Makala

Kilimo cha sukumawiki

June 5th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMMY WAWERU

UKIZURU mengi ya maboma hutakosa kuona mboga ya kijani.

Katika makazi mengi nchini, mboga aina ya sukumawiki ndiyo hukuzwa kwa wingi kwani inapendwa na idadi kubwa ya watu.

Inakadiriwa kuwa hupandwa na zaidi ya asilimia 90 ya Wakenya, mashambani na hata mijini.

Mboga hii imesheheni Vitamini C, K na kiini kizuri cha Beta Carotene.

Aidha, ni kitoweo kizuri cha ugali; mchanganyiko wa unga wa mahindi na maji moto, uliopikwa ukapikika barabara.

Kuna aina mbalimbali za sukuma wiki kama; Sukuma siku Hybrid, Marrow stem na Thousand headed.

Pia kuna Collard Southern Georgia na Collard Mfalme F1.

Kulingana na wataalamu wa kilimo na wakulima wenye uzoefu wa kukuza sukumawiki, ni miongoni mwa mboga rahisi kupanda na kutunza.

Sukumawiki inastawi katika udongo usiotuamisha maji na wenye ukwasi wa rutuba. Wataalamu wanahoji inahitaji kupandwa kwa mboleahai; ya kienyeji.

“Kiwango cha asidi ya udongo, pH inapaswa kuwa kati ya 6.0-7.5. Pia, kiwango cha alkalini kiwe cha chini,” anashauri Caroline Njeri, mtaalamu kutoka Safari Seeds.

Kitaalamu, shamba linalokuzwa mboga linapaswa kulimwa wiki 2 au tatu kabla ya upanzi. Bi Njeri anasema hili litawezesha makwekwe kukauka.

“Makwekwe mabichi husambaza magonjwa na wadudu. Yaliyokauka hayana magonjwa na zaidi ya yote ni mbolea na huongeza rutuba kwenye udongo. Pia, yanapopewa muda kukauka wadudu huaga, wengine kutoroka na kuliwa na ndege,” aelezea mdau huyu.

Kulingana na Njeri, linapaswa kuchimbwa hadi futi mbili kuenda chini ili kuruhusu mizizi ya sukuma wiki kupenyeza.

Apollo Maina ni mkulima wa mboga hii eneo la Kigumo kaunti ya Murang’a na anasema hutandaza sehemu inayopandwa na hata kuiinua kwa udongo ili kutengeneza muundo wa ‘kitanda’.

Andaa mashimo, yenye kipimo cha urefu wa sentimita 60 kutoka shimo moja hadi lingine. Pia, nafasi ya laini ya mashimo hadi nyingine iwe ya sentimita 60.

“Weka mbolea kwenye mashimo halafu uchanganye na udongo uliotolewa mashimoni, rejesha mchanganyiko huo,” aelekeza Bw Maina.

Miche ya mboga huchukua muda wa kati ya wiki 4-6 hivi kuwa tayari kwa upanzi.

Unashauriwa kufanya uhamisho wa miche majira ya jioni au wakati anga ina mawingu. Miale kali ya jua hufisha miche.

Kitalu (inakokuziwa miche), kimwagiliwe maji saa moja kabla ya kung’oa mimea hiyo michanga.

Wataalamu wanahimiza mashimo yamwagiliwe maji kiasi kisha miche ya sukuma wiki ipandwe na kumwagiliwa maji tena.

Maji ni kiungo muhimu kwa mimea, na iwapo mvua hainyei inapaswa kunyunyuziwa aghalabu mara mbili kwa siku yaani asubuhi na jioni.

Ili kuzuia uvukizi wa maji, mkulima anashauriwa nafasi iliyo kati ya mboga nyasi za boji (mulching) ziwekwe hasa msimu wa kiangazi.

Upaliliaji

Hatua nyingine muhimu katika kilimo cha sukumawiki ni upaliliaji.

Caroline Njeri, mtaalamu, anasema makwekwe yasipodhibitiwa huleta ushindani mkali wa lishe; maji na mbolea, vilevile mwangaza na nafasi ya majani kunenepa.

“Palizi pia hupunguza kasi ya usambaaji wa magonjwa na wadudu,” anadokeza Bi Njeri.

Ili kustawisha mazao na kuyaongeza, unapendekezwa kutia kwenye shina la sukuma wiki mbolea ya kisasa.

Magonjwa yanayoathiri mboga ni: black rot, alternaria leaf spot, anthracnose, na downy mildew.

Nematode, cabbage looper, viwavi, diamondback moth, vidukari, flea beetles na vithiripi, ndio wadudu wanaoshambulia sukumawiki.

Mboga hii huanza kuvunwa mwezi mmoja baada ya upanzi.