa mkulima akome kuzinyunyizia maji ili ziweze kuzowea hali ngumu katika mazingira mapya, yenye maji kidogo”aliongezea.

Ayub anaongezea kuwa yeye hukata matawi ya pilipili hoho kila baada ya wiki mbili ili kutoa nafasi ya mimea kutumia maji kidogo na kupunguza uwezekano wa wadudu kuvamia miea.

Uzuri wa kupunguza matawi ni kwa sababu hukosesha wadudu sehemu za kujificha wengi wao wakiwa ni aphids na whitefly.

Aidha mkulima anaweza kuondoa matunda ambayo yameanza kuoza au yale yaliyo madogo kupita kiasi ili aweze kukuza pilipili hoho zenye kimo sawa na rangi iliyokolea vizuri.

Kando ya mradi wa pilipili hoho Ayub anakuza Lettuce ambayo hutumika kutengeneza kachumbari.

Lettuce ni aina ya mboga ambayo huchanganywa na nyanya, kitunguu na pilipili na wakati mwingine inaweza kuliwa na mkate.

Manufaa ya kutumia pilipili hoho ni kama vile kunogesha ladha ya chakula, kupunguza shinikizo la damu mwilini na kutoa ajira kwa wakulima wanaojihusisha na kilimo biashara.

Hata hivyo anawashauri wakulima kutumia mbegu za F1 generation ili aweze kufaidika na mimea yake kwa muda mrefu, akitaja kuwa wakulima wengi hukosea pale wanapotumia mbegu za F2 generation